05. Kujitenga mbali na mizozo na kukaa na Ahl-ul-Ahwaa´

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Tunaonelea kuwa Sunnah imejengwa juu ya kushikamana na yale waliyokuwemo Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuwaiga, kujiepusha na Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu, kujiepusha na mizozo na kukaa na Ahl-ul-Ahwaa´… “

MAELEZO

Dalili ya hilo ni maneno Yake (Ta´ala):

وَقَدْ نَزَّلَ عَلَيْكُمْ فِي الْكِتَابِ أَنْ إِذَا سَمِعْتُمْ آيَاتِ اللَّـهِ يُكْفَرُ بِهَا وَيُسْتَهْزَأُ بِهَا فَلَا تَقْعُدُوا مَعَهُمْ حَتَّىٰ يَخُوضُوا فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ ۚ إِنَّكُمْ إِذًا مِّثْلُهُمْ

“Amekwishakuteremshieni katika Kitabu kwamba mnaposikia Aayah za Allaah zinakanushwa na zinafanyiwa istihzai, basi msikae pamoja nao mpaka waingie katika mazungumzo mengineyo. Vinginevyo mtakuwa kama wao.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika Hadiyth Swahiyh:

“Atayesikia kunazungumziwa juu ya ad-Dajjaal basi ajitenge naye mbali. Ninaapa kwa Allaah mtu atajiona ni muumini na amwendee ambapo hatimaye ataanza kumfuata kwa sababu ya shubuha zake.”[2]

Shaykh Ibn Battwah (Rahimahu Allaah) amesema pindi alipokuwa akiitilia taaliki Hadiyth hii:

“Haya ni maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye ni mkweli na ni mwenye kusadikishwa. Waislamu! Mcheni Allaah na asiwepo yeyote atayejiamini na akaamini usahihi wa madhehebu yake ambapo akaja kuiweka khatarini dini yake kwa kukaa na baadhi ya Ahl-ul-Ahwaa´ hawa ili kujadiliana nao au kutaka kuwafanya wakaacha madhehebu yao. Wana fitina kubwa kuliko ad-Dajjaal. Maneno yao yanakamata zaidi kuliko upele na yanaziunguza nyoyo zaidi kuliko moto. Nimewaona watu wengi walikuwa wakiwalaani na wakiwatukana hadharani na baadaye wakakaa nao ili kuwakemea na kuwaraddi. Lakini walikuwa wakionyesha urafiki, vitimbi vya kujificha na kufuru yenye kujificha mpaka hatimaye wakajiunga nao.”[3]

Kuna mtu alikuja kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh) na kumwambia:

“Abu Hamzah! Nimekutana na watu wanaokadhibisha uombezi na adhabu ya ndani ya kaburi.” Akasema: “Hao ni waongo. Usikae nao.”[4]

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Usikae na Ahl-ul-Ahwaa´. Kukaa nao kunazifanya nyoyo kuwa na maradhi.”[5]

Abul-Jawzaa´, ambaye alikuwa ni mmoja katika wakubwa wa Taabi´uun, amesema:

“Kuwa na jirani ngedere au nguruwe ni afadhali kuliko mmoja katika wao.”[6]

Bi maana Ahl-ul-Ahwaa´.

al-Fudhwayl bin ´Iyaadh amesema:

“Usikae na wazushi. Ninachelea usije ukashukiwa na laana.”[7]

Kuna watu wawili katika Ahl-ul-Ahwaa´ walikuja kwa Muhammad bin Siyriyn na kumwambia:

“Abu Bakr! Hebu tukusimulie Hadiyth.” Akasema: “Hapana.” Wakasema: “Hebu tukusomee Aayah kutoka katika Kitabu cha Allaah.” Akasema: “Hapana. Ima msimame nyinyi kutoka kwangu au mimi nitasimama.” Walipoenda zao baadhi ya watu wakasema: “Abu Bakr! Ungefanyika nini endapo wangekusomea Aayah kutoka katika Kitabu cha Allaah?” Akajibu: “Nimechelea wangenisomea Aayah na wakaikengeusha na hivyo ikakita kwenye moyo wangu.”[8]

´Abdur-Razzaaq amesema:

“Ibraahiym bin Muhammad bin Abiy Yahyaa alinambia: “Naona Mu´tazilah ni wengi kwenu.” Nikajibu: “Ndio na wanadai kuwa wewe ni mmoja wao.” Akasema: “Si uje na mimi tuingie kwenye duka hili ili nikuzungumzishe?” Akajibu: “Hapana.” Akasema: “Kwa nini?” Nikasema: “Moyo ni dhaifu na dini sio kwa yule mshindi.”[9]

Mubashshir bin Ismaa´iyl al-Halabiy amesema:

“Kulisemwa kuambiwa al-Awzaa´iy ya kwamba kuna mtu anasema kuwa yeye anakaa na Ahl-us-Sunnah na Ahl-ul-Bid´ah. al-Awzaa´iy akasema: “Huyu ni mtu anayetaka kusawazisha haki na badili.”[10]

[1] 04:140

[2] Abuu Daawuud (4319). Swahiy kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Mishkaah” (5488).

[3] al-Ibaanah al-Kubraa (2/469).

[4] al-Ibaanah al-Kubraa (2/448).

[5] al-Ibaanah al-Kubraa (2/438).

[6] al-Ibaanah al-Kubraa (2/467).

[7] al-Ibaanah al-Kubraa (2/459).

[8] ad-Daarimiy (411).

[9] al-Ibaanah al-Kubraa (1/65).

[10] al-Ibaanah al-Kubraa (2/456).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 74-77
  • Imechapishwa: 28/01/2017