04. Ni kwanini viongozi wa al-Qaa´idah na wao wasijitoe muhanga?

Mabalaa yaliyotajwa yanatokamana na kwamba Shaytwaan amewapambia na wafuasi wao wapumbavu uharibifu na ufisadi na kuwafanya wakawa ni wenye kuchukia matendo mema na utengenezaji. Ndio maana shari yao ni kubwa mno wakati mema yao ni machache. Wanasema kuwa kujitoa muhanga ni shahada na wanapuuzia Kauli ya Allaah:

وَلَا تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ

“Msijiue.” (04:29)

Wanapuuzia yale aliyopokea al-Bukhaariy kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema:

“Kuna mtu aliyekuwa akiishi kabla yenu ambaye aliumia. Akachukua kisu na kujikata mkono wake. Akatokwa na damu mpaka akafa. Hivyo Allaah (´Azza wa Jalla) Akasema: “Mja wangu ameiharakisha nafsi yake. Nimemharamishia Pepo.”[1]

Wanapuuzia yale al-Bukhaariy na Muslim waliyopokea kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Yeyote atakayejiua kwa chuma, atabeba chuma chake mkononi mwake na huku anajichoma mwenyewe kwenye tumbo Motoni ambako atadumishwa humo milele. Yeyote atakayejiua kwa sumu, atabeba sumu yake mkononi mwake huku anainywa Motoni ambako atadumishwa humo milele. Yeyote atakayejitupa kutoka kwenye mlima na akafa, atatupwa kwenye Moto wa Jahannam na humo atadumishwa milele.”[2]

Kwenye maandiko haya kuna matishio makali kabisa kwa yule mwenye kujiua au kumuua mtu mwingine ambaye ni haramu kufanya hivo. Shari´ah imemkataza kila yule ambaye matendo yanamuwajibikia [mkalifishwaji], wanaume kwa wanawake, kuiua nafsi yake. Kwa kuwa sio wao wenye kuzimiliki. Zinamilikiwa na Allaah. Yeye ndiye ambaye Ameamrisha kuzitakasa na kuziheshimisha kwa matendo mema ili mtu aweze kulipwa mema siku ya Qiyaamah. Hali kadhalika, kama tulivyosema, amekataza kujiua.

Nyinyi mnaolingania katika kujitoa muhanga na mnaita hayo kuwa ni shahada katika njia ya Allaah! Inakuweje tena kwa nyinyi wenyewe kutofanya hayo matendo machafu ambayo mmewaamrisha wapumbavu kufanya? Inakuweje nyinyi wenyewe hamko radhi kuwa mfano mzuri na kuwa msitari wa mbele kwa yale mnayowalingania watu kwayo? Ni kwa vile mmekata shauri kwa yule mwenye kufanya matendo hayo anapata shahada na mwenye kuyatenda anapata daraja ya shahidi. Ni ubaya ulioje mnavyohukumu! Ni kwa nini mmeigeuzia haki ya wazi mgongo kwa kueneza ufisadi ulio mbaya katika ardhi na kudai kwamba nyinyi ni watengenezaji?

[1] al-Bukhaariy (3276).

[2] al-Bukhaariy (5442) na Muslim (109).

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Waqafaat wa Ma´aalim, uk. 10-12
  • Imechapishwa: 02/12/2014