05. Ibn Laadin Hakuisalimisha Hata Makkah Na al-Madiynah


Wale wanaosema kuwa Usaamah bin Laadin ni mwenye kueneza ufisadi katika ardhi na mwenye jukumu kubwa ya fitina inayowakumba waislamu ulimwenguni, wana dalili nyingi za Kishari´ah na dalili za kiakili juu ya hilo. Uislamu unaharamisha mgawanyiko. Usaamah bin Laadin na wafuasi wake wameleta mgawanyiko na kutumbukia kwenye madhambi. Wanachuoni watukufu Saudi Arabia na nchi nyinginezo wamewahimiza kurejea kwenye akili yao timamu. Wakakataa. Wakaendelea kwenye upotevu wao baada ya kufikiwa na haki. Wakaedeleza ufisadi wao kwa fikira zao, bidii zao, maisha yao na mali zao na kwenda kinyume na njia ya waumini ambayo Allaah Ameamrisha kuifuata na kukataza kwenda kinyume nayo kwa mujibu wa wanachuoni wote katika Ummah. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Amesema:

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

“Na atakayempinga Mtume baada ya kuwa umeshambainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya Waumini, Tutamgeuza alikogeukia na [baada ya hapo] Tutamuingiza [Moto wa] Jahannam – na uovu ulioje marudio ya mwisho!” (04:115)

Jihaad ina masharti yake, vidhibiti vyake na makatazo yake katika Shari´ah yenye hekima. Ibn Laadin na kundi lake wakapuuza yote hayo. Alichofanya kiongozi wa al-Qaa´idah ni kuwadanganya vijana na wapumbavu kufanya milipuko isiyokuwa na maana kwa silaha zenye kuangamiza Saudi Arabia ikiwa ndio msingi. Bali uhakika wa mambo ni kwamba miji miwili mitukufu Makkah na al-Madiynah haikusalimika na jarima za ulipuaji ambazo Ibn Laadin ndiye anayezingatiwa kusimama nyuma ya yote hayo mpaka hii leo. Hakika dalili za Kishari´ah zinaharamisha matendo haya machafu ambayo anabebeshwa nayo [Ibn Laadin] na kutumiwa hoja na waharibifu ambao hawataki kupokea nasaha za wanasihiaji na wala hawamrehemu mtoto wala mzee, mwenye nguvu wala dhaifu, wanaume wala wanawake, watawala wa Kiislamu wala wanachuoni watukufu. Wao wanawaheshimu tu wale wanaofanana na wao na wale wenye kutekeleza yale wanayoamrishwa na viongozi wa al-Qaa´idah wakati wao wenyewe wako nyuma ya majibali ya Afghanistan. Shari yake imeacha nyayo kubwa ulimwenguni kupitia wapumbavu ambao wamekosa rehema kwenye nyoyo zao na kuweka nafasi yake uadui na chuki kwa watu wengine wote.

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Waqafaat wa Ma´aalim, uk. 12-14
  • Imechapishwa: 13/12/2014