04. Uwajibu wa swawm


Ndugu mpendwa! Hapa chini kunafuata baadhi ya hukumu muhimu kwa mfungaji:

1- Kila mwanaume na mwanamke muislamu ambaye ana jukumu juu ya matendo yake ni wajibu kwake kufunga Ramadhaan. Imependekezwa kwa mtoto aliye na miaka saba au zaidi kufunga iwapo ataweza kufanya hivo. Katika hali hii ni wajibu kwa walezi wao kuwaamrisha kama ambavyo wanawaamrisha kuswali. Msingi wa hili ni maneno Yake (´Azza wa Jall):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ ۚ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۚ وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ ۖ فَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ ۚ وَأَن تَصُومُوا خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa kufunga kama ilivyofaradhishwa kwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Allaah. [Kufunga ni] siku za kuhesabika. Yule atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu au safarini, basi akamilishe idadi [ya siku zilizompita] katika siku nyinginezo na kwa wale wanaoiweza lakini kwa tabu watoe fidia kulisha masikini. Na atakayejitolea kwa jema lolote lile basi ni bora kwake. Na mkifunga ni bora kwenu – mkiwa mnajua [namna ilivyo kheri kwenu]! Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo la batili. Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi mpya na afunge . Atakayekuwa mgonjwa au safarini basi atimize idadi katika siku nyinginezo.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Uislamu umejengwa juu ya vitano; kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kwenda kuhiji Nyumba.”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

2- Asli ni wajibu kufunga Ramadhaan na kuweka nia ya kufunga kabla ya kupambazuka. Hili ni kwa waislamu wote ambao wana jukumu juu ya matendo yao. Wanatakiwa kuamka hali ya kuwa wamefunga. Isipokuwa wale waliopewa ruhusa na Allaah ya kuacha kufunga. Miongoni mwao ni wagonjwa, wasafiri na wale walio na hukumu yao.

Ambaye atafikiwa na khabari ya kuingia kwa mwezi wa Ramadhaan baada ya kupambazuka ni wajibu kwake kujizuia na yale yote yanayokata swawm siku iliyobaki. Kwa sababu ni siku ya Ramadhaan ambayo haijuzu kwa mwenye afya aliye katika mji wake kufanya kitu kinachokata swawm. Vilevile ni juu yake kufunga siku hiyo kwa sababu hakunuia swawm kabla ya kuingia alfajiri. Imethibiti kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule asiyenuia swawm kabla ya alfajiri hana swawm.”[3]

Ameipokea ad-Daaraqutwniy kupitia kwa ´Amrah kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesema:

“Wote walio kwenye mnyororo wa wapokezi ni waaminifu.”

Muwaffiq-ud-Diyn bin Qudaamah ameitaja katika “al-Mughniy” na ndio maoni ya wanachuoni wengi. Swawm inayokusudiwa hapo ni ya faradhi. Kuhusu iliyopendekezwa inafaa kuianza wakati wa mchana ikiwa mtu hakufanya kitu kinachokata swawm baada ya alfajiri. Kumesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yanayofahamisha hivo.

3- Ni wajibu kwa muislamu kufunga kwa imani na kwa kutaraji malipo. Asifunge kwa kutaka kuonekana na kusikika. Asifunge kwa kuwafuata kichwa mchunga wengine wala kwa kufuata desturi. Bali ni wajibu afunge kwa kumuamini Allaah na kwa kutaraji malipo juu ya hilo.

Hali kadhalika inahusiana na kisimamo cha usiku katika Ramadhaan. Ni wajibu kwa muislamu afanye hivo kwa imani na kwa kutaraji malipo kutoka kwa Allaah. Asiwe na malengo mengine. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atayefunga Ramadhaan kwa imani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia. Atayesimama [nyusiku za] Ramadhaan kwa imani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia. Atayesimama usiku wa Qadar kwa imani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”[4]

Ee waja wa Allaah! Mcheni Allaah na yaadhimisheni maamrisho na makatazo Yake. Kimbilieni kutubia kwa madhambi yote. Mtegemeeni. Hakika Yeye ndiye Muumba wa viumbe na Mwenye kuwaruzuku. Yeye ndiye Mwenye kuwamiliki. Hakuna kiumbe yeyote anayemiliki juu ya nafsi yake madhara, manufaa, mauti, uhai wala kufufuliwa. Ipeni kipaumbele – Allaah akurehemuni – haki ya Mola Wenu na ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kabla ya wengine wote pasi na kujali ni nani. Amrisheni mema na katazeni maovu. Mdhanieni Allaah vyema. Kithirisheni kumdhukuru na mtakeni msamaha. Saidianeni juu ya wema na kumcha Allaah. Wazuieni watenda madhambi wenu kufanya madhambi. Walazimisheni yale waliyolazimishwa na Allaah na wakatazeni yale waliyokatazwa na Allaah. Pendeni kwa ajili ya Allaah. Chukieni kwa ajili ya Allaah. Wapendeni mawalii wa Allaah. Wachukieni maadui wa Allaah. Subirini na vumilieni mpaka pale mtapokutana na Mola Wenu ili muweze kufuzu furaha iliokubwa, karama, utukufu na ngazi za juu Peponi.

Tunamuomba Allaah atuongoze sisi na nyinyi kwa yale anayoyaridhia, azitengeneze nyoyo za watu wote na azijaze kumwogopa, kumpenda, kumcha Yeye na kupendea kheri kwa ajili Yake na kwa ajili ya waja Wake.

[1] 02:183-185

[2] al-Bukhaariy (8) na Muslim (16).

[3] at-Tirmidhiy (730), ad-Daaraqutwniy (2/171) na al-Bayhaqiy katika ”as-Sunan al-Kubraa” (7701). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (6534).

[4] al-Bukhaariy (1901) na (2014) bila ya ”Atayesimama [nyusiku za] Ramadhaan…” na vilevile Muslim (670). Hadiyth imepokelewa kikamilifu na at-Tirmidhiy (683) na Ahmad (10159).