05. Ahl-ul-Bid´ah ni khatari zaidi kuliko watenda maasi


Swali 5: Ni nani atayepata adhabu kali – mtenda dhambi au mtu wa Bid´ah?

Jibu: Mtu wa Bid´ah ni mbaya zaidi. Mtu wa Bid´ah ni mbaya zaidi kuliko mtenda dhambi. Mtu wa Bid´ah ni mwenye kupendwa zaidi na Shaytwaan kuliko mtenda dhambi. Mtenda dhambi hutubia wakati mtu wa Bid´ah ni wachache sana wanaotubia[1]. Kwa sababu hufikiria kuwa yuko katika haki tofauti na mtenda maasi ambaye hujua kuwa ni muasi na ni mtenda dhambi. Ama mtu wa Bid´ah yeye huona kuwa ni mtiifu na yumo katika ´ibaadah. Kwa ajili hiyo ndio maana mtu wa Bid´ah akawa ni shari zaidi kuliko mtenda dhambi na kinga inaombwa kwa Allaah. Kwa hivyo ndio maana Salaf walitahadharisha kukaa na watu wa Bid´ah. Wanamuathiri yule mwenye kukaa nao [2] na khatari yao ni kubwa.

Ni jambo lisilokuwa na shaka yoyote kuwa mtu wa Bid´ah ni mwenye shari zaidi kuliko mtenda dhambi. Khatari za mtu wa Bid´ah ni kubwa kuliko za mtenda maasi[3]. Ndio maana Salaf wamesema:

“Ni bora kukomeka na Sunnah kuliko kuwa ni mwenye bidii katika Bid´ah.”

[1] Sufyaan ath-Thawriy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Bid´ah ni zenye kupendwa zaidi kwa Ibliys kuliko maasi. Maasi mtu hutubia kwayo tofauti na Bid´ah.” (Ibn-ul-Jja´d (1885) na Madjmuu´-ul-Fataawaa (11/472))

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika ya Allaah Ameizuia Tawbah ya kila mtu wa Bid´ah.” Swahiyh (1620)

[2] Hasan al-Baswriy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Usikae na mtu wa Bid´ah. Hakika atautia moyo wako maradhi”. (al-I´tiswaam (1/172) na al-Bid´ah wan-Nahiy ´anhaa, uk. 45)

ash-Shaatwibiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hakika Firqat-un-Naajiyah (kundi lililookolewa) – yaani Ahl-us-Sunnah – limeamrishwa kuwachukia Ahl-ul-Bid´ah, wape mfano wa matahadharisho wale wenye kutaka kuwafuata na kuwaadhibu wale wenye kujiunga nao, ima kwa kuuawa au mengineyo. Wanachuoni wametahadharisha kutangamana nao na kukaa nao.” (al-I´tiswaam (1/158))

Allaah Awarahamu Salaf. Hakukuwepo mtu wa Bid´ah isipokuwa walimponda na kutahadharisha naye.

[3] Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema wakati alipokuwa anataja khatari ya Ahl-ul-Bid´ah:

“Lau Allaah Asingelifanya kupatikana watu wenye kuraddi madhara ya watu hawa basi dini ingeliharibika. Madhara haya yangelikuwa makubwa kuliko pindi adui kafiri anapouteka mji. Wanapouteka mji uharibifu wao wa miji unafuatiwa na mioyo na dini yao, ama kuhusu watu wa Bid´ah huanza kuharibu mioyo kwanza.” (Majmuu´-ul-Fataawaa (28/232))

Vilevile amesema (Rahimamu Allaah):

“Kwa mujibu wa Sunnah na maafikiano Ahl-ul-Bid´ah ni wenye shari zaidi kuliko watenda maasi.” (Majmuu´-ul-Fataawaa (20/103))

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Adjwibah al-Mufiydah ´an As'ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 26-27
  • Imechapishwa: 18/02/2017