Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Unapojua kuwa shirki inapoingia katika ´ibaadah inaiharibu na kubatilisha kitendo hicho na mwenye nayo anakuwa ni katika wataodumishwa Motoni milele, ndipo utaona kuwa suala hili ni muhimu sana kwa ulazima kulitambua. Huenda Allaah akakusalimisha na mtego huu, jambo ambalo ni kumshirikisha Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema juu yake:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakikaha hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa Amtakae.” (04:116)

Hili litatambulika kwa kuijua misingi mitatu ambayo Allaah (Ta´ala) ameitaja katika Kitabu Chake:

MAELEZO

Midhali umejua ni nini Tawhiyd, nayo ni kumpwekesha Allaah katika ´ibaadah, basi ni lazima vilevile ujue shirki ni kitu gani. Kwa kuwa yule asiyekitambua kitu hutumbukia ndani yake. Ni lazima ujue aina mbalimbali za shirki ili uweze kuziepuka, kwa sababu Allaah ametahadharisha shirki na kusema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa Amtakae.” (04:48)

Hii ndio khatari ya shirki ambayo inaharamisha Pepo:

إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ

“Hakika mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah atamharamishia Pepo.” (05:72)

Vilevile inaharamisha kupata msamaha:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa Amtakae.”

Hii ni khatari iliokubwa. Ni lazima uitambue kabla ya kila kitu kingine. Watu wengi wenye fahamu na akili wamepotea juu ya suala hili la shirki. Hebu wacha tujue shirki ni kitu gani kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah. Allaah hakutahadharisha kitu isipokuwa amekibainisha na kadhalika hakuamrisha kitu isipokuwa amewabainishia nacho watu. Hakuharamisha shirki na kuiacha hivo kijumlajumla. Uhakika wa mambo ni kuwa ameibainisha katika Qur-aan tukufu na vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameibainisha katika Sunnah kwa njia ya wazi kabisa. Hivyo tukitaka kujua shirki ni kitu gani, basi ni lazima turejee kwenye Qur-aan na Sunnah na sio katika maoni ya huyu na yule.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 16-17
  • Imechapishwa: 18/08/2022