05. Mbinu alizotumia Shaytwaan kuingiza shirki kwa watu

Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimhu Allaah) amesema:

Halafu yalipokuwa kwa watu wengi katika Ummah yale yaliyokuwa, shaytwaan akawadhihirishia Ikhlaasw katika sura ya kuwadharau watu wema na kupunguza katika haki zao na vilevile akawadhihirishia kumshirikisha Allaah katika sura ya kuwapenda watu wema na wafuasi wao.

MAELEZO

Halafu yalipokuwa kwa watu wengi katika Ummah… – Wanapoambiwa wasiwaombe viumbe na wasitake uokozi kutoka kwao na badala yake wamwombe Allaah, watake uokozi kutoka kwa Allaah, wamwombe Allaah na wamtegemee Allaah na wasiyategemee makaburi na wafu, wanasema kuwa wewe unawadharau mawalii. Wanasema kuwa hawa ni mawalii. Hadhi yao kwetu ni sisi kuwatukuza, kuwaheshimu na kutaja majina yao. Wanasema kuwa hii ndio hadhi yao na kwamba wewe unawadharau na hutambui fadhila zao. Wanawaambia namna hii wale walinganizi wa Tawhiyd.

Tunawaambia kuwa sisi tunawapenda watu wema na mawalii wa Allaah. Tunawapenda, tunawatukuza na tunawaheshimu. Lakini pamoja na yote haya hatuwapi kitu katika haki za Mola (Subhaanahu wa Ta´ala). Hatuwapi kitu katika ´ibaadah kwa kuwa hii sio haki yao. Isitoshe, wao wenyewe hawaridhii hili. Hawaridhii kuombwa pamoja na Allaah na kuwataka uokozi wakati wa matatizo.

Vilevile akawadhihirishia kumshirikisha Allaa… – Wao wanachosema ni kwamba kuwataka uokozi watu wema ni kutambua fadhila zao na ni kuwatukuza! Shaytwaan amewapambia haya. Makusudio hapa ni shaytwaan wa kijini na wa kibinaadamu. Wanazuoni wa upotevu ni mashaytwaan wa kibinaadamu. Wanazungumza, wanaandika na kutunga [vitabu] vinavyolingania katika shirki na huku wanadai kuwa kufanya hivi ni kuwaadhimisha watu wema na kutambua fadhila zao na kuwapenda. Upande mwingine wanasema kutowaomba na kuwataka uokozi ni kuzembea katika haki zao, ni kuwachukia na mengineyo wanayoyasema. Haya yanapatikana katika vitabu vyao.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 15-16
  • Imechapishwa: 18/05/2021