05. Sababu ya Allaah kuwatuma Mitume na Manabii

2- Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Maana yake ni kwamba kumpwekesha Allaah (´Azza wa Jall) kwa ´ibaadah. Haya ni kinyume na kumpwekesha Allaah kwa kuumba, kuruzuku na kuendesha mambo. Sampuli hii maana yake ni kwamba kusiswaliwe, kusiombwe, kusichinjwe, kusiwekwe nadhiri, kusihijiwe, kusifanywe ´Umrah, kusitolewe swadaqah na aina nyenginezo za ´ibaadah kwa ajili ya mwengine asiyekuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Mivutano ilitokea hapa kati ya Mitume na nyumati zao.

Hakukuwepo mivutano yoyote juu ya ile aina ya kwanza iliotangulia. Nyumati zote zilikiri kwamba Allaah ndiye Mwenye kuumba na Mwenye kuruzuku ambaye anahuisha na anafisha na anaendesha walimwengu. Hakuna ambao walipinga Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah isipokuwa viumbe waovu, lakini walipinga kwa uinje. Lakini kwa undani walikuwa ni wenye kuiamini. Fir´awn ni mmoja katika wao. Japokuwa kwa uinje alipinga uwepo wa Mola (Subhaanahu wa Ta´ala) na akasema:

أَنَا رَبُّكُمُ الْأَعْلَىٰ

“Mimi ni mola wenu mkuu.”[1]

Lakini kwa undani alikuwa ni mwenye kuyakinisha kwamba hakuwa mola mwenye kuumba na mwenye kuruzuku. Alikuwa ni mwenye kuamini kwa undani ya kwamba Allaah ndiye Muumbaji na Mruzukaji.

Kadhalika wakomunisti wa leo wanaopinga uwepo wa Mola. Hili ni kwa njia ya uinje. Vinginevyo kila mtu mwenye busara anatambua kuwa ulimwengu haukupatikani hivihivi pasi na muumbaji na mwenye kuuendesha. Kila mtu mwenye busara anatambua Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah.

Kuhusu Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah, ni wachache wanaoikubali. Hakuna wenye kuikubali isipokuwa tu waumini ambao ni wafuasi wa Mitume. Makafiri wengine wanaipinga. Hawamwabudu Allaah pekee hata kama wataikubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah na kumwabudu Allaah kwa aina kadhaa za ´ibaadah. Kwa ajili hii wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowaambia waseme ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah wakasema:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ

“Amewafanya waungu kuwa ni mungu Mmoja?  Hakika hili ni jambo la ajabu mno!”[2]

Walikataa kutamka kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, pamoja na kuwa wanakubali uola wa Allaah. Walikataa kukubali kwamba Allaah pekee ndiye Mwenye kustahiki kuabudiwa. Walikuwa wakisema kuwa wanamwabudu Allaah na wanawaabudu waombezi na wakati na kati wengine ambao walikuwa wakiona kuwa wanawakurubisha mbele ya Allaah. Hivyo wakawaabudu wakati na kati na wakakataa kumwabudu Allaah pekee. Walisema:

وَقَالُوا لَا تَذَرُنَّ آلِهَتَكُمْ وَلَا تَذَرُنَّ وَدًّا وَلَا سُوَاعًا وَلَا يَغُوثَ وَيَعُوقَ وَنَسْرًا

“Wakasema: “Msiwaache waungu wenu na wala msimwache Wadd na wala Suwaa´ na wala Yaghuuth na Ya’uuq na Nasr!”[3]

Kadhalika waabudu makaburi hii leo wanaambizana wao kwa wao wasiache kumwabudu al-Hasan, al-Husayn, al-Badawiy na wengineo. Wanaona kuwa wana fadhilah na wana vyeo na matokeo yake wanawachinjia, wanawawekea nadhiri, wanatukufu kwenye makaburi yao, wanatafuta baraka kutoka kwao. Wanashaji´ishana wao kwa wao kuendelea kushikamana na matendo haya na kutowasikiliza wale wanaowaita kuwa ni watovu wa adabu ambao wanapigana vita na kuabudiwa kwa makaburi na wasiotambua haki ya mawalii. Mtindo ni uleule kama watu wa Nuuh:

وَقَالُوا لَا تَذَرُنَّ آلِهَتَكُمْ وَلَا تَذَرُنَّ وَدًّا وَلَا سُوَاعًا وَلَا يَغُوثَ وَيَعُوقَ وَنَسْرًا

“Wakasema: “Msiwaache waungu wenu na wala msimwache Wadd na wala Suwaa´ na wala Yaghuuth na Ya’uuq na Nasr!”[4]

Hii ndio aina ya pili ya Tawhiyd, Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah, ambayo ni kumpwekesha Allaah (´Azza wa Jall) kwa ´ibaadah na kuacha kuabudu vyengine visivyokuwa Yeye. Hii ndio aina ya Tawhiyd ambayo Allaah, amewatumiliza Mitume na akateremsha vitabu. Nyinyi wenyewe mnasoma maneno Yake (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.”[5]

Hakusema kwamba amewaumba ili wakiri kuwa Yeye ndiye Mola, kwa sababu hiki ni kitu ambacho kipo tayari. Vilevile amesema:

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

”Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut [waungu batili].”[6]

Hakusema kwamba wamekuja ili wakiri kwamba Yeye ndiye Muumbaji na Mruzukaji, kwa sababu tayari walikuwa ni wenye kuyaamini. Lakini haitoshi. Washirikina walikuwa wakipinga aina hii ya Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Walikuwa ni wengi hapo zamani na hii leo. Walikataa kuwaacha waungu wao na kumwabudu Allaah (´Azza wa Jall) pekee. Yote haya kwa sababu walikuwa ni wenye kudai kwamba waungu wao ni wakati na kati na ni wenye kuwaombea mbele ya Allaah:

وَزَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ فَصَدَّهُمْ عَنِ السَّبِيلِ وَكَانُوا مُسْتَبْصِرِينَ

“Shaytwaan aliwapambia matendo yao akawazuia na njia, japokuwa walikuwa ni wenye kutambua vyema.”[7]

[1] 79:24

[2] 38:05

[3] 71:23

[4] 71:23

[5] 51:56

[6] 16:36

[7] 29:38

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 22-23
  • Imechapishwa: 07/08/2019