05. Kulingania katika kushuhudia ya kwamba hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي

”Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah kwa ujuzi – mimi na anayenifuata.” (02:108)

2- Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi alipomtuma Mu´aadh Yemen alimwambia:

“Hakika wewe unawaendea watu katika watu wa Kitabu, basi iwe kitu cha kwanza utakachowalingania kwacho iwe ni kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah… “

Katika upokezi mwingine imekuja:

“… wampwekeshe Allaah. Ikiwa watakutii kwa hilo, basi wafundishe ya kwamba Allaah amewafaradhishia swalah tano kila mchana na usiku. Ikiwa watakutii kwa hilo, wafundishe ya kwamba Allaah amewafaradhisha zakaah itayochukuliwa kutoka kwa matajiri wao na wapewe mafakiri wao. Ikiwa watakutii kwa hilo, tahadhari na kuwachukulia mali yao. Iogope du´aa ya mwenye kudhulumiwa, kwani hakika hakuna baina yake na baina ya Allaah kizuizi.”[1]

Imepokelewa na al-Bukhaariy na Muslim.

3- al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Sahl bin Sa´d (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema siku ya Khaybar:

“Kuna mtu nitampa bendera kesho, ni mtu anampenda Allaah na Mtume Wake na Allaah na Mtume Wake wanampenda. Allaah atafungua mji kwa mikono yake.” Watu wakabaki macho usiku ule na kutafakari ni nani atapewa nayo. Ilipofika asubuhi wakaamkia mapema kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kila mmoja akitaraji atapewa yeye. Akasema: “Yuko wapi ´Aliy bin Abiy Twaalib.” Akaambiwa: “Ni mgonjwa wa macho.” Akamtumia ujumbe. Akaletwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamtemea mate machoni mwake na kumuombea du´aa. Akapona papo hapo kana kwamba hakuwa mgonjwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akampa bendera na kumwambia: “Nenda zako taratibu na kwa upole mpaka ufike maeneo yao, kisha uwalinganie katika Uislamu na uwaeleze haki za Allaah (Ta´ala) ambazo ni wajibu kwao. Naapa kwa Allaah! Lau Allaah atamuongoza mtu mmoja kupitia kwako ni bora kwako kuliko ngamia wekundu.”[2]

MAELEZO

Mlango unahusiana na ni wajibu kulingania katika kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Shahaadah mbili hizi ni zenye kulazimiana. Makusudio ya mwandishi ni kulingania katika Tawhiyd na kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hili ni wajibu kwa wanachuoni. Mwandishi amethibitisha hilo kwa Qur-aan na Sunnah kama maneno Yake (Ta´ala):

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ

“Lingania katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi.” (16:125)

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي

”Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah kwa ujuzi – mimi na anayenifuata.” (02:108)

وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلًا مِّمَّن دَعَا إِلَى اللَّـهِ

“Na nani aliye na kauli nzuri zaidi kuliko yule anayelingania kwa Allaah.” (41:33)

Ni wajibu kwa wanachuoni kulingania katika Tawhiyd na Allaah atakasiwe ´ibaadah shirki iachwe. Vilevile ni wajibu kulingania katika kumuamini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kusadikishwa, kufuatwa yale aliyokuja nayo na kutomkhalifu.

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي

”Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah kwa ujuzi – mimi na anayenifuata.” (02:108)

Mzungumzishwa hapa ni Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Ummah wake. Sema ya kwamba hii ndio njia yangu ninayopita ambapo nampwekesha Allaah na kumtakasia ´ibaadah, kutoa zakaah na mengineyo. Hii ndio njia ya Allaah iliyonyooka, uongofu na imani.

أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ

“… nalingania kwa Allaah kwa ujuzi… “

Ninalingania katika dini ya Allaah na sio katika ufalme, maslahi, mali au mambo ya kidunia. Ninalingania katika kumpwekesha Allaah Pekee na kufuata Shari´ah Yake na ninafanya hivo kwa ujuzi na uongofu.

أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي

“… mimi na anayenifuata.”

Bi maana wafuasi wangu vilevile wanalingania kwa ujuzi na umaizi. Wafuasi wake wana ujuzi na umaizi. Wanachuoni ambao wanalingania ulinganizi wao wanafanya hivo kwa ujuzi na umaizi. Wanachuoni ambao hawalinganii katika njia ya Allaah sio katika wafuasi zake kihakika. Kwa sababu wafuasi zake hawanyamazi na wala hawalinganii kwa ujinga. Allaah (Ta´ala) amesema:

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ

“Lingania katika njia ya Mola wako kwa hekima… “

Bi maana kwa ujuzi. Hii ndio kazi ya Mitume, wanachuoni na wema wote. Hili ni wajibu kwa yule ambaye yuko na elimu. Anatakiwa kulingania kila mahali ikiwa ni pamoja vilevile na msikitini na sehemu nyenginezo na awe na subira.

2- Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi alipomtuma Mu´aadh Yemen alimwambia:

“Hakika wewe unawaendea watu katika watu wa Kitabu, basi iwe kitu cha kwanza utakachowalingania kwacho iwe ni kushuhudia ya kwamba hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah… “

Katika upokezi mwingine imekuja:

“… wampwekeshe Allaah. Ikiwa watakutii kwa hilo, basi wafundishe ya kwamba Allaah amewafaradhishia swalah tano kila mchana na usiku. Ikiwa watakutii kwa hilo, wafundishe ya kwamba Allaah amewafaradhisha zakaah itayochukuliwa kutoka kwa matajiri wao na wapewe mafakiri wao. Ikiwa watakutii kwa hilo, tahadhari na kuwachukulia mali yao. Iogope du´aa ya mwenye kudhulumiwa, kwani hakika hakuna baina yake na baina ya Allaah kizuizi.”

Maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “Hakika wewe unawaendea watu katika watu wa Kitabu” yanaonyesha kuwa hawakuwa wajinga. Wana elimu na utata. Anamzindua ili amuandae na kufikisha maamrisho ya Allaah.

Maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “Basi iwe kitu cha kwanza utakachowalingania kwacho iwe ni kushuhudia ya kwamba hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” ina maana ya kwamba asibabaike na utata wao na elimu yao. Anachotakiwa ni kuhakikisha amewafikishia Tawhiyd na kuwa wanamuabudu Yeye peke yake na si mwingine kama ´Uzayr, ´Iysaa, marabi na watawa wao. Katika upokezi mwingine imekuja ya kwamba awalinganie katika kumuabudu Allaah peke yake. Hii ndio tafsiri ya kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah.

Maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “Ikiwa watakutii kwa hilo… ” bi maana wakimuabudu Allaah peke yake na si mwingine.

Maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “… basi wafundishe ya kwamba Allaah amewafaradhishia swalah tano kila mchana na usiku” ni dalili yenye kuonesha kuwa mshirikina kwanza anatakiwa kulinganiwa katika Tawhiyd. Akiikubali ndio alinganiwe katika swalah. Akikubali na kuisimamisha ndio analinganiwa katika zakaah ambayo inachukuliwa kutoka kwa matajiri na kupewa mafukara. Wametajwa mafukara kwa sababu ndio muhimu wenye kustahiki zaidi kupewa zakaah. Kadhalika ndio ambao Allaah ameanza pale aliposema:

إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَابْنِ السَّبِيلِ ۖ فَرِيضَةً مِّنَ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

“Hakika Zakaah ni kwa ajili ya mafakiri na masikini na wanaozitumikia na wanaotiwa nguvu nyoyo zao [kwa ajili ya Uislamu] na kuwakomboa mateka na wenye deni na katika njia ya Allaah na msafiri [aliyeharibikiwa]. Ni faradhi itokayo kwa Allaah; na Allaah ni Mjuzi, Mwenye hekima.” (09:60)

Maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “Ikiwa watakutii kwa hilo, tahadhari na kuwachukulia mali yao” bi maana usichukue mali yao yenye thamani kwa nguvu. Chukua kati kwa kati. Kuna mali tukufu, mali ya kati kwa kati na mali isiyokuwa na maana. Hata hivyo lililo bora kwao ni kutoa mali yao tukufu kwa khiyari yao.

Maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “Iogope du´aa ya mwenye kudhulumiwa” bi maana tahadhari na kuwadhulumu wakaja kuomba dhidi yako na kuitikiwa. Du´aa ya mwenye kudhulumiwa ni yenye kuitikiwa.

Mtume (Swalla ALlaahu ´alayhi wa sallam) alitosheka na mambo haya matatu kwa sababu ndio muhimu zaidi. Mwenye kuyakubali hukubali hajj, swawm na mengineyo. Wakiyakubali mambo hayo matatu ya kwanza basi watafanya hivo kwa imani na kukinaika. Imani hiyo hiyo itawafanya kutekeleza mambo mengine ya Shari´ah. Ndio maana Allaah amekomeka nayo kwa kusema:

فَإِن تَابُوا وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ فَخَلُّوا سَبِيلَهُمْ

“Lakini akitubu na wakasimamisha swalah na wakatoa zakaah, basi waacheni huru.” (09:05)

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamuabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia yeye dini kwa imani safi kabisa na ya asli na wasimamishe swalah na watoe zakah.” (98:05)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nimeamrishwa kuwapiga watu vita mpaka washuhudie ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na mimi ni Mtume wa Allaah, wasimamishe swalah na watoe zakaah.”

Misingi hii mitatu ndio muhimu zaidi.

3- al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Sahl bin Sa´d (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema siku ya Khaybar:

“Kuna mtu nitampa bendera kesho, ni mtu anampenda Allaah na Mtume Wake na Allaah na Mtume Wake wanampenda. Allaah atafungua mji kwa mikono yake.” Watu wakabaki macho usiku ule na kutafakari ni nani atapewa nayo. Ilipofika asubuhi wakaamkia mapema kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kila mmoja akitaraji atapewa yeye. Akasema: “Yuko wapi ´Aliy bin Abiy Twaalib.” Akaambiwa: “Ni mgonjwa wa macho.” Akamtumia ujumbe. Akaletwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamtemea mate machoni mwake na kumuombea du´aa. Akapona papo hapo kana kwamba hakuwa mgonjwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akampa bendera na kumwambia: “Nenda zako taratibu na kwa upole mpaka ufike maeneo yao, kisha uwalinganie katika Uislamu na uwaeleze haki za Allaah (Ta´ala) ambazo ni wajibu kwao. Naapa kwa Allaah! Lau Allaah atamuongoza mtu mmoja kupitia kwako ni bora kwako kuliko ngamia wekundu.”

[1] al-Bukhaariy (1395) na Muslim (19).

[2] al-Bukhaariy (309) na Muslim (405).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 30-33
  • Imechapishwa: 20/03/2018