Katika ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni pamona na kuonelea kuwa imani ni kutamka shahaadah ya upwekeshaji ya kwamba hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kuyaamini yakini maneno haya na matendo ya viungo vya mwili. Imaam ash-Shaafi´iy amesema:

“Maswahabah, Taabi´uun na wale tuliokutana nao walikuwa ni wenye kuafikiana kwa kusema kwamba imani ni maneno, matendo na nia. Mtu halipwi kwa kuacha moja katika hivyo vitatu.”

Imepokelewa na al-Laalakaa´iy katika “as-Sunnah”.

Imani inazidi kwa utiifu na inapungua kwa maasi. Allaah (Ta´ala) amesema:

الَّذِينَ قَالَ لَهُمُ النَّاسُ إِنَّ النَّاسَ قَدْ جَمَعُوا لَكُمْ فَاخْشَوْهُمْ فَزَادَهُمْ إِيمَانًا

“Wale walioambiwa na watu: “Hakika watu wamejumuika dhidi yenu, basi waogopeni” yakawazidishia imani… ” (03:173)

وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ

“Wanaposomewa Aayah Zake huwazidishia imani na kwa Mola wao wanategemea.” (08:02)

وَإِذَا مَا أُنزِلَتْ سُورَةٌ فَمِنْهُم مَّن يَقُولُ أَيُّكُمْ زَادَتْهُ هَـٰذِهِ إِيمَانًا ۚ فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا فَزَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَهُمْ يَسْتَبْشِرُونَ

“Na inapoteremshwa Suurah, basi miongoni mwao wako wanaosema: “Nani kati yenu [Suurah] hii imemzidishia imani?” Ama wale walioamini huwazidishia imani nao wanafurahia.” (09:124)

وَلَمَّا رَأَى الْمُؤْمِنُونَ الْأَحْزَابَ قَالُوا هَـٰذَا مَا وَعَدَنَا اللَّـهُ وَرَسُولُهُ وَصَدَقَ اللَّـهُ وَرَسُولُهُ ۚ وَمَا زَادَهُمْ إِلَّا إِيمَانًا وَتَسْلِيمًا

“Basi waumini walipoona yale makundi, walisema: “Haya ndio yale aliyotuahidi Allaah na Mtume Wake na amesema kweli Allaah na Mtume Wake – na haikuwazidishia isipokuwa imani na kujisalimisha.” (33:22)

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ السَّكِينَةَ فِي قُلُوبِ الْمُؤْمِنِينَ لِيَزْدَادُوا إِيمَانًا مَّعَ إِيمَانِهِمْ

“Yeye ndiye Aliyeteremsha utulivu katika nyoyo za waumini ili awazidishie imani pamoja na imani zao.” (48:04)

وَيَزْدَادَ الَّذِينَ آمَنُوا إِيمَانًا

“Na iwazidishie imani wale walioamini.” (74:31)

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwa Ibn ´Umar ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwatolea mawaidha wanawake na akawaambia:

“Sijaona walio na akili punguani na dini pungufu wanaomghalibu mtu mwenye busara kama nyinyi [wanawake].”

Hii ni dalili juu ya kupungua kwa imani. Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Muumini aliye na imani kamilifu zaidi ni yule aliye na tabia njema zaidi.”

Ameipokea Ahmad na wengineo kutoka kwa Abu Hurayrah.

Ikiwa ambaye yuko na imani kamilifu zaidi ana tabia njema zaidi, basi aliye na tabia mbaya ana imani pungufu zaidi.

Imani sio maneno na matendo peke yake pasi na kuamini, kwa kuwa hii ni imani ya wanafiki. Amesema (Ta´ala):

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ آمَنَّا بِاللَّـهِ وَبِالْيَوْمِ الْآخِرِ وَمَا هُم بِمُؤْمِنِينَ

“Na miongoni mwa watu wako wasemao: ”Tumemuamini Allaah na siku ya Mwisho”, hali ya kuwa si wenye kuamini.”” (02:08)

Wala imani sio kule kuwa na utambuzi peke yake, kwa kuwa hii ni imani ya makafiri na wakanamungu. Amesema (Ta´ala):

وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَيْقَنَتْهَا أَنفُسُهُمْ ظُلْمًا وَعُلُوًّا

“Wakazikanusha na hali kuwa nafsi zao zimeziyakinisha kwa dhuluma na majivuno.” (27:14)

فَإِنَّهُمْ لَا يُكَذِّبُونَكَ وَلَـٰكِنَّ الظَّالِمِينَ بِآيَاتِ اللَّـهِ يَجْحَدُونَ

“Hakika wao hawakukadhibishi wewe lakini madhalimu wanakanusha Aayah za Allaah.” (06:33)

الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَعْرِفُونَهُ كَمَا يَعْرِفُونَ أَبْنَاءَهُمْ

“Wale Tuliowapa Kitabu wanatambua kama wanavyowatambua watoto wao.” (02:146)

فَلَمَّا جَاءهُم مَّا عَرَفُواْ كَفَرُواْ بِهِ

“Yalipowajia yale waliyokuwa wakiyatambua waliyakanusha.” (02:89)

وَعَادًا وَثَمُودَ وَقَد تَّبَيَّنَ لَكُم مِّن مَّسَاكِنِهِمْ ۖ وَزَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ فَصَدَّهُمْ عَنِ السَّبِيلِ وَكَانُوا مُسْتَبْصِرِينَ

“Na ‘Aad na Thamuud na yamekwishakubainikieni masikani yao; na shaytwaan aliwapambia matendo yao akawazuia na njia, na walikuwa ni wenye kumaizi.” (29:38)

Kadhalika imani sio maneno na kuamini pasi na matendo. Allaah ameyaita matendo kuwa ni imani. Amesema (Ta´ala):

وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُضِيعَ إِيمَانَكُمْ

“Na Allaah hakuwa Mwenye kupoteza imani zenu.” (02:143)

Bi maana swalah zenu kuelekea Yerusalemu. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kuuambia msafara wa ´Abdul-Qays:

“Ninakuamrisheni mambo mane; kumuamini Allaah na hivi mnajua ni nini kumuamini Allaah? Ni kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kutoa khumusi ya mateka yenu.”

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea vilevile kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Imani ni tanzu sabini na kitu – au ni tanzu sitini na kitu. Bora yake ni kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na ya chini yake ni kuondosha chenye kudhuru njiani. Hayaa pia ni tanzu katika imani.”

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mu´taqad as-Swahiyh, uk. 65-69
  • Imechapishwa: 21/06/2020