05. Nafasi ya Sunnah na msimamo wake juu ya Qur-aan

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Tunaonelea kuwa Sunnah ni mapokezi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Sunnah inaifasiri Qur-aan na kuiweka wazi Qur-aan.”

MAELEZO

Hivi ndivyo Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) anavyoieleza na kuisifu Sunnah. Sunnah ni yale mapokezi yaliyonukuliwa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa msemo mwingine ni yale maneno yake yaliyothibiti, matendo na mambo aliyoyakubali. Kushikamana na mambo haya ni uokozi na kujiepusha nayo ni maangamivu. Ahl-ul-Bid´ah wamejipusha mbali na Sunnah, ima kikamilifu au baadhi yake. Badala yake wanafuata fikira za watu wa kawaida ambazo zinaenda kinyume na Sunnah ambapo wanatumbukia kwenye Bid´ah. Yule mwenye kushikamana barabara na maneno ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), vitendo vyake na yale mambo aliyoyakubali basi amesalimika. Yule mwenye kuyapa mgongo na akaenda kushikamana na maoni na fikira za watu amepotea na anawapotosha wengine.

Nafasi ya Sunnah juu ya Qur-aan umenyanyuliwa. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ameitaja kwa kuiambatanisha na Qur-aan. Alipotuneemesha kwa Qur-aan akaitaja pamoja na hekima na akasema:

هُوَ الَّذِي بَعَثَ فِي الْأُمِّيِّينَ رَسُولًا مِّنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِهِ وَيُزَكِّيهِمْ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَإِن كَانُوا مِن قَبْلُ لَفِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ

“Yeye ndiye aliyempeleka Mtume kwa wasiojua kusoma wala kuandika anayetokamana na wao; anawasomea Aayah Zake na anawatakasa na anawafunza Kitabu na hekima na japo walikuwa hapo kabla katika upotofu wa wazi.”[1]

Kitabu ni Qur-aan na hekima ni Sunnah. Kama tulivyotangulia kusema kwamba Sunnah ina nafasi ya juu katika Qur-aan. Katika hali fulani Qur-aan haiwezi kufasiriwa isipokuwa tu na kile kifungu cha Sunnah inayoipambanua na kuyabainisha yale yasiyokuwa wazi na yaliyotajwa kwa njia ya ujumla. Kuna mifano mingi juu ya hili katika Qur-aan tukufu ikiwa ni pamoja na zile swalah tano, viwango vya zakaah, namna ya kuhiji, kufunga na hukumu zengine zilizowekwa katika Shari´ah zilizotajwa kwa njia ya ujumla ndani ya Qur-aan na baadaye yakafasiriwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa maneno, vitendo na yale mambo aliyoyakubali. Kwa mfano Allaah ameamrisha swalah na zakaah:

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ

“Simamisheni swalah na toeni Zakaah.”[2]

Upande wa pili Sunnah imekuja kubainisha namna ya jinsi mtu atakavyoswali na kutoa zakaah. Haya yamebainishwa katika Sunnah. Nyakati za swalah, idadi ya Rak´ah ya swalah za faradhi, zile swalah za sunnah na mengine yote yametajwa kwa undani katika Sunnah takasifu, licha ya kuwa yametajwa ndani ya Qur-aan kwa njia ya ujumla.

Vivyo hivyo zakaah. Allaah ameamrisha zakaah, lakini upambanuzi wake umetajwa ndani ya Sunnah. Humo mmetajwa zile mali ambazo zakaah inatakiwa kutolewa, wakati ambao inakuwa ni wajibu kuitoa na hukumu zengine zilizowekwa katika Shari´ah zinazohusiana na dini hii tukufu.

Fungu lingine la Sunnah lina hukumu zenye kujitegemea ambazo hazikutajwa ndani ya Qur-aan tukufu. Fungu hili ni kidogo. Mfano wa hilo ni maneno ya Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa):

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kula kila mnyama wa mwitu mwenye kutia meno na kila ndege mwenye kutumia makucha.”[3]

Mfano mwingine ni maneno ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh):

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza mtu kumuoa shangazi yake na mama yake mdogo.”[4]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Amekataza mtu kumuoa mwanamke na shangazi yake na mwanamke na mama yake mdogo.”[5]

Fungu lingine la Sunnah ni zile ambazo hukumu zake zimekuja kuafikiana na hukumu za Qur-aan tukufu, ´ibaadah na mada nyenginezo.

[1] 62:02

[2] 02:43

[3] Muslim (1534), Abu Daawuud (3803), an-Nasaa’iy (7/206) na Ibn Maajah (3234).

[4] Ahmad (2/229), al-Bukhaariy (5108), Muslim (1408), Abu Daawuud (2065), an-Nasaa’iy (3290), at-Tirmidhiy (1126) na Ibn Maajah (1929).

[5] Ahmad (2/401), al-Bukhaariy (5110), Muslim (1408), Abu Daawuud (2066) na an-Nasaa’iy (3289).

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 26-29
  • Imechapishwa: 01/10/2019