04. Qur-aan imeizungumza Tawhiyd na shirki wazi kabisa

Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimhu Allaah) amesema:

Sehemu kubwa ya Qur-aan imebainisha msingi huu kwa njia mbalimbali kwa maneno ambayo anayafahamu zaidi mpumbavu zaidi katika wale wasiokuwa wasomi.

MAELEZO

Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote.” (04:36)

Je, haya ni maneno yaliyofichikana? Wajinga wasiokuwa na elimu wanayafahamu.

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote.”

Wanafahamu kwa maneno haya maamrisho ya ´ibaadah na makatazo ya shirki. Wanayafahamu kwa lugha zao hata kama hawajasoma. Wanayafahamu kwa lugha zao. Hii ni Aayah moja ingawa Qur-aan imejaa Aayah mfano wa hizi. Aayah kama hizi wanazipitia na kuzisoma lakini hata hivyo hawazizingatii. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote.”

Pamoja na hivyo wanasema “Ee ´Aliy!”, “Ee Husayn!”, “Ee Badawiy!”, “Ee Tijaaniy!”, “Ee ´Abdul-Qaadir [al-Jaylaaniy]!”. Wanawapigia makelele na kuwaita kwa sauti za juu “Ee fulani!”, “Ee fulani!”, ilihali wameshakufa. Huyu ambaye anawaita na kuwapigia makelele waliokufa pengine amehifadhi Qur-aan kwa visomo vyake saba au kumi na anaisoma vizuri kabisa kwa Tajwiyd. Anaipa haki yake inavotakikana kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ametilia umuhimu katika herufi zake na wakati huo huo ni mwenye kupoteza mipaka yake.

Imaam Ibn-ul-Qayyim amesema kuwa Qur-aan yote imezungumzia Tawhiyd; ima ndani yake kuna maamrisho ya kumuabudu Allaah na kuacha shirki, malipo ya watu wa Tawhiyd na malipo ya watu wa shirki, hukumu za halali na haramu ambayo ndio haki ya Tawhiyd au visa vya Mitume na nyumati zao na magomvi yaliyopitika kati yao ambayo ni malipo ya Tawhiyd na shirki. Kwa hivyo Qur-aan yote imezungumzia Tawhiyd kuanzia mwanzo wake mpaka mwisho wake. Pamoja na kuwa wanasoma Qur-aan hii lakini bado wamo katika shirki kubwa. Wakati huohuo wanasema “Hapana mungu mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah” lakini hawaifanyii kazi. Wako upande huu na Qur-aan na Shahaadah viko upande mwingine. Wao wanachojali ni kutamka kwa ndimi zao tu.

Ukimuuliza mmoja wao ni nini maana ya “Hapana mungu mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah”? Jibu atakwambia hajui na hajajifunza! Tunamuuliza kwa kumwambia ni vipi utasema “Hapana mungu mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah” ilihali hujui maana yake? Namna hii anapasa muislamu kuwa? Unasema maneno ambayo hujui maana yake na wala huyatilii umuhimu! Au unataka kusema kuwa umewasikia watu wanasema kitu na wewe ukakisema! Namna hii ndivyo watavyosema wanafiki ndani ya makaburi pindi watapoulizwa. Watasema:

“Niliwasikia watu wakisema kitu na mimi nikakisema.”

Kama alivyosema (Ta´ala):

وَمَثَلُ الَّذِينَ كَفَرُوا كَمَثَلِ الَّذِي يَنْعِقُ بِمَا لَا يَسْمَعُ إِلَّا دُعَاءً وَنِدَاءً ۚ صُمٌّ بُكْمٌ عُمْيٌ فَهُمْ لَا يَعْقِلُونَ

“Na mfano wa wale waliokufuru ni kama mfano wa yule ambaye anapiga kelele kwa asiyesikia ila wito na kelele tu [za wanyama anaowachunga]; viziwi, mabubu, vipofu kwa hiyo hawaelewi!” (02:171)

Allaah amewafananisha na wanyama ambao wanasikia sauti ya mchungaji na mfanya kazi na anatembea kwa mujibu wa sauti ya mchungaji lakini hata hivyo haelewi maana yake.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 13-14
  • Imechapishwa: 18/05/2021