05. Radd kwa wenye kusema “Qur-aan peke yake inatosheleza”

Inasikitisha kuona ya kwamba kumepatikana baadhi ya wafasiri na waandishi wa sasa ambao wameonelea kujuzu kwa yale tuliyoyataja katika mifano miwili ya mwisho ambapo wamejuzisha kula wanyama mwitu [waliyoharamishwa], kuvaa dhahabu na hariri. Wamefanya hivo kwa sababu ya kuitegemea Qur-aan peke yake. Bali wamepatikana watu wanaojiita “Qur-aaniyyuun” ambao wanaifasiri Qur-aan kwa kufuata matamanio yao na akili zao pasi na wakati wa kufanya hivo kutaka usaidizi wa Sunnah Swahiyh. Kwa mujibu wao Sunnah ni yenye kufuata matamanio yao; yale yanayowafikiana nayo wanayafuata na yale yasiyowafikiana nao wanayatupilia mbali. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaashiria watu hawa pale aliposema katika Hadiyth Swahiyh:

“Asiwepo yeyote mwenye kulala juu ya kitanda chake akajiwa na amri miongoni mwa amri zangu katika zile nilizoamrishwa au kukatazwa akasema: “Sijui; yale tunayoyapata katika Kitabu cha Allaah tutayafuata.”

Ameipokea at-Tirmidhiy.

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Yale tutayoyapa [katika Qur-aan] kuwa ni haramu ndio tutayoharamisha. Tanabahini! Hakika mimi nimepewa Qur-aan na mfano wake pamoja.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Tanabahini! Hakika yale aliyoharamisha Mtume wa Allaah ndio mfano wa yale aliyoharamisha Allaah.”

Miongoni mwa mambo ya kusikitisha ni kuwa baadhi ya waandishi waheshimiwa wametunga vitabu kuhusu Shari´ah ya Uislamu na ´Aqiydah yake na wakataja mwanzoni mwa vitabu hivyo kuwa wametunga na hawana vyanzo vingine zaidi ya Qur-aan peke yake.

Hadiyth hii Swahiyh inafahamisha dalili ya kukata kabisa juu ya kwamba Shari´ah ya Kiislamu sio kufuata Qur-aan peke yake. Uhakika wake ni kufuata Qur-aan na Sunnah. Yule atakayeshikamana na kimoja wapo pasi na kingine, basi hakushikamana na vyote viwili. Kila kimoja katika hivyo kinaamrisha kushikamana na kingine. Amesema (Ta´ala):

مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ

“Atakayemtii Mtume basi kwa hakika amemtii Allaah.” (04:80)

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Naapa kwa Mola wako hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni mwamuzi katika yale wanayozozana kati yao kisha wasipate katika nafsi zao kinyongo chochote katika yale uliyohukumu na wajisalimishe kikamilifu.” (04:65)

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا

“Haiwi kwa muumini mwanamme na wala muumini mwanamke anapohukumu Allaah na Mtume wake jambo lolote iwe wana khiyari katika jambo lao; na anayemuasi Allaah na Mtume wake basi kwa hakika amepotea upotevu wa wazi.” (33:36)

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا

“Kile alichokupeni Mtume, basi kichukueni, na kile anachokukatazeni, basi kiacheni.” (59:07)

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manzilat-us-Sunnah fiyl-Islaam, uk. 12-14
  • Imechapishwa: 10/02/2017