04. Mke mwema uhusiano wake na Shetani


Sifa nyingine ambayo mke mwema anapaswa kuwa nayo ni kwamba atahadhari na Shetani aliyefukuzwa. Kazi ya Shetani katika maisha haya ni kuharibu. Anaharibu dini, tabia, matangamano, mshikamano, udugu na kila kilicho na kheri. Kila siku anatuma wajumbe na wanajeshi kutekeleza kazi hii. Zingatia Hatiyth hii katika “as-Swahiyh” ya Muslim iliyopokelewa na Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Iblisi hukiweka kiti chake juu ya maji. Kisha anatuma vikosi vyake. Yule mwenye nafasi ya karibu zaidi kwake ni yule mwenye fitina kubwa. Pindi mmoja wao anapomjia anamuuliza aliyofanya. Wakati anaposema aliyofanya, anamwambia: “Hujafanya lolote.” Wakati mwingine anapomjia na kusema: “Sikumuacha mpaka nimehakikisha nimemfarikisha yeye na mke wake” hivyo anamchukua na kumwambia: “Wewe ni mzuri ulioje!”[1]

Anawatuma wanajeshi na wajumbe ili waende kuharibu. Anayekuwa karibu zaidi na yeye ni yule ambaye anasababisha matatizo makubwa kati ya watu. al-A´mash amesema kwamba Shetani anamkumbatia na kujichukulia wanajeshi wanaofarikisha kati mwanamke na mume wake.

Mwanamke mwema anatakiwa kufahamu na kuelewa uhakika huu. Hali kadhalika mume. Wote wawili wanapaswa kufahamu kwamba kuna adui aliyejificha. Anakuona, lakini wewe huwezi kumuona. Anapita ndani ya mwili wako kama damu inavyopita kwenye mishipa. Anapuliza na kutia wasiwasi. Anapanga hila na njama. Anafanya yote hayo bila ya wewe kumuona. Anauzungumzisha moyo wako wewe mume na moyo wako wewe mke. Anakuja na wasiwasi unaopelekea katika uadui. Ana njia nyingi za ufanyaji kazi wake.

Kwa ajili hii imekuja katika Sunnah jinsi ya mtu atakavyojikinga kutokamana na Shetani wakati mtu anapoingia nyumbani kwake, wakati wa jimaa, wakati wa chakula, wakati anapokuwa na hasira na mambo mengine yote ambayo mtu anahitajia kujikinga kutokamana na Shetani ili Shetani asiweze kuwa na ushirikiano wowote na watu wa nyumbani kwake, nyumba yake na watoto wake. Hivyo anahitajia mtu kuikinga nafsi yake na Adhkaar zilizobarikiwa, Qur-aan Tukufu,  du´aa zilizopokelewa na kuhifadhi utiifu kwa ´ibaadah za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Mke mwema anapaswa kujihadhari na vitimbi vya Shetani na wasiwasi wake autiao katika nasfi na ambao unaharibu uhusiano na maisha ya ndoa.

Ni familia ngapi na nyumba ambazo zimefarakana daima kwa sababu tu ya kumtii Shetani na kufuata wasiwasi wa Shetani? Lau kila mmoja angeliomba kinga kwa Allaah kutokamana na Shetani aliyefukuzwa na kujiweka na kujitenga mbali na uchochezi wake na wasiwasi wake kusingelitokea mambo hayo na mfarakano huo.

Ni nyumba ngapi kumetokea mfarakano kwa sababu ya kumtii Shetani? Kisha baadaye huyu muharibifu – askari wa Shetani – anaenda kwa Iblisi ili aweze kupata nafasi ya karibu zaidi na yeye pindi atakapomuhadithia alivyofarikisha kati ya mume na mke.

Kuna kitu cha manufaa ambacho kinatakiwa kuzingatiwa. Huyu adui aliyejificha ambaye anakuona na wewe humuoni ni kiumbe aliye na uzoefu mkubwa. Leo wakati kunapozungumziwa baadhi ya waajiriwa wa kampuni na uzoefu wao mara nyingi huwa ni uzoefu wa miaka khamsini au sitini. Lakini uzoefu wa Iblisi wa kupotosha, kuzuia watu na njia ya Allaah na kueneza uadui kati ya watu? Ni uzoefu wa maelfu ya miaka. Ni watu wangapi wamekufa na kuzikwa baada ya kuwa ni wafungwa wa Shetani na kutumbukia katika uharibifu na upotoshaji wake?  Kwa ajili hii ndio maana ni lazima nyumba ya muislamu ajikinge yeye mwenyewe na kuiweka nafsi yake mbali kutokamana na Shetani aliyefukuzwa.

[1] Muslim (2813).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifaat-uz-Zawjah as-Swaalihah, uk. 19-23
  • Imechapishwa: 17/06/2017