04. Mtume alikuwa ni mtu wa kawaida

1- Allaah (Ta´ala):

قُلْ إِنَّمَا أَنَا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُوحَى إِلَيَّ أَنَّمَا إِلَهُكُمْ إِلَهٌ وَاحِدٌ فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاء رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا

”Sema: “Hakika mimi ni mtu [wa kawaida] kama nyinyi. Nafunuliwa Wahy kwamba hakika mwabudiwa wenu wa haki ni Mungu mmoja pekee. Hivyo yule anayetaraji kukutana na Mola wake basi na atende matendo mema na wala asimshirikishe katika ‘ibaadah za Mola wake yeyote!”

Allaah amemwamrisha Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwaambia watu:

قُلْ إِنَّمَا أَنَا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ

”Sema: “Hakika mimi ni mtu [wa kawaida] kama nyinyi.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ni mtu. Mitume wote walikuwa ni watu. Kuna aina mbili za wajumbe:

1- Malaika.

2- Watu.

Allaah (Ta´ala) amesema:

اللَّـهُ يَصْطَفِي مِنَ الْمَلَائِكَةِ رُسُلًا وَمِنَ النَّاسِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ بَصِيرٌ

“Allaah anateua wajumbe miongoni mwa Malaika na miongoni mwa watu. Hakika Allaah ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

Wajumbe wa ki-Malaika wanakuwa ni wakati na kati baina ya Allaah na wajumbe wa ki-watu. Mtu hawezi kuwaona Malaika katika umbile lao la kihakika. Anaweza tu kumuona mtu mwenzake. Kwa aj0ili hii ndio maana Allaah akamtumia mtu wajumbe wa ki-watu, kwa sababu hiyo inapelekea huruma Wake juu ya waja Wake, wawaelewe, wajifunze kutoka kwao na wajihisi vizuri nao. Lau wangelikuwa ni Malaika wasingeliweza kuwaona. Kwa sababu umbile la Malaika linatofautiana na umbile la mtu.

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

أَنَا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ

“Hakika mimi ni mtu [wa kawaida] kama nyinyi.”

Bi maana sina sifa yoyote ile ya kiuola wala ya kiuungu. Ni mja tu miongoni mwa waja wa Allaah. Hapa kuna Radd dhidi ya wale wanaochupa mipaka juu ya haki ya Mtume (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam), wanamuomba, wanamtaka msaada badala ya Allaah na wanasema kwamba ameumba kutokana na nuru au kwa kitu kingine kinachotofautiana na maumbile ya wanadamu wengine na kwamba ameumbwa kabla ya Aadam. Yote haya ni miongoni mwa aina kubwa kabisa ya kuchupa mipaka na kumkufuru Allaah (´Azza wa Jall). Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kama watu wengine wote. Anapatwa na njaa, anagonjweka na anachoka safarini. Kwa msemo mwingine yeye ni kama watu wengine wote. Anapatwa na yale yote yanayowafika watu wengine. Vilevile anapatwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hamu na huzuni:

قَدْ نَعْلَمُ إِنَّهُ لَيَحْزُنُكَ الَّذِي يَقُولُونَ ۖ فَإِنَّهُمْ لَا يُكَذِّبُونَكَ وَلَـٰكِنَّ الظَّالِمِينَ بِآيَاتِ اللَّـهِ يَجْحَدُونَ

“Hakika tunajua kwamba yanakuhuzunisha yale wanayoyasema. Hakika wao hawakukadhibishi wewe lakini madhalimu wanakanusha alama za Allaah.”[2]

وَلَا تَحْزَنْ عَلَيْهِمْ

”… na wala usihuzunike juu yao… ”[3]

فَلَعَلَّكَ بَاخِعٌ نَّفْسَكَ عَلَىٰ آثَارِهِمْ إِن لَّمْ يُؤْمِنُوا بِهَـٰذَا الْحَدِيثِ أَسَفًا

”Basi huenda ukaiangamiza nafsi yako kwa ajili yao kusikitika kutokuamini kwao usimulizi huu.”[4]

Hakika yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapatwa na wasiwasi na huzuni pale anapowaona watu wanamuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwa sababu anawatakia watu kheri na kufaulu. Kwa sababu ya ukamilifu wa kujali kwake anahuzunika pindi anapowaona wanajisababishia wao wenyewe maangamivu. Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametofautiana na watu wengine kwa ujumbe, fadhilah na ukamilifu wa ´ibaadah. Yeye ndiye kiumbe mkamilifu anayeabudu, anayemuogopa na kumcha Allaah zaidi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] 22:75

[2] 06:33

[3] 15:88

[4] 18:06

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 441-442
  • Imechapishwa: 26/08/2019