Jengine ni kwamba kusoma Qur-aan taratibu ipasavyo ni bora kuliko kuswali kwa kasi. Haraka yenye kuruhusiwa ni ile ambayo haidondoshi na kuharibu herufi yoyote. Akidondosha na kuharibu baadhi ya herufi kwa sababu ya haraka itakuwa ni jambo lisilofaa na likemewe. Ni vema akisoma kisomo cha wazi ambacho waswaliji watanufaika kwacho.

Allaah amewasimanga wale wanaosoma Qur-aan pasi na kufahamu maana yake. Amesema (Ta´ala) amesema:

وَمِنْهُمْ أُمِّيُّونَ لَا يَعْلَمُونَ الْكِتَابَ إِلَّا أَمَانِيَّ

“Miongoni mwao wako wasiojua kusoma wala kuandika; hawakijui Kitabu isipokuwa matamanio ya kudhania.”[1]

Bi maana kisomo bila kufahamu. Makusudio ya kuteremshwa Qur-aan ni kufahamu maana yake na kuitendea kazi na sio kusoma peke yake.

Baadhi ya maimamu wa misikiti hawasomi Tarawiyh kwa njia iliowekwa katika Shari´ah. Wanafanya haraka katika kisomo kasi ambayo inaharibu utendaji kazi wa Qur-aan kwa njia sahihi. Hawafanyi utulivu katika hali ya kusimama, Rukuu´ na Sujuud.

Kutulia ni nguzo miongoni mwa nguzo za swalah na wanatendea kazi ile idadi ya chini kabisa ya Rak´ah. Hivyo wanakusanya kati ya uchache wa Rak´ah, kuwepesisha swalah na kufanya vibaya katika kisomo. Huku ni kufanya mchezo katika ´ibaadah[2]. Ni lazima kwao kumcha Allaah na wazifanye vizuri swalah zao. Wasizikoseshe nafsi zao na walioko nyuma yao kutekeleza Tarawiyh kwa njia iliowekwa katika Shari´ah[3].

[1] 02:78

[2] Baadhi yao wanazitoa nje sauti zako kwa kisomo ca Qur-aan kwa kutumia kipaza sauti. Matokeo yake wanawashawishi misikiti ilioko pembezoni, kitu ambacho hakijuzu. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Ambaye anasoma Qur-aan wakati ambapo watu wanaswali swalah ya sunnah basi haifai kwake kusoma kwa sauti ya juu ambayo itawashughulisha. Kwani hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwatokea Maswahabah zake wakati walipokuwa wanaswali msikitini akasema:

“Enyi watu! Kila mmoja wenu anamnong´oneza Mola wake. Hivyo wamoja wasisome Qur-aan kwa sauti juu ya wengine.”(Majmuu´-ul-Fataawaa 23/61-64).

[3] Baadhi ya maimamu wa misikiti wanasoma Qur-aan haraka na wanairefusha ili wapate kukamilisha Qur-aan katika lile kumi la mwanzo na la katikati. Anapokamilisha basi  wanaikimbia misikiti yao na wanamweka mtu mwengine na wanasafiri katika ´Umrah ilihali nyuma pengine wamemwacha mtu ambaye hafai kufanywa imamu. Hilo ni kosa kubwa, upungufu mkubwa na kupoteza ile kazi aliyopewa ya kuwaswalisha waswaliji mpaka mwishoni mwa mwezi. Kwani kazi aliyopewa ni lazima kuitekeleza na kufanya ´Umrah ni jambo lililopendekezwa. N vipi ataacha jambo la lazima juu yake kwa ajili ya jambo lililopendekezwa? Kubaki kwake msikitini kwa ajili ya kazi yake ni bora kuliko kufanya ´umrah.

Baadhi ya maimamu wengine wakimaliza Qur-aan basi wanawepesisha swalah na wanapunguza kisomo katika nyusiku zengine za mwezi ambazo watu huachwa huru kutokamana na Moto. Kana kwamba watu hawa wanaona kuwa lengo la Tarawiyh na Tahajjud ni kusoma Qur-aan yote na si kuhuisha nyusiku hizi zilizobarikiwa kwa kusimama kwa ajili ya kumwigiliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kutafuta fadhilah zake. Huu ni ujinga wao na kucheza na ´ibaadah. Tunataraji kwa Allaah atawarudisha katika usawa.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mulakhasw al-Fiqh (01/169-171)
  • Imechapishwa: 10/05/2021