05. Kuifanya imani kuwa na nguvu


Lengo la tano: Kuzidisha imani

Miongoni mwa malengo ya hajj ni kuifanya imani kuwa na nguvu. Ni jambo linalotambulika kwamba imani inazidi na inapungua. Uchaji Allaah unadhoofika. Imani inazidi kwa kumdhukuru Allaah, kumtii, kutubia Kwake na kuelekea Kwake (Tabaarak wa Ta´ala) kwa uzuri. Vilevile inapungua kwa kughafilika, kufanya michezo, kwa kufanya maasi na madhambi. Hajj inachukuliwa ni sehemu kubwa ya kuzitengeneza nafsi, kuzitengeneza nyoyo na kuzidisha imani. Ndani yake kuna darsa ngapi nzuri na mawaidha yenye kuathiri yanayozielekeza nyoyo kwa Allaah (´Azza wa Jall), kumfanya mtu akawa na shauku kubwa, woga mkubwa, matumaini makubwa, khofu kubwa na akatubu kwa wingi! Ni machozi mangapi ya kweli katika hajj yamemwagwa! Ni tawbah ngapi za kweli zimekubaliwa! Ni makosa mangapi yamesamehewa! Ni du´aa ngapi za unyenyekevu zimekubaliwa! Ni watu wangapi wanaoachwa huru kutokamana na Moto!

Uwanja na sababu za kuifanya imani kuwa na nguvu katika hajj ni nyingi na ziko aina mbalimbali. Hajj inafuta yaliyokuwa kabla yake. Hajj yenye kukubaliwa haina malipo isipokuwa Pepo. Mwenye kuitekeleza bila maneno machafu wala kufanya kitendo cha ndoa, basi anatoka katika madhambi yake kama ile siku aliyozaliwa na mama yake. Hajj inafuta madhambi kama ambavyo kile chombo cha kufua chuma kinavyoondoa na kusafisha uchafu wa dhahabu na fedha. Yote hayo zimesihi Hadiyth kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Ni mara ngapi hajj imekuwa ndio chanzo cha mabadiliko katika maisha ya watu wengi kutoka katika hali mbaya na kwenda katika hali nzuri, kutoka katika hali nzuri kwenda katika hali bora zaidi! Ushahidi juu ya haya na uhalisia wenye kuyatia nguvu hauwezi kudhibitiwa.

Ni mahujaji wangapi wamechunga zile nyakati za kuitikiwa du´aa katika hajj na wakanyanyua mikono yao kwa Mola wao hali ya kuwa ni wenye kunyenyekea, kujidhalilisha, kutaraji fadhilah Zake kuu na wakaomba Azifanye upya imani zao katika mioyo yao na Awathibitishe juu yake, awaondoshee fitina zilizo dhahiri na zilizojificha, awatengenezee maisha ya dunia yao na Aakhirah yao, awapambe kwa pambo la imani na awafanye kuwa miongoni mwa waongofu wenye kuongoza! Allaah (´Azza wa Jall) hamwachi bure mja mwenye kumuomba na wala hamrudishi mja mwenye kumnong´oneza. Kwani Yeye ndiye kasema (Subhaanah):

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ

“Watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi [wajuze kwamba] Mimi Niko karibu Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Hivyo basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi wapate kuongoka.”[1]

Imethibiti katika Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Mahujaji na wenye kufanya ´Umrah ni wageni wa Allaah. Amewaita wakamuitikia. Wakamuomba akawapa.”

Itafakari ile hali ya mahujaji ambao wameziacha nchi zao, familia zao, biashara zao, manufaa yao na wakabeba uzito wa kusafiri kisha alipofika katika Miyqaat akavua yale mavazi aliyozowea kuyavaa na akanyenyekea kwa Mola wake ambapo akavaa mavazi ya unyenyekevu; Izaar na Ridaa´ na huku akakiacha wazi kichwa chake. Sambamba na hilo akatembelea kwa kujidhalilisha na kwa unyenyekevu kuelekea katika Nyumba ya Allaah kongwe akisema:

“Nimekuitikia, ee Allaah, nimekuitikia. Nimekuitikia, hauna Wewe mshirika, nimekuitikia. Hakika himdi zote, neema na ufalme ni Wako. Hauna mshirika Wewe.”

Akiirudirudi mpaka atapofika katika Nyumba ya Allaah na akiirudirudi tena wakati wa kwenda huku na kule katika zile nembo za hajj. Haya yana athari kiasi gani katika maisha ya mwanaadamu inapokuja katika mwenendo wake na tabia yake na khaswakhaswa ikiwa anahisi maana hizi na akazihudhurisha kwenye moyo wake? Hapana shaka kwamba huu ni mlango mkubwa kabisa katika kuifanya imani kuwa na nguvu na kuzidi.

Ni zaidi kwa yule ambaye Allaah (´Azza wa Jall) amemkirimu kuhiji awe katika hajj yake ni mnyenyekevu kwa Mola wake na awe na hali ya udhalilikaji mbele Yake na huku akitarajia huruma na msamaha Wake na sambamba na hilo anaiogopa adhabu na hasira Zake. Awe ni mwenye kutubia juu ya kila dhambi iliyotendwa na mikono yake, kila dhambi iliyoendewa na miguu yake, kukithirisha kumdhukuru Allaah, du´aa, msamaha na unyenyekevu. Lengo anatakiwa atoke katika hajj kwa mabadiliko mazuri na arudi nchini kwake na kwa familia yake akiwa na hali bora kabisa. Anatakiwa aanze ukurasa mpya katika maisha yake uliyopambwa na matendo mema na kuwa na msimamo kwa moyo wenye utulivu, nafsi na kifua vyenye kutubia hali ya kuwa ni mwenye kumuomba Allaah uthabiti juu ya imani na kusalimika kutokamana na fitina mbalimbali.

[1] 02:186

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Maqaaswid-ul-Hajj, uk. 24-28
  • Imechapishwa: 16/08/2018