Ramadhaan ndio mwezi bora katika mwaka. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameufanya kuwa ni maalum swawm yake kuwa ni faradhi na nguzo ya nne katika nguzo za Uislamu. Amewawekea katika Shari´ah waislamu kusimama nyusiku zake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Uislamu umejengwa juu ya vitano; kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kwenda kuhiji Nyumba.”[1]

“Atayesimama [nyusiku za] Ramadhaan kwa imani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”[2]

Swawm ina faida na hekima tele. Miongoni mwazo ni kuusafisha moyo na kuutakasa kutokamana na tabia na sifa mbaya kama mfano wa shari, jeuri na ubakhili. Badala yake kuipa mazoezi ya tabia njema kama mfano wa subira, upole, kutoa na ukarimu. Nafsi inafanyishwa mapambano na yale yanayomridhisha Allaah na kumfanya mtu akamkaribia.

Faida na hekima nyingine ni kuwa mja anaitambua nasfi yake, udhaifu wake, haja yake na ufakiri wake kwa Mola. Swawm inamkumbusha neema za Allaah kwake. Swawm inamkumbusha vilevile haja za ndugu zake mafakiri na kwamba anatakiwa kuwaangalia. Haya yanapelekea yeye kumshukuru Allaah (Subhaanah) na kuzitumia neema Zake katika kumtii. Yanapelekea vilevile kukabiliana vizuri na ndugu zake mafakiri na kuwatendea wema. Allaah ameashiria faida hii pale aliposema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa kufunga kama ilivyofaradhishwa kwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Allaah.”[3]

Ameweka wazi (Subhaanah) ya kwamba ametuwekea swawm ili tumche (Subhaanah). Ni dalili inayoonyesha kuwa swawm ni njia inayopelekea katika uchaji Allaah. Uchaji Allaah maana yake ni kumtii Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kutekeleza yale waliyoamrisha na kujiepusha na yale waliyokataza. Yote hayo yafanyike kwa kumtakasia nia Allaah, kumpenda na kumwogopa. Kwa njia hiyo mja anakuwa mwenye kuepuka adhabu na ghadhabu za Allaah. Swawm ina ngazi kubwa ya uchaji Allaah na kukurubisha kwa Mola (´Azza wa Jall). Swawm ina mchango mkubwa pia wa kumcha Allaah katika mambo ya kidunia na ya kidini. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Enyi kongamano la vijana! Yule katika nyinyi mwenye uwezo na aoe. Hakika hilo linasahilisha kushusha macho na kuhifadhi tupu. Kwa ambaye hawezi na afunge. Hakika hiyo ni ngao.”[4]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amebainisha kuwa swawm ni ngao na inamtwaharisha. Swawm anatembea ndani ya mwanaadamu kama ambavyo damu inatembea ndani ya mishipa ilihali swawm inafunga njia hizo na inamkumbusha Allaah na ukubwa Wake. Matokeo yake zinadhoofika nguvu za shaytwaan na upande mwingine nguvu za imani zinakuwa na nguvu zaidi. Kwa hiyo matendo mema yanakuwa mengi zaidi  na maasi yanapungua.

Miongoni mwa faida zake vilevile ni kuwa swawm inasafisha tumbo kutokamana na michanganyiko isiyosalimika. Inampa afya nzuri na nguvu. Hili linakubalika na madaktari wengi ambao wametibu magonjwa mengi kwa swawm. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwanaadamu hajapatapo kujaza chombo kibaya kama tumbo. Inatosha kwa mwanaadamu kutumia matonge kadhaa kuunyoosha mgongo wake. Ikiwa hana budi basi afanye theluthi iwe ya chakula chake, theluthi iwe ya maji yake na theluthi kwa ajili ya nafsi yake.”[5]

Hadiyth hii ni Swahiyh na inafahamisha kuwa haikupendekezwa kupindukia katika kula. Bali ni jambo la khatari. Inatosha kwa mwanaadamu kwa siku kutumia tu kile chenye kumfanya akawa na afya na kunyoosha mgongo wake.

Ee waislamu! Kimbilieni kumcha Allaah (´Azza wa Jall) na kutafuta radhi Zake. Pambaneni na nafsi zenu juu ya kumcha Allaah (´Azza wa Jall) na hakikisheni daima mnatubia kikweli juu ya madhambi yote. Yapigeni vita matamanio, shaytwaan na nafsi yenye kuamrisha sana maovu. Ipupieni Nyumba ya Aakhirah. Mdhalilikieni Mola Wenu (´Azza wa Jall). Kithirisheni kumuomba du´aa na kumdhukuru kwa wingi na kumuomba msamaha. Ataziitikia du´aa zenu, kuzitengeneza hali zenu, kuwafanyia wepesi mambo yenu, kuwatunuku fadhila Zake, kuwasalimisheni na majanga yote na kuwalindeni na njama za maadui wenu na kila baya duniani na Aakhirah. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَالَّذِينَ جَاهَدُوا فِينَا لَنَهْدِيَنَّهُمْ سُبُلَنَا ۚ وَإِنَّ اللَّـهَ لَمَعَ الْمُحْسِنِينَ

“Na wale waliofanya juhudi kwa ajili Yetu, bila shaka Tutawaongoza njia Zetu. Hakika Allaah yu pamoja na wafanyao wema.”[6]

وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَىٰ لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا ۚ يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا

“Allaah amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi – kama alivyowafanya makhalifa wale waliokuwa kabla yao – na atawamakinishia dini yao aliyowaridhia na atawabadilishia amani badala ya khofu yao – [kwa sharti] wananiabudu Mimi na hawanishirikishi na chochote.”[7]

وَإِن تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا لَا يَضُرُّكُمْ كَيْدُهُمْ شَيْئًا ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ

“Mkisubiri na mkaogopa haitokudhuruni chochote katika hila zao. Hakika Allaah ni mwenye kuyazunguka yote wayatendayo.”[8]

إِنَّ لِلْمُتَّقِينَ عِندَ رَبِّهِمْ جَنَّاتِ النَّعِيمِ

“Hakika wachaji Allaah watapata kwa Mola wao mabustani ya neema.”[9]

Ni jambo zuri kabisa hii leo mtu akajikurubisha kwa Allaah kwa kuwahurumia mafukara na wahitaji na kuwatendea wema. Hakika swadaqah ni miongoni mwa matendo makuu ambayo kwayo Allaah anazuia matatizo na kutunuku rehema. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَأَنفِقُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَلَا تُلْقُوا بِأَيْدِيكُمْ إِلَى التَّهْلُكَةِ ۛ وَأَحْسِنُوا ۛ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ

“Toeni katika njia ya Allaah wala msijitupe kwa mikono yenu katika maangamizi. Na fanyeni wema – Hakika Allaah anapenda wafanyao wema.”[10]

إِنَّ رَحْمَتَ اللَّـهِ قَرِيبٌ مِّنَ الْمُحْسِنِينَ

“Hakika Rahmah ya Allaah iko karibu na wafanyao wema.”[11]

وَأَن تَصَدَّقُواْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Mkitoa swadaqah basi ni kheri kwenu – mkiwa mnajua.”[12]

آمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَأَنفِقُوا مِمَّا جَعَلَكُم مُّسْتَخْلَفِينَ فِيهِ ۖفَالَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَأَنفَقُوا لَهُمْ أَجْرٌ كَبِيرٌ

“Muaminini Allaah na Mtume Wake na toeni kutokana na yale aliyokurithisheni; basi wale walioamini miongoni mwenu na wakatoa watapata ujira mkubwa.”[13]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swadaqah inafuta madhambi kama jinsi maji yanazima moto. Hali kadhalika swawm ya mtu usiku.”

Kisha akasoma:

تَتَجَافَىٰ جُنُوبُهُمْ عَنِ الْمَضَاجِعِ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ خَوْفًا وَطَمَعًا وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Mbavu zao zinatengana na vitanda wanamuomba Mola wao kwa khofu na matumaini na katika yale tuliyowaruzuku wanatoa. Basi nafsi yoyote haijui yaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho. Ni malipo kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.”[14]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwingi wa Rahmah anawarehemu wenye huruma. Warehemu walio juu ya ardhi atakurehemuni Aliye juu ya mbingu.”[15]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Asiyerehemu harehemewi.”[16]

Tunamuomba Allaah azitengeneze hali za waislamu wote, azijaze nyoyo zao uchaji Allaah na awatengeneze viongozi wao na awafanye wote waweze kutubia kikweli kutokamana na madhambi yao na wawe na msimamo washikamane na Shari´ah ya Allaah (´Azza wa Jall) katika mambo yote. Tunamuomba Allaah awalinde kutokamana na njama za maadui wao. Hakika Yeye juu ya kila kitu ni muweza. Swalah na amani zimwendee mja na Mtume Wake Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wake.

[1] al-Bukhariy (8) na Muslim (16).

[2] al-Bukhaariy (1901) na (2014) na Muslim (670).

[3] 02:183

[4] al-Bukhaariy (5065) na Muslim (1400).

[5] at-Tirmidhiy (2380), Ibn Maajah (3349) na Ahmad (17225). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (5674).

[6] 29:69

[7] 24:55

[8] 03:120

[9] 68:34

[10] 02:195

[11] 07:56

[12] 02:280

[13] 57:07

[14] 32:16-17 Ibn Maajah (3973) na Ahmad (22069). Swahiyh kwa njia zingine kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (2866).

[15] Abu Daawuud (4941), at-Tirmidhiy (1924) na Ahmad (6494). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (3522).

[16] al-Bukhaariy (5997) na Muslim (2318).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mufiyd fiy Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 18-21
  • Imechapishwa: 02/04/2022