Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

2- Tunasema kuhusu upwekekaji wa Allaah hali ya kuwa ni wenye kuitakidi kwa tawfiyq ya Allaah ya kwamba Allaah ni mmoja asiyekuwa na mshirika.

MAELEZO

Bi maana Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Tawhiyd na ´Aqiydah yana maana moja. Ni mamoja ukasema “Tawhiyd”, “´Aqiydah” au “imani”, japokuwa matamshi yanatofautiana.

Hapa mwandishi anajisalimisha kwa Allaah (´Azza wa Jall) na kunyenyekea mbele Yake na kujiweka mbali na hila na nguvu zake zote. Mtu hatakiwi kujisifu nafsi yake. Bali anatakiwa siku zote kutegemea tawfiyq ya Allaah na kwamba anaweza kufanya kila kitu kwa matakwa na uwezo wa Allaah. Hii ni katika adabu ya wanachuoni (Rahimahumu Allaah).

Ana ni mmoja na hana mshirika. Hii ndio Tawhiyd. Ni mmoja katika uola Wake, katika kustahiki Kwake kuabudiwa na katika majina na sifa Zake.

Bi maana tunaamini upwekekaji wa Allaah (´Azza wa Jall). Upwekekaji wa Allaah, Tawhiyd, unahusiana na kumwabudu Allaah (Subhanaahu wa Ta´ala) pekee na kutomwabudu mwengine yeyote.

Kupitia usomaji wa Qur-aan na Sunnh Tawhiyd imegawanyika mafungu matatu. Haya ndio yaliyothibitishwa na Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Mwenye kuzidisha kifungu cha nne au cha tano ni kitu amekitoa kwake mwenyewe. Maimamu wameigawanya Tawhiyd mafungu matatu kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah. Aayah zote za Qur-aan na za Hadiyth hazitoki nje ya mafungu haya matatu.

1- Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Ni kule kumpwekesha Allaah (Subhaanah) kwa matendo Yake. Kama mfano wa uumbaji, uruzukaji, kuhuisha, kufisha na kuendesha ulimwengu. Hakuna mungu mwingine asiyekuwa Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala), Mola wa walimwengu.

2- Tawhiyd-ul-´Ibaadah, huitwa vilevile Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Maana yake ni kwamba Allaah pekee ndiye anafaa kuabudiwa kwa mapenzi, kuogopwa, kutarajiwa,  kutii maamrisho Yake na kuacha yale aliyokataza. Kwa msemo mwingine Allaah anatakiwa kupwekeshwa kwa matendo ya waja aliyowawekea katika Shari´ah.

3- Tawhiyd-ul-Asmaa´ was-Swifaat. Maana yake ni kwamba inatakiwa kuthibitisha yale majina na sifa zote za Allaah zilizotajwa katika Qur-aan na Sunnah, sambamba na hilo kumkanushia zile kasoro na aibu zote ambazo Allaah amejikanushia Mwenyewe au Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Aayah zote zinazozungumzia matendo ya Allaah zinahusiana na Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah.

Aayah zote zinazozungumzia ´ibaadah, kuamrishwa kwa ´ibaadah na kuita katika ´ibaadah zinahusiana na Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah.

Aayah zote zinazozungumzia majina ya Allaah (´Azza wa Jall) na sifa Zake zinahusiana na Tawhiyd-ul-Asmaa´ was-Swifaat.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 28-29
  • Imechapishwa: 04/06/2019