2. Anayotakiwa kufanya na ambayo anatakiwa ajizuie katika nywele za kichwa chake, nyusi zake na hukumu ya kutia hina na hukumu ya kupaka rangi

a) Mwanamke wa Kiislamu anatakiwa kuachia nywele za kichwani mwake na ni haramu kwake kuzinyoa isipokuwa kwa dharurah. Shaykh Muhammad bin Ibrahiym Aalush-Shaykh (Rahimahu Allaah), ambaye alikuwa Muftiy wa Saudi Arabia, amesema:

“Haijuzu kunyoa nywele za kichwani kwa mwanamke. Hayo ni kutokana na yale aliyopokea an-Nasaa´iy katika “as-Sunan” yake kwa cheni ya wapokezi wake kutoka kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh), al-Bazzaar amepokea katika “al-Musnad” yake kutoka kwa ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh), Ibn Jariyr amepokea kwa cheni ya wapokezi wake kutoka kwa ´Ikrimah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza mwanamke kunyoa kichwa chake.”

Makatazo yakija kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi yanapelekea katika uharamu midhali hakuna kilichoonyesha kinyume. Mullaa ´Aliy Qaariy amesema katika “al-Mirqaah Sharh-il-Mishkaah”: “Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… mwanamke kunyoa kichwa chake.”

hayo ni kwa sababu ile mikia ya wanawake ni kama ndevu kwa wanaume katika pambo na uzuri.”[1]

Ama mwanamke kupunguza nywele za kichwani mwake ikiwa amefanya hivo kwa sababu ya haja na lengo sio kujipamba, kwa mfano hawezi kuzihudumia, zimekuwa ndefu sana na zinamtia uzito, basi hakuna neno akakata kwa kiasi cha haja kama ambavyo baadhi ya wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakifanya baada ya kufa kwake. Baada ya yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kufa waliacha kujipamba na wakajitosheleza kurefusha nywele.

Lakini mwanamke kukata nywele zake lengo ikiwa ni kujifananisha na wanawake wa kikafiri, wanawake wachafu au kujifananisha na wanaume, basi kitendo hichi ni haramu pasi na shaka yoyote. Hayo ni kwa sababu ya makatazo yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa jumla kujifananisha na makafiri na mwanamke kujifananisha na wanaume. Makusudio ikiwa ni kujipamba kinachonidhihirikia ni kwamba haifai pia. Shaykh wetu Muhammad al-Aamiyn ash-Shanqiytwiy (Rahimahu Allaah) amesema katika “Adhwaa´-ul-Bayaan”:

“Desturi ambayo ilikuwa inapita katika miji mingi ambapo mwanamke anakata nywele za kichwani mwake mpaka kufika karibu na mashina ya nywele zake ni mwenendo wa wazungu unaoenda kinyume na walivyokuwa wanawake wa Kiislamu na wanawake wa kiarabu kabla ya Uislamu. Ni miongoni mwa jumla ya upondokaji ambao majanga yameenea katika dini, tabia, sifa za wanawake na kadhalika.”

Kisha akajibu kuhusu Hadiyth inayosema kuwa wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikata nywele za kichwani mwao mpaka zikawa kama kitu kilichokusanywa ya kwamba: wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walipunguza nywele za vichwani mwao baada ya kufa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa sababu walikuwa wakijipamba wakati wa uhai wake na miongoni mwa mapambo yao makubwa ni pamoja na nywele zao. Lakini baada ya kufa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wana hukumu ambazo ni maalum kwao pekee wasizoshirikiana na mwanamke yeyote katika wanawake wa ulimwenguni. Hukumu yenyewe ni kukatika kwa matarajio na tamaa ya kuolewa ambayo haikuchanganyikana na tamaa yoyote. Wao ni kama wenye eda wenye kufungwa kwa sababu yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mpaka pale watapokufa. Amesema (Ta´ala):

وَمَا كَانَ لَكُمْ أَن تُؤْذُوا رَسُولَ اللَّـهِ وَلَا أَن تَنكِحُوا أَزْوَاجَهُ مِن بَعْدِهِ أَبَدًا ۚ إِنَّ ذَٰلِكُمْ كَانَ عِندَ اللَّـهِ عَظِيمًا

“Haikupasini kwenu kumuudhi Mtume wa Allaah na wala kuwaoa wake zake baada yake maishani – hakika jambo hilo mbele ya Allaah ni kubwa mno.”[2]

Kukata tamaa ya wanaume kabisa ni sababu ya kuruhusiwa kuhalalishiwa vitu katika mapambo ambavyo haviwezi kuhalalishwa pasi na sababu hiyo.”[3]

Kwa hivyo ni lazima kwa mwanamke kuzichunga nywele za kichwani mwake, azifanyie bidii na azifanye kuwa mikia mitatu. Haijuzu kwake kuzikusanya juu ya kichwa au kuziteremsha upande wa kichogo chake. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika “Majmuu´-ul-Fataawaa”:

“Kama wanavokusudia baadhi ya wanawake wachafu kuzifunga upande mmoja hali ya kuziteremsha kati ya mabega yake.”[4]

Shaykh Muhammad bin Ibrahiym Aalush-Shaykh (Rahimahu Allaah), ambaye alikuwa Muftiy wa Saudi Arabia, amesema:

“Ama yale yanayofanywa na baadhi ya wanawake wa Kiislamu hii leo ambapo wanazilaza nywele za kichwani upande mmoja na kuzikusanya upande wa kichogo au kiziweka juu ya kichwa – kama wanavofanya wanawake wa kizungu – kitendo hichi hakijuzu kwa sababu ni kujifananisha na wanawake wa makafiri.”[5]

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amepokea katika Hadiyth ndefu ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kuna watu aina mbili wa Motoni sijawaona; wanaume walio na bakora kama mkia wa ng´ombe ambazo wanawapiga kwazo watu, na wanawake waliovaa vibaya, uchi, Maaylaat na Mumiylaat. Vichwa vyao ni kama nundu ya ngamia. Hawatoingia Peponi na wala hawatonusa harufu yake. Harufu yake inapatikana umbali wa kadhaa na kadhaa.”

Ameipokea Muslim.

Wanachuoni wamefasiri maneno yake “Maaylaat na Mumiylaat” ya kwamba wanachana ile mitindo inayokuwa upande mmoja; misuko ambayo ni ya wale wanawake wachafu. Isitoshe wanawachana wengine mitindo hiyo. Mitindo hii ni ya wanawake wa kizungu na wale wanawake wa waislamu wanaowafuata kichwa mchunga.”[6]

Kama ambavyo mwanamke wa Kiislamu anakatazwa kunyoa au kukata nywele za kichwani mwake pasi na haja, vivyo hivyo anakatazwa kuziunganisha na kuziongeza kwa nywele zengine. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemlaani mwanamke mwenye kuunganisha nywele na mwenye kuunganishwa.”

Mwanamke mwenye kuunganisha nywele ni yule anayeziunga nywele zake kwa nywele za mwengine na mwenye kuunganisha ni yule anayemuunganisha. Kwa sababu huo ni udanganyifu.

Miongoni mwa uunganishaji ulioharamishwa ni kuvaa baruka inayojulikana hii leo. al-Bukhaariy na Muslim na wengineo wamepokea ya kwamba Mu´aawiyah (Radhiya Allaahu ´anh) alitoa Khutbah wakati alipofika Madiynah na akatoa mkusanyiko wa nywele akasema:

“Wana nini wanawake wenu wanaweka vichwani mfano wa hii. Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema: “Hakuna mwanamke yeyote atakayeweka kichwani mwake nywele zisizokuwa zake isipokuwa itakuwa ni udanganyifu.”

Baruka ni nywele za bandia zinazofanana na nywele za kichwani. Kuivaa ni udanganyifu.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (02/49).

[2] 33:53

[3] Adhwaa´-ul-Bayaan (05/598-601).

[4] Majmuu´-ul-Fataawaa (22/145).

[5] Majmuu´-ul-Fataawaa (02/47).

[6] Majmuu´-ul-Fataawaa (02/47). Tazama pia ”al-Iydhwaah”, uk. 85 ya Shaykh Hamuud at-Tuwayjiriy.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 17-20
  • Imechapishwa: 22/10/2019