04. Mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah katika majina na sifa za Allaah

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni wale walio na umoja katika kushikamana na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuzitendea kazi kwa maneno, matendo na I´tiqaad kwa dhahiri na kwa ndani.

´Aqiydah yao katika majina na sifa za Allaah ni kama ifuatavyo:

Mosi: Katika kuthibitisha. ´Aqiydah yao ni kuthibitisha yale Allaah aliyojithibitishia Mwenyewe katika Qur-aan au yale ambayo Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemthibitishia. Uthibitishaji huu unatakiwa uwe bila ya upotoshaji, ukanushaji, kufanya namna wala ufananishaji.

Pili: Katika kukanusha. Wanakanusha yale Allaah na Mtume Wake waliyokanusha. Sambamba na hilo wanaamini kuwa Allaah (Ta´ala) anasifika kwa ukamilifu wa kinyume chake.

Tatu: Istilahi ambazo hakukuthibiti uthibitishwaji wala ukanushwaji wake na ambayo watu wametofautiana kwayo kama mfano wa kiwiliwili, kiasi, upande na mfano wa hayo. Matamshi ya istilahi kama hizi, hawazithibitishi na wala hawazikanushi kwa vile hazikutajwa [katika Qur-aan wala Sunnah]. Ama kuhusu maana zake, mtu anatakiwa kupambanua. Ikiwa maana yake ni batili, Allaah anatakaswa nayo. Ikiwa maana yake ni haki na yenye kuendana na Allaah, wanaikubali.

Huu ndio mwenendo wa wajibu. Ndio ambao uko kati kwa kati baina ya wale wenye kukanusha na wale wenye kufananisha. Mwenendo huu unathibitishwa na akili na Wahy.

Akili: Yale ambayo ni wajibu kwa Allaah (Ta´ala), inafaa na haifai kusifika nayo hilo linaweza kufahamika kwa Wahy peke yake. Kwa hivyo ni wajibu kufuata Wahy na kuthibitisha yale inayothibitisha na kukanusha yale inayokanusha na kunyamazia yale inayonyamazia.

Wahy: Miongoni mwa dalili zake ni maneno Yake (Ta´ala):

وَلِلَّهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَى فَادْعُوهُ بِهَا وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Allaah ana majina mazuri kabisa, basi muombeni kwayo na waacheni wale wanaopotoa katika majina Yake, watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda.”[1]

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[2]

وَلا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ

“Wala usiyafuate yale usiyokuwa nayo elimu.”[3]

Aayah ya kwanza inatoa dalili ya uwajibu wa kuthibitisha pasi na upotoshaji wala ukanushaji, kwani yote mawili ni kupotoa.

Aayah ya pili inatoa dalili ya uwajibu wa kukanusha ufananishaji.

Aayah ya tatu inatoa dalili ya uwajibu wa kukanusha ufanyaji namna na kukomeka na yale ambayo hayakuthibitishwa wala hayakukanushwa.

Sifa zote zilizothibiti kwa Allaah ni kamilifu. Anasifiwa na kutapwa kwazo. Hazina mapungufu kwa njia yoyote ile. Sifa kamilifu zote za Allaah ni kamilifu kwa njia zote.

Yale yote ambayo Allaah amejikanushia, ni sifa zenye mapungufu. Zinapingana na uwajibu wa ukamilifu Wake. Kwa vile sifa Zake kamilifu ni za wajibu, ni jambo lisilowezekana akajisifia kwa sifa pungufu. Maana ya zile sifa ambazo Allaah amekanusha, ni kwamba hazipo na wakati huohuo mtu anathibitisha ukamilifu wa kinyume chake. Ukanushaji hautoi dalili kuonyesha ukamilifu wowote midhali hauna sifa iliyothibiti anayosifika kwayo. Ukanushaji peke yake unaweza kuwa ni wenye kutokamana na kutokuweza, jambo ambalo ni kasoro. Kama ilivyo katika maneno ya mshairi:

“Kijikabila hakisaliti ahadi na wala hakiwadhulumu watu chembe kidogo kabisa ya hardali.”

Kadhalika sababu inaweza kuwa kukosekana uwezo, jambo ambalo halipelekei katika sifa. Mfano wa hilo ni kama useme:

“Ukuta haudhulumu.”

Yakibainika haya, tunasema ya kwamba dhuluma ni sifa ambayo Allaah amejikanushia. Katika hali hii ina maana ya kwamba Allaah hasifiki kudhulumu na wakati huohuo tunamthibitishia ukamilifu wa kinyume chake, ambao ni uadilifu. Vilevile Amejikanushia kutaabika. Ina maana ya kwamba hasifiki kutaabika na wakati huohuo tunamthibitishia ukamilifu wa kinyume chake, ambao ni nguvu. Vivyo hivyo kuhusiana na sifa nyenginezo ambazo Allaah amejikanushia – na Allaah ndiye anajua zaidi.

Upotoshaji (Tahriyf): Maana yake ya kilugha ni “ugeuzaji”. Maana yake ya kidini ni “kugeuza andiko kimatamshi au kimaana”. Kunapogeuzwa andiko kimatamshi, kuna uwezekano vilevile maana ikabadilika au isibadilike. Upotoshaji unagawanyika mafungu matatu:

La kwanza: Matamshi na maana vyote viwili vinabadilika. Mfano wa hilo ni pale baadhi yao wanapopotosha maneno ya Allaah:

وَكَلَّمَ اللَّهُ مُوسَى تَكْلِيماً

”Allaah alimsemesha Muusa maneno ya kihakika.”[4]

Wanajaribu ionekane kuwa Muusa ndiye alimsemesha Allaah (Allaaha) na sio kinyume chake.

La pili: Upotoshaji wa matamshi usiyobadilisha maana. Mfano wa hilo ni mtu kusoma:

الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

“Sifa njema na shukurani zote njema (al-Hamdu) ni za Allaah, Mola wa walimwengu.”[5]

akasoma “al-Hamda”. Hili mara nyingi hutokea kwa mjinga asiyefanya hivo kwa kusudio lolote.

La tatu: Maana ikabadilishwa. Kuyageuza matamshi kuyatoa nje ya udhahiri wake pasi na dalili. Kwa mfano kupotosha maana ya Mikono miwili anayosifiwa nayo Allaah (Ta´ala) na kusema kuwa ni nguvu, neema na mfano wa hayo.

Ukanushaji (Ta´twiyl): Maana yake kilugha ni kufanya kitu “kitupu”. Maana yake kidini ni “ima kupinga majina na sifa zote ambazo ni wajibu Allaah kuthibitishiwa au kupinga baadhi yazo”. Hili linaweza kufanyika kwa njia mbili:

Ya kwanza: Kukanusha kikamilifu. Hili kwa mfano linafanywa na Jahmiyyah ambao wanakanusha sifa na wale waliopindukia wanakanusha majina pia.

Ya pili: Kukanusha sehemu tu. Hili kwa mfano linafanywa na Ashaa´irah ambao wakananusha baadhi ya sifa. Mtu wa kwanza anayejulikana kukanusha sifa ni al-Ja´d bin Dirham.

Kufanya namna (Takyiyf): Maana yake ni kuifanyia sifa namna. Kwa mfano mtu kusema mkono wa Allaah au Anavyoshuka katika mbingu ya chini ya dunia ni namna hivi na hivi.

Kufananisha (Tamthiyl) na kushabihisha (Tashbiyh): Kufananisha maana yake ni kulinganisha kitu na kingine. Kushabihisha maana yake ni kushabihisha kitu na kingine. Kuna uwezekano tamko moja likaingia ndani ya lingine. Tofauti kati ya istilahi hizo mbili na kufanya namna ni ifuatayo:

Ya kwanza: Kufanya namna ni kuelezea namna ya kitu kwa njia isiyofungamanishwa au kwa njia iliyofungamanishwa. Upande mwingine kufananisha na kushabihisha kunaonyesha namna yenye kulinganishwa na nyingine na kushabihiana nayo. Kwa njia kama hii ufanyaji namna ni kitu kilichoenea kwa vile kila mwenye kufananisha ni mwenye kufanya namna na si kinyume chake.

Ya pili: Kufanya namna ni jambo maalum linalofanywa katika sifa. Lakini kufananisha kunakuwa katika hadhi, sifa na dhati. Kwa njia hii kufananisha inakuwa ni jambo lililoenea kwa vile linahusiana na dhati, sifa na hadhi. Jengine ni kwamba ushabihishaji, ambao umewafanya wengi kupotea, unagawanyika sehemu mbili:

Ya kwanza: Kumshabihisha kiumbe na Muumba.

Ya pili: Kumshabihisha Muumba na kiumbe.

Kumshabihisha kiumbe na Muumba ina maana ya kumwelezea kiumbe kwa sifa ambayo ni maalum kwa Muumba kama matendo, haki na sifa. Mfano wa matendo, ni kama kuonelea kuwa kuna muumbaji anayeshirikiana na Allaah. Mfano wa haki, ni kama kuonelea kuwa masanamu yana haki ya kuabudiwa. Hivyo washirikina wakamshirikisha kwayo Allaah. Mfano wa sifa, ni yale yanayofanywa na baadhi pindi wanapopitiliza kumsifu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kuhusu kumshabihisha Muumba na kiumbe ina maana ya kuthibitisha dhati ya Allaah maalum na sifa kama ambavyo mtu anavyomthibitishia kiumbe. Mfano wa hilo ni kama mtu kusema kuwa mikono miwili ya Allaah ni kama mikono ya viumbe, kulingana Kwake juu ya ´Arshi ni kama kulingana kwao n.k. Mtu wa kwanza kujulikana kwa hili ni Hishaam bin al-Hakam ar-Raafidhwiy – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

Upindaji (Ilhaad): Maana yake kilugha ni “kupinda”. Maana yake kidini ni “kupinda juu ya yale ambayo ni wajibu kuyaamini au kuyatendea kazi”. Umegawanyika sehemu mbili:

Ya kwanza: Kupinda katika majina ya Allaah.

Ya pili: Kupinda katika ishara/alama za Allaah.

Kupinda katika majina Yake ina maana ya kuharibu haki zake za wajibu. Hili limegawanyika sehemu nne:

Mosi: Kupinga kitu katika majina hayo au sifa zilizofahamihwa na dalili. Haya yamefanywa na Mu´tazilah.

Pili: Kudai kwamba yanafahamisha juu ya kumshabihisha Allaah na viumbe Wake. Haya yamefanywa na Mushabbihah.

Tatu: Kumwita Allaah kwa jina ambalo hakujiita Mwenyewe, kwa sababu majina ya Allaah ni jambo la kukomeka. Mfano wa hilo wakristo wanamwita Allaah kuwa ni “Baba” na wanafalsafa wanamwita “Msababishaji” na mfano wa hayo.

Nne: Kunyofoa jina la masanamu kutoka katika majina ya Allaah. Kwa mfano walinyofoa jina al-Ilaah (Mungu) na kumpa nalo sanamu al-Laat. Kadhalika jina al-´Aziyz na wakampa nalo sanamu al-´Uzzaa.

Kupinda katika alama za Allaah inakuwa katika alama za Kishari´ah, zile hukumu na maelezo ambayo Mitume walikuja nayo, au inaweza kuwa katika alama za kilimwengu, ambazo Allaah ameumba mbinguni na ardhini.

Kupinda katika ishara za Kishari´ah ina maana ya kuzipotosha, kukadhibisha maelezo Yake au kuasi hukumu zake.

Kupinda katika ishara za Allaah za kilimwengu ina maana ya kuzinasibisha kwa mwengine asiyekuwa Allaah, kuamini mshirika au mwenza na mfano wa hayo.

Upindaji wote aina mbili ni haramu. Allaah (Ta´ala) amewatishia wenye kufanya hivi na kusema:

وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Waacheni wale wanaopotoa katika majina Yake, watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda.”[6]

إِنَّ الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي آيَاتِنَا لا يَخْفَوْنَ عَلَيْنَا أَفَمَنْ يُلْقَى فِي النَّارِ خَيْرٌ أَمَّنْ يَأْتِي آمِناً يَوْمَ الْقِيَامَةِ اعْمَلُوا مَا شِئْتُمْ إِنَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ

“Hakika wale wanaozipotosha Aayaat Zetu hawawi kujificha kwetu. Je, basi yule atakayetupwa katika Moto ni bora au yule atakayekuja akiwa katika amani Siku ya Qiyaamah? Tendeni mpendavyo; hakika Yeye kwa myatendayo ni Mwenye kuona.”[7]

Kuna upindaji ambao ni kufuru kutegemea na vile maandiko katika Kitabu na Sunnah yanavyopelekea.

[1] 07:180

[2] 42:11

[3] 17:36

[4] 04:164

[5] 01:02

[6] 07:180

[7] 41:40

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 12-22
  • Imechapishwa: 07/01/2020