Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Msingi wa pili wanasema: “Sisi hatuwaombi wala hatuelekei kwao isipokuwa ni kwa sababu ya kutafuta ukurubisho na uombezi. Dalili ya ukurubisho ni maneno Yake (Ta´ala):

وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ إِنَّ اللَّـهَ يَحْكُمُ بَيْنَهُمْ فِي مَا هُمْ فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي مَنْ هُوَ كَاذِبٌ كَفَّارٌ

“Na wale wanaowafanya wengine badala Yake kuwa walinzi [wakisema]: “Hatuwaabudu isipokuwa kwa lengo la kutukurubisha kwa Allaah ukaribu.” Hakika Allaah atahukumu baina yao katika yale yote waliyokhitilafiana nayo. Hakika Allaah hamwongoi aliye muongo, kafiri.” (39:03)

MAELEZO

Washirikina ambao Allaah amewaita kuwa ni ´washirikina` na akawahukumu kudumu Motoni milele, hawakushirikisha katika uola wa Allaah, bali walishirikisha katika ´ibaadah. Hawasemi kuwa waungu wao wanaumba, wanaruzuku, wananufaisha, wanadhuru au wanaendesha mambo pamoja na Allaah. Kazi yao ilikuwa ni kuwafanya tu kuwa waombezi na watetezi. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Na wanaabudu asiyekuwa Allaah ambao [hawawezi] kuwadhuru na wala kuwanufaisha na wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”” (10:18)

Wanakubali kuwa hawadhuru na wala hawanufaishi na kwamba ni waombezi peke yao ambao wanamweleza Allaah mahitaji yao. Wanawachinjia na wanawawekea nadhiri. Hawakufanya haya kwa sababu wanaona kuwa wanaumba, wanaruzuku, wananufaisha na wanadhuru. Bali ni kwa sababu wanawaombea mbele ya Allaah. Hii ndio dini ya washirikina.

Hii leo ukihojiana na mwabudia kaburi utaona anasema maneno hayahaya:

“Mimi najua kuwa walii au mja huyu mwema hanufaishi wala hadhuru. Lakini ni mja mwema na ninachotaka kutoka kwake aniombee mbele ya Allaah.”

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 19-20
  • Imechapishwa: 18/08/2022