04. Ubainifu wa kumshirikisha Allaah na sampuli zake


Kama ambavo Allaah amebainisha na kudhihirisha kitendo cha kumtakasia dini vivyo hivyo amebainisha kinyume chake ambacho ni shirki. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

 “Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[1]

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe Yeye na chochote.”[2]

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

”Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut [waungu batili].”[3]

Zipo Aayah  nyingi juu ya hilo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote mwenye kukutana na Allaah pasi na kumshirikisha na chochote ataingia Peponi. Yeyote mwenye kukutana na Allaah hali ya kumshirikisha na chochote ataingia Motoni.”[4]

Ameipokea Muslim kupitia kwa Jaabir.

Shirki imegawanyika sampuli mbili:

1 – Shirki kubwa inayomtoa mtu nje ya dini. Kila shirki iliyotajwa na Shari´ah kwa njia ya kuachia na wakati huohuo ikawa ni yenye kukinzana na Tawhiyd makinzano ya moja kwa moja. Mfano wake ni kama mtu kumtekelezea aina moja wapo ya ´ibaadah kumfanyia asiyekuwa Allaah. Kwa mfano akaswali kwa ajili ya mwingine asiyekuwa Allaah, akachinja kwa ajili ya mwingine asiyekuwa Allaah, akamuwekea nadhiri mwingine asiyekuwa Allaah, akamwomba asiyekuwa Allaah kama mfano akamwomba aliyemo ndani ya kaburi na akamwomba asiyekuweko mbele yake amwokoe kutokamana na jambo asiloliweza mwingine isipokuwa aliyeko mbele yake. Aina zake ni zenye kutambulika kutokamana na yale yaliyoandikwa na wanachuoni.

2 – Shirki ndogo. Ni kila kitendo cha kimatamshi au kimatendo kilichotajwa na Shari´ah kwa njia ya kuachia na kueleza kuwa ni shirki lakini hata hivyo hakipingani na Tawhiyd mapingano ya moja kwa moja. Mfano wa hilo ni kuapa kwa jina la mwingine asiyekuwa Allaah. Yule mwenye kuapa kwa jina la mwingine asiyekuwa Allaah na wakati huohuo si mwenye kuamini kwamba huyo mwingine asiyekuwa Allaah hana utukufu unaolingana na utufuku wa Allaah. Mtu kama huyu ni mwenye kushirikisha shirki ndogo.

Mfano mwingine ni kujionyesha, jambo ambalo ni khatari. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yake:

“Kikubwa ninachokikhofia kwenu ni shirki ndogo. Alipoulizwa juu yake akasema: “Ni kujionyesha.”[5]

Kujionyesha kunaweza kupelekea katika shirki kubwa. Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amepigia mfano shirki ndogo kwa ujionyesha mdogo, jambo ambalo linajulisha kuwa ujionyeshaji mwingi unaweza kupelekea katika shirki kubwa.

[1] 04:116

[2] 04:36

[3] 16:36

[4] al-Bukhaariy (129) na Muslim (93).

[5] Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) katika ”as-Silsilah as-Swahiyhah” (951).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 09-10
  • Imechapishwa: 16/06/2021