04. Uchambuzi wa baadhi ya mifano iliyopigwa

Kutokana na yale yaliyotangulia inapata kutubainikia umuhimu wa Sunnah katika uwekaji Shari´ah wa Kiislamu. Tukirudisha jicho katika ile mifano tuliyotaja, seuze mifano mingine ambayo hatukuitaja, basi tutakubali ya kwamba hakuna njia nyingine ya kuifahamu Qur-aan tukufu isipokuwa kwa kuiambatanisha na Sunnah.

Katika ule mfano wa kwanza Maswahabah walielewa neno dhuluma katika Aayah juu ya udhahiri wake pamoja na kuwa wao (Radhiya Allaahu ´anhum) walikuwa, kama alivyosema Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh):

“Wabora wa Ummah huu ambao walikuwa na mioyo miema, elimu ya kina na wachache wa kujikakama.”

pamoja na kuwa hivyo walikosea katika uelewa huo. Iwapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) asingewarekebisha kosa lao na akawaelekeza katika usawa kuhusu ´dhuluma` iliyokusudiwa ni shirki, basi tungeliwafuata katika kosa lao hilo. Lakini hata hivyo Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) akaepusha hilo kwa fadhila za maelekezo yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Sunna zake.

Tunapokuja katika ule mfano wa pili kusingelikuwa Hadiyth iliyotajwa basi angalau kwa uchache tungelibaki hali ya kuwa ni wenye mashaka kuhusu kufupisha swalah safarini katika hali ya kuwa na amani tusingeonelea ushurutishaji wa kupatikana khofu ndani yake. Hivyo ndivyo ulivyo udhahiri wa Aayah na hivyo ndivyo walivyokimbilia kuelewa baadhi ya Maswahabah endapo wasingelimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anafupisha na hivyo na wao wakafupisha pamoja naye. Kwa hali hiyo kukapatikana kuondokwa na wasiwasi.

Kuhusu mfano wa tatu kusingelipatikana Hadiyth, basi tungeliharamisha vilivyo vizuri tulivyohalalishiwa nzige, samaki, ini na wengu.

Tunapokuja katika mfano wa nne kama isingelikuwa Hadiyth ambazo tumezitaja baadhi yake tungehalalisha vile Allaah alivyotuharamishia kupitia Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika wanyama mwitu wenye kutia meno na kila ndege wenye kutumia makucha.

Vivyo hivyo kuhusu mfano wa tano kama isingelikuwa Hadiyth, basi tungelihalalisha dhahabu na hariri ambavyo vimeharamishwa na Allaah kupitia Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuanzia hapa wamesema baadhi ya Salaf:

“Sunnah inaihukumu Qur-aan.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manzilat-us-Sunnah fiyl-Islaam, uk. 10-12
  • Imechapishwa: 10/02/2017