05. Wanandoa wanatakiwa kuswali Rakaa´ mbili pamoja

3- Mume na mke kuswali pamoja

Imependekezwa wakaswali Rakaa´ mbili pamoja, kwa sababu hilo ni jambo limenukuliwa kutoka kwa Salaf. Vilevile kuna mapokezi mawili:

1- Abu Sa´iyd ambaye aliachwa huru na Abu Asyad amesema:

“Nilioa wakati nilikuwa bado mtumwa. Nikawaalika baadhi ya Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwemo Ibn Mas´uud, Abu Dharr na Hudhayfah. Kukakimiwa kwa ajili ya swalah ambapo Abu Dharr akasogea mbele na wengine wakasema: “Hapana!” Akasema: “Ndivyo?” Wakasema: “Ndio.”[1] Ndipo nikatangulia mbele na kipindi hicho nilikuwa bado ni mtumwa mwenye kumilikiwa. Wakasema: “Atapoingia mke wako, basi swali pamoja naye Rakaa´ mbili kisha muombe Allaah wema aliokuja nao na jilinde Kwake kutokamana na shari yake. Hiyo ni shani yako na shani ya mke wako.”[2]

2- Shaqiyq ameeleza:

“Kuna mtu mmoja alikuja kwa jina Abu Hariyz akasema: “Mimi nimeoa mjakazi bikira na nachelea asije kunichukia.” ´Abdullaah bin Mas´uud akasema: “Hakika muungano unatoka kwa Allaah na mfarakano unatoka kwa shaytwaan ambaye anataka kukufanyeni mkichukie kile alichokuhalalishieni Allaah. Atapokujia basi muamrishe aswali nyuma yako Rakaa´ mbili.”

Ameongeza katika upokezi mwingine kutoka kwa Ibn Mas´uud:

“Kisha sema:

اللهم بارك لي في أهلي وبارك لهم في اللهم اجمع بيننا ما جمعت بخير وفرق بيننا إذا فرقت إلى خير

“Ee Allaah! Nibarikie mke wangu na nibarikie na wabarikie. Ee Allaah! Tuunge pamoja muda wa kuwa tumeungana kwa kheri na tutenganishe muda wa kuwa tutatengana kuielekea kheri.”[3]

[1] Wanachoashiria ni kwamba mgeni hamwongozi mwenyeji nyumbani kwake. Isipokuwa kwa idhini yake. Dalili ya hilo ni maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Haongozwi mtu katika nyumba yake wala katika utawala wake.” (Ameipokea Muslim na Abu ´Awaanah katika “as-Swahiyh” zao. Inapatikana vilevile katika “Swahiyh Abiy Daawuud”, nambari. 594.

[2] Ameipokea Abu Bakr bin Abiy Shaybah katika “al-Muswannaf” (07/50).

[3] Ameipokea Abu Bakr bin Abiy Shaybah katika marejeo yaliyotangulia na vilevile kaipokea ´Abdur-Razzaaq katika “al-Muswannaf” (10461). Mlolongo wa wapokezi wake ni Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Aadaab-uz-Zafaaf, uk. 94-96
  • Imechapishwa: 23/02/2018