05. Mke mwema anatakiwa kumfurahisha mume


Miongoni mwa sifa nyingine za mke mwema ni kwamba anamfurahisha mume wake pindi anapomtazama sura yake, muonekano wake na mavazi yake yamfurahishe pindi mume wake anapomtazama. Anatakiwa awe tayari kwa kumtii na kutimiza maamrisho yake bila kuhisi kipingamizi wala jeuri. Zingatia Hadiyth katika “as-Sunan” ya an-Nasaa´iy[1] iliyopokelewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa juu ya mwanamke aliye bora. Akajibu:

“Ni yule mwenye kumfurahisha [mume wake] pindi anapomtazama, anamtii pale anapomuamrisha na haendi kinyume juu ya nafsi yake mwenyewe na mali yake kwa yale anayoyachukia.”[2]

Namna hii ndivyo anavyotakiwa kuwa kwa njia ya sura na muonekano wake. Anatakiwa kutilia umuhimu mkubwa juu ya sura na muonekano wake wakati anapokuwa mbele yake. Kadhalika anatakiwa kutilia uzito na kutilia umuhimu kwa kutimiza maamrisho yake, hamu yake na haja zake.

Kwa masikitiko makubwa wanawake wengi hawajipambi na kujipodoa isipokuwa tu wakati wanapotaka nyumbani kwa ajili kwenda katika sikukuu, mkusanyiko na mfano wa hayo. Lakini wakati mume anapoingia nyumbani anamkuta katika mavazi mabaya na kunuka. Nywele zimevurugika na hazikutengenezwa. Anamkuta kwa sifa ambazo zinamkimbiza naye. Halafu anakuwa ni mwenye kuumia kwa yeye kila siku kujipamba pindi anapotoka nyumbani bila hata yeye kupata moja ya kumi. Vipi mwanaume atamtamani mwanamke kama huyu ambaye hizi ndizo sifa zake? Ni mahaba sampuli gani ambayo atakuwa nayo kwa mwanamke ambaye yuko namna hii? Hii ni dalili inayoonesha upumbavu wa mwanamke na upungufu wa akili yake kutokamana na kuhakikisha maisha ya ndoa na furaha yake.

Aidha kuna wanawake wengi ambao ni waasi na wapekutevu. Wanawapuuza waume zao na kuwakasirisha. Kunalalamikiwa sana juu ya tabia zao kwa waume zao na wengine. Mwanamke huyu anakuwa ni mwenye kuleta maisha magumu, maisha ya tabu na maisha ya udhaifu nyumbani kwake na anakuwa ni mwenye kuitendea jinai nafsi yake mwenyewe.

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh”[3] yake kupitia kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mmoja wenu anapofika wakati wa usiku [kutoka safari] basi asiwaendee familia yake.”

Asimshtukizie mke usiku. Kwa nini? Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ili mwanamke ambaye mume wake alikuwa hayupo aweze kujinyoa na mwanamke wa nywele zilizovurugika aweze kuchanua nywele zake.”

Hapa kuna ishara tukufu kwa mwanamke. Nayo ni kwamba anatakiwa kumkaribisha mume wake kwa usafi kamilifu, muonekano mzuri na makutano mazuri. Hili khaswa pale ambapo mume wake alikuwa hayupo au amesafiri. Hili linahitajia kwa mwanamke kuweza kujiandaa na kujitayarisha. Hili linahusu hata kufanya mpangilio na muonekano wa nyumba. Mama wa waumini ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameelezea:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifika kutoka safarini. Nikawa nimefunika mapazia yangu kwa kusahau na yalikuwa na picha. Wakati (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoyaona akayararua na kusema: “Watu watakaokuwa na adhabu kali siku ya Qiyaamah ni wale wanaoigiza viumbe vya Allaah.” Tukafanya kwayo mto mmoja au mito zaidi.”[4]

Kwa nini aliweka mapazia haya? Kwa kuwa alitaka atakapoingia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nyumbani aikute nyumba na yeye mwenyewe katika muonekano mzuri.

Katika Hadiyth hii tunapata faida kwamba mwanamke anatakiwa kuitengeneza nyumba yake na kuipanga kama ambavyo vilevile anatakiwa kujitayarisha maandalizi kwa njia kamilifu na kukutana na mume wake kwa njia nzuri. Hizi zote ni sifa zilizokuja katika Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) za mwanamke na mke mwema.

Miongoni mwa hayo ni yale yaliyopokea at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Awsatw”[5] kupitia kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Je, nisikuelezeni wanawake wenu Peponi?”

Yaani mke mwenye sifa zinazosifika na zenye baraka zinazomfanya kustahiki kuwa Peponi. Akaendelea na kusema:

“Kila mwanamke mwenye mahaba na mwenye rutuba ambaye, pindi anapokasirika au akafanyiwa vibaya au mume wake akakasirika, anasema: “Nauweka mkono wangu kwenye mkono wako. Sintosinzia mpaka utapofurahi.”

Bi maana hatofumba macho, hatolala wala kufurahi mpaka awe radhi naye.

Kwa masikitiko makubwa kuna wanawake wanaolala pasi na kujali waume zao wamekasirika usiku wa kwanza, usiku wa pili, usiku wa tatu, usiku wa kumi au mwezi mzima. Kana kwamba jambo hili halimuhusu kabisa. Kana kwamba hatokutana na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na kumfanyia hesabu kwa matendo haya anayoyafanya.

[1] Nambari. (3231). Imaam al-Albaaniy ameisahihisha katika ”as-Swahiyhah” (1738)

[2] al-Bukhaariy (5954) na Muslim (2107).

[3] (715).

[4] al-Bukhaariy (5954) na Muslim (2107).

[5] (1743). Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika “as-Swahiyhah” (3370).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifaat-uz-Zawjah as-Swaalihah, uk. 23-27
  • Imechapishwa: 18/06/2017