05. Masharti ya kupatikana al-Jamaa´ah


al-Jamaa´ah haiwepo isipokuwa kwa mambo mawili:

La kwanza: Mfumo wake iwe ni Qur-aan na Sunnah. Mfumo wake isiwe ni madhehebu na maoni ya fulani. Mfumo wake iwe ni Qur-aan na Sunnah.

La pili: al-Jamaa´ah iwe na kiongozi muislamu ambaye anaiongoza na kurejea kwake. Haiwezekani al-Jamaa´ah ikakusanyika pasi na kiongozi. Ni lazima awepo kiongozi ambaye anarejelewa. Kwa ajili hii ndio maana alimwambia (Swalla Allaahu ´ayahi wa sallam) Hudhayfah:

“Shikamana na Jamaa´ah ya Waislamu na kiongozi wao.”

Akamuuliza: “Vipi ikiwa kama kutakuwa hakuna al-Jamaa´ah wala kiongozi?” Akamwambia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Jiepushe na mapote yote.”

Amemuamrisha ajiepishe na mapote hayo. Kwa hivyo usiwe isipokuwa pamoja na al-Jamaa´ah ya Waislamu na usiwe na makundi kinyume na al-Jamaa´ah ya Waislamu. Afadhali ubaki peke yako mpaka yatapokujia mauti na wewe uko katika hali hiyo. Hapa tunapata funzo ya kwamba mtu asiwe pamoja na makundi yanayokwenda kinyume na mfumo wa haki na akasema kwamba hii ndio al-Jamaa´ah. al-Jamaa´ah haipatikani isipokuwa kwa sharti mbili:

La kwanza: Mfumo wao iwe ni Qur-aan na Sunnah na wanafuata mfumo wa Salaf-us-Swaalih.

La pili: Wawe na kiongozi ambaye ni Muislamu anaiongoza na wanarejea kwake.

Hakuna al-Jamaa´ah isipokuwa kwa kuwepo kiongozi na hakuna kiongozi isipokuwa ni lazima kumsikiliza na kumtii. Huu ndio mfumo wa Waislamu na ndio Sunnah ambayo anaipambanua (Rahimahu Allaah).

Katika haya kuna makatazo ya kuleta mfarakano katika maoni na kwenda kinyume. Ni lazima kwa mtu kulazimiana na al-Jamaa´ah. Anatakiwa kulazimiana nao maadamu hawako katika upotevu.

atakuwa ni mpotevu mwenye kupoteza.

Atakuwa amepotea mwenyewe na njia na vilevile ni mwenye kuwapoteza wengine. Amepotea mwenyewe na ni mwenye kuwapoteza wale wenye kumuiga na kumfuata. Amesema (Ta´ala):

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

“Na atakayempinga Mtume baada ya kuwa imeshambainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya Waumini, tutamgeuza alikogeukia na tutamuingiza Motoni – na uovu ulioje mahali pa kurejea!” (04:115)

Lililo wajibu kwa muislamu ni kufuata njia ya Waumini na wala asende kinyume nao na kutofautiana nao.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Sharh-is-Sunnah, uk. 16-17
  • Imechapishwa: 13/06/2017