05. Hadiyth “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alfajiri ilikuwa ikimkuta… “


Hadiyth ya tano

05- ´Aaishah mama wa waumini (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alfajiri ilikuwa ikimkuta akiwa na janaba kutokana na mke wake kisha anaoga na kufunga.”

Maana ya kijumla:

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifanya jimaa usiku na wakati mwingine alfajiri ikimkuta akiwa na janaba bado hajaoga. Lakini anakamilisha swawm yake na halipi. Hukumu hii inafanya kazi katika Ramadhaan na miezi mingine. Haya ndio madhehebu ya wanachuoni wengi. Hakuna waliowakhalifu isipokuwa wachache miongoni mwa wale ambao tofauti zao hazizingatiwi. Kuna ambao wamesimulia maafikiano juu ya maoni haya.

Faida zinazochukuliwa kutoka katika Hadiyth:

1- Mtu ambaye amefanya jimaa usiku na akaamka akiwa na janaba swawm yake ni sahihi.

2- Kunatumiwa kipimo (Qiyaas) juu ya jimaa mtu akaota, jambo ambalo lina haki zaidi. Kwa sababu ikiwa mtu ambaye amefanya kwa khiyari yake amepewa ruhusa, basi mwingine ana haki zaidi.

3- Hapana tofauti kati ya swawm ya wajibu na ya sunnah, Ramadhaan na miezi mingine.

4- Inajuzu kufanya jimaa nyusiku za Ramadhaan ijapokuwa ni karibu na kuingia kwa alfajiri. Kuna baadhi wameonelea kuwa inafaa kwa mwenye janaba kufunga hali ya kutoa katika maneno Yake (Ta´ala):

أُحِلَّ لَكُمْ لَيْلَةَ الصِّيَامِ الرَّفَثُ إِلَىٰ نِسَائِكُمْ

“Mmehalalishiwa usiku wa kufunga kuingiliana na wake zenu.” (01:187)

Kwa sababu Aayah inapelekea kujuzu kufanya jimaa usiku mzima kukiwemo karibu na kuingia kwa alfajiri. Katika udharurah wake ni mtu kuamka akiwa na janaba. Dalili hii ni ya ishara kwa Usuuliyyuun.

5- Fadhilah za wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wema wao juu ya Ummah. Kwani hakika wamenukuu sehemu kubwa ya elimu yenye manufaa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na khaswa hukumu za Kishari´ah za kinyumba ambazo hakuna ambao wanaweza kuzitambua isipokuwa wao tu kutoka katika matendo ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – Allaah awawie radhi na wao wawe radhi Naye.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdullaah bin ´Abdir-Rahmaan al-Bassaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-´Allaam Sharh ´Umdat-il-Ahkaam, uk. (01/318-319)
  • Imechapishwa: 25/05/2018