05. Ni nani atayepata adhabu kali kati ya mtenda dhambi na mzushi?

Swali 5: Ni nani atayepata adhabu kali kati ya mtenda dhambi na mzushi?

Jibu: Mtu wa Bid´ah ni mbaya zaidi. Mtu wa Bid´ah ni mbaya zaidi kuliko mtenda dhambi. Mtu wa Bid´ah ni mwenye kupendwa zaidi na shaytwaan kuliko mtenda dhambi. Mtenda dhambi hutubu ilihali mzushi ni mara chache mno kutubia[1]. Kwa sababu hujiona kuwa yuko katika haki tofauti na mtenda maasi ambaye hujua kuwa ni muasi na ni mtenda dhambi. Lakini mtu wa Bid´ah yeye huona kuwa ni mtiifu na yumo katika ´ibaadah. Kwa ajili hiyo ndio maana mtu wa Bid´ah akawa ni shari zaidi kuliko mtenda dhambi. Kwa hivyo ndio maana Salaf walitahadharisha kukaa na wazushi. Wanamuathiri yule mwenye kukaa nao[2] na khatari yao ni kubwa zaidi.

Hapana shaka yoyote kuwa mtu wa Bid´ah ni mwenye shari zaidi kuliko mtenda dhambi. Khatari za mtu wa Bid´ah ni kubwa zaidi kwa watu kuliko za mtenda maasi[3]. Ndipo Salaf wakasema:

“Kuwa ni mwenye ukati na kati katika Sunnah ni bora kuliko kuwa ni mwenye bidii katika Bid´ah.”[4]

[1] Sufyaan ath-Thawriy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Bid´ah ni zenye kupendeza zaidi kwa Ibliys kuliko maasi. Maasi mtu hutubia kwayo tofauti na Bid´ah.” (al-Laalakaa’iy (1/132))

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika ya Allaah ameizuia tawbah ya kila mtu wa Bid´ah.” (Ibn-ul-Ja´d (1885). Sahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (54))

[2] Hasan al-Baswriy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Usikae na mzushi. Hakika atautia moyo wako maradhi”. (al-I´tiswaam (1/172) na ”al-Bid´ah wan-Nahiy ´anhaa”, uk. 45)

ash-Shaatwibiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hakika kundi lililookoka wameamrishwa kuwachukia Ahl-ul-Bid´ah, kuwafanyia ukali na kuwaadhibu wale wenye kujiunga nao, ima kwa kuuawa au kitu kingine. Wanazuoni wametahadharisha kutangamana nao na kuketi nao.” (al-I´tiswaam (1/158))

Allaah awarehemu Salaf. Hawakumwacha mzushi yeyote isipokuwa walimponda na kutahadharisha naye.

[3] Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema wakati alipokuwa anataja khatari ya Ahl-ul-Bid´ah:

“Lau Allaah asingefanya kupatikana watu wenye kuraddi madhara ya watu hawa, basi dini ingeliharibika. Madhara haya yangelikuwa makubwa kuliko pindi adui kafiri anapouteka mji. Kwa sababu watu hawa wanapouteka mji uharibifu wao wa miji unafuatiwa na nyoyo na dini yao, lakini kuhusu wazushi huanza kuziharibu nyoyo kwanza.” (Majmuu´-ul-Fataawaa (28/232))

Vilevile amesema (Rahimamu Allaah):

“Kwa mujibu wa Sunnah na maafikiano Ahl-ul-Bid´ah ni wenye shari zaidi kuliko watenda maasi.” (Majmuu´-ul-Fataawaa (20/103))

[4] Yamesemwa na Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh). Tazama ”Sharh Usuul I´tiqaad Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah” (114) ya al-Laalakaa’iy, ”al-Ibaanah” (161) ya Ibn Battwah, ”as-Sunnah” (30) ya Ibn Naswr na ”as-Swahiyhah” (5/14).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 26-27
  • Imechapishwa: 18/02/2017