04. Tuache Qur-aan na Sunnah viamue


Lipo jopo la wanazuoni waliokemea kwa uwazi kabisa mazazi na wakayatahadharisha. Wamefanya hivo kwa ajili ya kutendea kazi dalili zilizotajwa na nyenginezo. Baadhi ya wengine waliokuja nyuma wakaonelea kinyume ambapo wakayajuzisha pale ambapo yatakuwa hayana chochote katika maovu kama mfano wa kuchupa mpaka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kuchanganyika wanawake na wanamme, kusikiliza nyenzo za pumbao na mengineyo yanayopingana na Shari´ah takasifu. Walidhania kwamba ni miongon mwa Bid´ah nzuri. Kanuni ya ki-Shari´ah inasema:

“Yale ambayo watu wametofautiana kwayo yanarudishwa katika Qur-aan na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Hivo ni kama alivosema Allaah (´Azza wa Jall):

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

“Mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[1]

وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِن شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّـهِ

“Jambo lolote lile mlilokhitilafiana ndani yake, basi hukumu yake ni kwa Allaah.”[2]

Tumerudisha jambo hili la kusherehekea mazazi ya Mtume katika Qur-aan na tumeona kuwa inatuamrisha kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika yale aliyokuja nayo na sambamba na hilo inatutahadharisha na yale aliyotukataza. Aidha inatueleza kwamba Allaah (Subhaanah) ameukamilishia Ummah huu dini yake. Usherehekea huu sio katika yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hivyo sio katika dini ambayo Allaah ametukamilishia na akatuamrisha kumfuata Mtume katika dini hiyo. Vilevile tumeyarudisha hayo katika Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hatukuona humo kuwa ameyafanya, ameyaamrisha, kufanywa na Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum). Hivyo ikatambulika kuwa sio katika dini. Bali ni miongoni mwa Bid´ah zilizozuliwa. Aidha ni kujifananisha na watu wa Kitabu miongoni mwa mayahudi na manaswara katika sikukuu zao.

[1] 04:59

[2] 42:10

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr minal-Bid´ah, uk. 9-10
  • Imechapishwa: 12/01/2022