Kumuamini Allaah ina maana ya kukubali uola na kuabudiwa Kwake. Kwa msemo mwingine ina maana ya kukubali aina tatu za Tawhiyd, kuziamini na kuzitendea kazi. Nazo ni Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah, Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah na Tawhiyd al-Asmaa´ was-Swifaat.

Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah maana yake ni kumpwekesha Allaah kwa matendo Yake Yeye kukiwemo kuumba, kuruzuku, kuhuisha na kufisha na kwamba Yeye ndiye mola na mmiliki wa kila kitu.

Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah maana yake ni kumpwekesha kwa matendo ya waja ambayo wao wanajikurubisha kwayo Kwake ikiwa ni katika yale aliyoyaweka Allaah katika Shari´ah. Mfano wa hayo ni kama du´aa, kuwa na khofu, kutaraji, kupenda, kuchinja, kuweka nadhiri, kuomba msaada, kuomba hifadhi, kuomba uokozi wa haraka, swalah, swawm, hajj, kujitolea katika njia ya Allaah na kila alichokiweka Allaah au kukiamrisha, hashirikishwi pamoja na Allaah mwengine asiyekuwa Yeye. Ni mamoja mtu huyo ni mfalme, Mtume, walii na wengine.

Tawhiyd al-Asmaa´ was-Swifaat maana yake ni kumthibitishia Allaah yale majina na sifa alizojithibitishia Yeye Mwenyewe au alizomthibitishia Mtume Wake na wakati huohuo kumtakasa Allaah kutokamana na yale mapungufu na kasoro alizojitakasa Mwenyewe au alizomtakasa kwazo Mtume Wake. Inatakiwa kufanya hivo pasi na kufananisha, kushabihisha, kupotosha, kukanusha wala kupindisha maana. Amesema (Ta´ala):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا

“Allaah ana majina mazuri kabisa, hivyo basi muombeni kwayo.”[2]

[1] 42:11

[2] 07:180

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min Usuwl ´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 17-18
  • Imechapishwa: 12/05/2022