1- Inajuzu kwa mfungaji kunuia swawm na huku yuko na janaba kisha akaoga baada ya kuingia kwa alfajiri.

2- Ni wajibu kwa mwanamke akisafika kabla ya alfajiri katika Ramadhaan kutokamana na hedhi au nifasi afunge ijapokuwa hatowahi kuoga isipokuwa baada ya kuingia alfajiri.

3- Inajuzu kwa mfungaji kutoa gego lake au jino lake, kutia dawa kwenye jeraha/donda lake na vilevile kutia dawa za matone machoni mwake au kwenye masikio yake. Hakufungui kwa kufanya hivo hata kama atahisi ladha ya matone kooni mwake.

4- Inajuzu kwa mfungaji kutumia Siwaak mwanzoni mwa mchana na mwishoni mwake. Ni Sunnah kwake kama wasiofunga.

5- Inajuzu kwa mfungaji kufanya yale mambo yatayompunguzia ukali wa joto na kiu. Mfano wa mambo hayo ni kama kujitia baridi kwa maji na kiyoyozi (air conditioner).

6- Inajuzu kwa mfungaji kupuliza mdomoni mwake yanayopunguza dhiki ya kupumua inayotokamana na pumu au mengineyo.

7- Inajuzu kwa mfungaji kulowesha lips/midomo yake ikikauka na kuusukutua mdomo wake ukikauka pasi na kuichezesha kooni.

8- Ni Sunnah kwa mfungaji kuchelewesha daku mpaka kabla ya alfajiri na kuharakisha kukata swawm baada tu ya kuzama jua. Anatakiwa kukata swawm kwa tende tosa, kama hakupata akate swawm kwa tende za kawaida, kama hakupata akate swawm kwa maji na hakupata akate swawm kwa chakula chochote kile ambacho ni halali.  Asipopata kabisa basi anuie kukata swawm kwa moyo wake mpaka pale atapopata [cha kukatia swawm].

9- Imesuniwa kwa mfungaji kukithirisha matendo mema na kujiepusha na yale yote yaliyokatazwa.

10- Ni wajibu kwa mfungaji kuhifadhi yale mambo yaliyowajibishwa na kujiepusha na yale mambo yaliyoharamishwa. Anatakiwa kuswali vipindi vitano kwa wakati wake na aziswali pamoja na mkusanyiko – ikiwa ni miogoni mwa wale watu wanaotakiwa kufanya hivo – na aache uongo, kusengenya, kughushi, miamala inayohusiana na ribaa na kila neno au kitendo cha haramu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Asiyeacha maneno ya uongo, kuutendea kazi na ujinga, basi Allaah hana haja kwa yeye kuacha chakula na kinywaji chake.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

Himdi zote anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na salaam zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wake wote.

Imeandikwa na fakiri kwa Allaah; Muhammad Swaalih al-´Uthaymiyn.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nubadh fiys-Swiyaam, uk. 05-06
  • Imechapishwa: 17/05/2018