05. Kufaa kukosa swalah ya mkusanyiko kwa aliye na udhuru wa ki-Shari´ah


Swali 05: Naishi katika nyumba ambayo hakuna isipokuwa baba na mke wangu na watoto wawili wadogo. Wakati mmoja baba yangu aliniamrisha kwenda kuswali msikitini. Lakini mke wangu aliniapia kwa jina la Allaah kwamba sintotoka nyumbani isipokuwa baada ya baba yangu kurudi kutoka msikitini kwa kukhofia asibaki mwenyewe. Wakati baba yangu aliporudi akaniuliza sababu ilionifanya kutoenda msikitini ambapo nikamweleza kwamba nimeapiwa kwa jina Allaah nisende kuswali msikitini na badala yake niswali nyumbani. Nikamweleza [mke wangu] kwamba kuswali msikitini ni bora kuliko kuswali nyumbani na kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hapana swalah kwa anayeishi karibu na msikiti isipokuwa msikitini.”

Pamoja na hivyo akanisisitiza kuswali nyumbani na kwamba nikitoka nje basi hatoniruhusu kuingia nyumbani tena ambapo nikamtii kwa kutii amri yake. Tunaomba utupe fatwa Allaah akujaze kheri khaswa kwa kuzingatia kwamba mwanamke daima analalamika kubaki peke yake nyumbani[1].

Jibu: Ikiwa kuna khatari juu ya mke wako na hayuko salama na pambizoni mwake kuna yanayokhofiwa juu yake, basi unao udhuru wa kuswali nyumbani kwa kuchelea juu ya mke wako. Lakini mahali pakiwa na amani na hakuna utata juu ya kile anachosema mke, si venginevyo isipokuwa ni kuchukulia kwake wepesi, basi unatakiwa kuswali msikitini. Utatakiwa kumtii baba yako kwa yale mema anayokuamrisha. Bali unatakiwa kumtii Allaah kabla ya baba yako. Ni lazima kwako kuswali msikitini pamoja na waislamu wengine. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayesikia adhaana na asiitikie basi hana swalah isipokuwa akiwa na udhuru.”[2]

Bwana mmoja kipofu alisema: “Ee Mtume wa Allaah! Sina kiongozi wa kuniongoza msikitini. Je, ninayo ruhusa ya kuswali nyumbani kwangu?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuuliza: “Je, wasikia wito wa swalah?” Akasema: “Ndio.” Akasema: “Basi imewajibika.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwamrisha kipofu ambaye hana kiongozi wa kumwongoza kuswali msikitini na wala hakumpa udhuru. Wewe una haki zaidi [ya kuamrishwa]. Hulazimiki kumtii baba katika kwenda kinyume na Shari´ah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika si venginevyo utiifu unakuwa katika mema.”[4]

“Hakuna utiifu kwa kiumbe katika kumuasi Muumba.”[5]

Lakini ikiwa mke hayuko salama, maeneo hapako salama na khatari ipo, basi hapana vibaya kuswali nyumbani. Huu ni udhuru unaokubalika katika Shari´ah.

Kuhusu Hadiyth isemayo:

“Hapana swalah kwa anayeishi karibu na msikiti isipokuwa msikitini.”

ni dhaifu na haikuhifadhiwa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Imetangaa kutoka kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh). Lakini kumesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yale yanayotosheleza kutoihitajia. Nazo ni zile Hadiyth mbili zilizotangulia:

“Yeyote atakayesikia adhaana na asiitikie basi hana swalah isipokuwa akiwa na udhuru.”[6]

Pia Hadiyth ya kipofu ambayo tumetangulia kuitaja. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia:

“Imewajibika.”

Hadiyth hizi mbili Swahiyh zinatosheleza kutohitajia Hadiyth isemayo:

“Hapana swalah kwa anayeishi karibu na msikiti isipokuwa msikitini.”

Tunacholenga ni kwamba ni lazima kwa waislamu wanne kuswali msikitini, wakithirishe wingi wa waislamu, watoke kuelekea msikitini na wala wasijifananishe na wanafiki. Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Tulikuwa tukiona hakuna anayeiacha – swalah ya mkusanyiko – isipokuwa ni mnafiki ambaye unatambulika unafiki wake au mgonjwa. Mtu alikuwa akibebwa kati ya watu wawili mpaka anasimamishwa katika safu.”[7]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitamani kuzitia moto nyumba za wale wanaobaki nyuma kuacha swalah ya mkusanyiko.

Kwa hivyo ni lazima kwako na kwa kila muislamu muweza kuswali msikitini. Haifai kwake kuswali nyumbani isipokuwa kutokana na udhuru unaokubalika katika Shari´ah.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/41-44)

[2] Ibn Maajah (785).

[3] Muslim (653) na an-Nasaa´iy (850).

[4] al-Bukhaariy (6612) na Muslim (3424).

[5] Ibn Abiy Shaybah (15564).

[6] Ibn Maajah (785).

[7] Muslim (1045).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 28-31
  • Imechapishwa: 24/11/2021