Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Msingi wa kwanza utambue kuwa makafiri ambao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita, walikuwa wakikubali ya kwamba Allaah (Ta´ala) ndiye Muumbaji Mwenye kuyaendesha mambo. Hata hivyo hili halikuwaingiza wao katika Uislamu. Dalili ya hilo ni maneno Yake (Ta´ala):

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُون

“Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini au nani anayemiliki kusikia na kuona na nani anayemtoa [aliye] hai kutoka maiti na anayemtoa maiti kutoka [aliye] uhai na nani anayeendesha mambo? Watasema: “Ni Allaah”. Basi sema: “Je, basi hamchi?” (10:31)

MAELEZO

Msingi wa kwanza utambue kuwa makafiri ambao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita, walikuwa wakikubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Pamoja na kukubali kwao Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah hakukuwafanya waingie katika Uislamu na hakukufanya damu na mali zao zisichukuliwe. Hili linafahamisha ya kwamba Tawhiyd haihusiani na kuthibitisha uola peke yake na vivyo hivyo shirki haihusiani tu na kuamini kuwa Allaah amepwekeka katika matendo Yake. Uhakika wa mambo ni kwamba hakuna yeyote asiyeamini kuwa Allaah amepwekeka katika matendo Yake isipokuwa viumbe waovu na waliopinda peke yake. Vinginevyo ni kwamba viumbe wote wanathibitisha Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah maana yake ni kwamba Allaah peke yake ndiye muumbaji, mruzukaji, muhuishaji, mfishaji na mwenye kuendesha mambo. Kwa ibara nyingine iliyofupi Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah ni kumpwekesha Allaah kwa matendo Yake.

Hakuna kiumbe yeyote aliyedai kuwa kuna yeyote anayeumba, anayeruzuku, anayehuisha au anayefisha pamoja na Allaah (Ta´ala). Washirikina walikuwa wakiamini kuwa Allaah peke yake ndiye muumbaji, mwenye kuruzuku, mwenye kuhuisha na kufisha:

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ

“Ukiwauliza: “Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi?” bila shaka watasema: “Allaah.” (31:25)

قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ السَّبْعِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ

“Sema: “Nani Mola wa mbingu saba na Mola wa ´Arshi tukufu?” Watasema: “Ni ya Allaah pekee.” (23:86-87)

Soma mwisho wa Suurah “al-Mu´minuun” uone namna ambavyo washirikina walikuwa wakithibitisha Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Vivyo hivyo Suurah “Yuunus”:

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُون

“Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini au nani anayemiliki kusikia na kuona na nani anayemtoa [aliye] hai kutoka maiti na anayemtoa maiti kutoka [aliye] uhai na nani anayeendesha mambo? Watasema: “Ni Allaah”. Basi sema: “Je, basi hamchi?”

Walikuwa wakithibitisha haya pasi na shaka.

Kwa hivyo Tawhiyd haina maana kuwa ni kukiri Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah, kama wanavyodai wanafalsafa na wananadharia katika ´Aqiydah zao. Wanaonelea kuwa Tawhiyd ni kuthibitisha kuwa Allaah peke yake ndiye muumbaji, mruzukaji, muhuishaji na mfishaji. Wanasema:

“Ni Mmoja katika dhati Yake na hagawanyiki, ni Mmoja katika sifa Zake na hafanani na yeyote na ni mmoja katika matendo Yake na hana mshirika.”

Haya si chengine zaidi ya Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Hakuna kitabu chochote kilichoandikwa na wanafalsafa, isipokuwa mtaona kuwa hawaongelei jengine zaidi ya Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Hii sio aina ya Tawhiyd ambayo Allaah aliwatuma kwayo Mitume. Kuthibitisha hili peke yake halimnufaishi kitu mwenye nayo. Aina hii ilikuwa ikithibitishwa na washirikina na viongozi wa kikafiri na halikuwafanya wakatoka katika ukafiri wala kuwaingiza katika Uislamu. Hili ni kosa kubwa kubwa. Mwenye kuamini namna hii hakuzidisha kitu zaidi ya kile alichokuwa akiamini Abu Jahl na Abu Lahab.

Wanateolojia wa leo wanathibitisha tu aina ya Tawhiyd yenye kusema kuwa Allaah amepwekeka katika uola Wake, hawagusii kabisa aina ya Tawhiyd yenye kusema kuwa Allaah peke yake ndiye mwenye haki ya kuabudiwa. Kuita hii kuwa ndio Tawhiyd ni kosa kubwa kubwa.

Kuhusu shirki, wanaifasiri ifuatavyo:

“Mtu kuamini kuwa kuna ambaye anaumba au anaruzuku pamoja na Allaah.”

Haya hayakusemwa si na Abu Jahl wala Abu Lahab. Hawakusema kuwa kuna ambaye anaumba wala kuruzuku pamoja na Allaah. Bali uhakika wa mambo ni kwamba walikuwa wakithibitisha kuwa Allaah ndiye mwenye kuumba, mwenye kuruzuku, mwenye kuhuisha na mwenye kufisha.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 16-19
  • Imechapishwa: 18/08/2022