Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Suala la tatu: Kuilingania

MAELEZO

Bi maana kulingania katika Shari´ah ya Allaah (Ta´ala) iliyokuja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutokana na ngazi zake tatu au nne ambazo amezitaja Allaah (´Azza wa Jall) katika  pale aliposema:

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ

“Ita katika Njia ya Mola wako kwa hekima na maneno mazuri.” (an-Nahl 16 : 125)

وَلَا تُجَادِلُوا أَهْلَ الْكِتَابِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ إِلَّا الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنْهُمْ

“Na wala msijadiliane na watu wa kitabu isipokuwa kwa yale ambayo ni mazuri zaidi – isipokuwa wale waliodhulumu miongoni mwao.” (al-´Ankabuut 29 : 46)

Ni lazima Da´wah hii iwe imefungamana na elimu juu ya Shari´ah ya Allaah (´Azza wa Jall) ili iweze kuwa imejengeka juu ya ujuzi na umaizi. Amesema (Ta´ala):

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي ۖ وَسُبْحَانَ اللَّـهِ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ

“Sema: “Hii ndio njia yangu nalingania kwa Allaah juu ya ujuzi mimi na anayenifuata. Utakasifu ni wa Allaah – nami si miongoni mwa washirikina.” (Yuusuf 12 : 108)

Umaizi ina maana mlinganizi awe ni mjuzi wa hukumu ya Shari´ah, namna ya kulingania na hali ya yule anayemlingania.

Da´wah inaweza kuwa kwa njia na nyanja mbalimbali. Miongoni mwazo ni kulingania katika dini ya Allaah kwa khutbah, mihadhara, makala, duara za kielimu, kutunga vitabu na vikao binafsi. Kwa mfano mtu akikaa katika duara ya kielimu  ambapo kunalinganiwa katika dini ya Allaah, inahesabika kuwa ni uwanja ambapo kunalinganiwa katika dini ya Allaah (´Azza wa Jall). Lakini hata hivyo inatakiwa iwe kwa njia isiyokuwa ndani yake na uchovu wala uzito. Hili hupatikana pale ambapo kwa mfano mlinganizi akatoa suala fulani la kielimu kwa wale waliokaa pale halafu baada ya hapo likaanza kujadiliwa. Ni jambo lenye kujulikana ya kwamba majadiliano na maswali na majibu ni jambo lililo nafasi kubwa katika kufahamu yale aliyoteremsha Allaah kwa Mtume Wake na kuwafanya wengine wakafahamu. Vivyo hivyo njia hii inaweza kuwa na taathira kubwa kuliko khutbah au muhadhara, kama inavyojulikana.

Kulingania katika dini ya Allaah (´Azza wa Jall) ndio kazi ya Mitume wote (´alayhimus-Swalaatu was-Salaam) na ndio njia ya wale waliowafuata kwa wema. Pindi Allaah anapomneemesha mtu akamjua ni nani Mola Wake, ni nani Mtume Wake na ni ipi dini yake, basi kinachompasa ni yeye kufanya bidii kuwaokoa ndugu zake kwa kuwalingania katika dini ya Allaah (´Azza wa Jall) na kuwabashiria kheri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kumwambia ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) siku ya Khaybar:

“Nenda mpaka utapofika katika uwanja wao. Halafu uwalinganie katika Uislamu na uwaeleze kuhusu haki za Allaah (Ta´ala) aambazo ni wajibu juu yao. Naapa kwa Allah! Endapo Allaah atakuongozea mtu mmoja tu ni kheri kwako kuliko kupata ngamia wekundu.”[1]

Muslim vilevile amepokea kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anayelingania kwenye uongofu basi anapata sawa na ujira wa yule atakayemfuata pasi na kupungua chochote katika ujira wao. Na anayelingania katika upotevu basi anapata sawa na madhambi ya yule atakayemfuata pasi na kupungua chochote katika madhambi yao.”[2]

Muslim amepokea tena kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule anayeelekeza katika kheri anapata ujira sawa na yule mwenye kuitenda.”[3]

[1] al-Bukhaariy (2942), Muslim (2407) na Abu ´Awaanah (4/279).

[2] Muslim (2674), Abu Daawuud (4609), at-Tirmidhiy (2764), Ibn Maajah (206), Ahmad (2/397), ad-Daarimiy (513), Ibn Hibbaan (112), Abu Ya´laa (6458) na Abu ´Awaanah (5823).

[3] Muslim (1893), at-Tirmidhiy (2809), Abu Daawuud (5139), Ahmad (4/120), Ibn Hibbaan (289) na Abu ´Awaanah (6/3).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 21-24
  • Imechapishwa: 16/05/2020