Baadhi ya wanachuoni wameona kwamba maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ

 “Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa.“[1]

yanajumuisha shirki zote ijapo ni shirki ndogo. Kwa hiyo ni lazima kujichunga kutokamana na shirki aina zote. Kwani hakika mwisho wake ni mbaya. Amesema (Ta´ala):

إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ

“Hakika yule atakayemshirikisha Allaah, basi hakika Allaah atamharamishia Pepo na makazi yake yatakuwa ni motoni – na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kuwanusuru.”[2]

Ikishakuwa mshirikina ameharamishiwa shirki basi ni lazima awe mwenye kudumishwa Motoni milele. Hapana shaka kwamba yule mwenye kumshirikisha Allaah amekhasirika kwa kuikosa Aakhirah. Kwa sababu ataingizwa Motoni milele na pia ameikosa dunia. Kwa sababu alisimamikiwa na hoja na akajiwa na waonyaji. Lakini pamoja na hivyo akakhasirika. Hakufaidika na dunia chochote. Allaah (Ta´ala) amesema:

قُلْ إِنَّ الْخَاسِرِينَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ وَأَهْلِيهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ أَلَا ذَٰلِكَ هُوَ الْخُسْرَانُ الْمُبِينُ

“Sema: “Hakika waliokhasirika ni wale waliokhasiri nafsi zao na familia zao Siku ya Qiyaamah.” Tanabahi!  Huko ndiko kukhasirika kwa wazi.”[3]

Ameikhasiri nafsi yake mwenyewe. Kwa sababu hakufaidika nayo lolote. Atafikishwa Motoni – na ubaya ulioje mahali pa maingio watakapoingizwa! Amewakosa familia yake. Kwani kama wao ni waumini basi watakuwa Peponi na hivyo hatostareheka nao. Na wakiwa Motoni basi vivyo hivyo. Kwa sababu kila utakapoingia ummah basi utalaani nduguye.

[1] 04:116

[2] 05:72

[3] 39:15

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 11
  • Imechapishwa: 16/06/2021