05. Msingi wa ujumbe wa Mitume na Radd kwa Hizbiyyuun


Allaah (Ta´ala) amesema:

يُوحَى إِلَيَّ

“Nafunuliwa Wahy… “

Bi maana kutoka kwa Allaah kupitia kwa Jibriyl (´alayhis-Salaam) kama Mitume wengine wote. Yote anayofikisha katika Shari´ah ni Wahy kutoka kwa Allaah:

أَنَّمَا إِلَهُكُمْ إِلَهٌ وَاحِدٌ

“… kwamba hakika mwabudiwa wenu wa haki ni Mungu mmoja pekee… ”

Bi maana Mungu mmoja pekee anayeabudiwa kwa haki. Mungu maana yake mwabudiwa. Allaah pekee ndiye mwenye kuabudiwa kwa haki. Wengine wote ni wenye kuabudiwa kwa batili. Amesema (Ta´ala):

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ هُوَ الْبَاطِلُ وَأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ

“Hivyo ni kwa kuwa Allaah ndiye wa haki na kwamba vile wanavyoomba badala Yake ndiyo batili na kwamba Allaah ndiye Aliye juu kabisa, Mkubwa.”[1]

Hapa kuna dalili ya chanzo ya ujumbe wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na asili ya dini yake aliyokuja nayo na akaanza nayo ilikuwa ni kulingania katika Tawhiyd na kukataza shirki. Mitume wote kitu cha kwanza walichoanza nacho ni kulingania katika Tawhiyd na kuonya shirki. Hapa kuna Radd juu ya wale wenye kusema hii leo kwamba Mitume wamekuja ili kuhakikisha hukumu ya Allaah pekee juu ya ardhi. Maneno haya ni yenye kuzuliwa na batili. Mitume wamekuja kwa ajili ya kuhakikisha aina zote za ´ibaadah afanyiwe Allaah pekee. Amesema (Ta´ala):

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

”Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut [waungu batili].”[2]

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe Yeye na chochote.”[3]

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Mimi; hivyo basi niabuduni.”[4]

Huu ndio ulikuwa ujumbe wa Mitume. Ndani yake kunaingia maamrisho yote ya dini kukiwemo hukumu ya Allaah. Hata hivyo ni batili kuifanya yenyewe ndio msingi wa ujumbe. Hiyo maana yake ni kuipuuza Tawhiyd, kutotilia umuhimu jambo la shirki na ina maana kwamba Mitume walikuja kwa lengo la kutafuta utawala na uongozi.

[1] 22:62

[2] 16:36

[3] 04:36

[4] 21:25

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 442
  • Imechapishwa: 26/08/2019