Hebu wacha tupige mfano

Miongoni mwa majina ya Allaah ni Mwenye kusikia (السميع). Kwa mujibu wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni lazima kuthibitisha jina hilo ambalo ni la Allaah. Hivyo mtu amuombe na amwabudu Allaah kwalo. Kwa mfano mtu anaweza kujiita ´Abdus-Samiy (mja wa Mwenye kusikia) na amwite “Ee Mwenye kusikia!”, “Ee Mjuzi wa kila jambo” na mfano wa hivo. Kwa sababu Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا

”Allaah ana Majina mazuri kabisa, hivyo basi muombeni kwayo.”[1]

Vivyo hivyo mtu anatakiwa kuthibitisha ile sifa inayofahamishwa na jina hilo ambayo ni sifa ya usikizi. Hivyo tunamthibitishia usikizi wenye kuenea usiofichikwa na sauti yoyote japokuwa itakuwa nyonge.

Vilevile tunatakiwa kumthibitishia athari ya sifa hii ambayo ni kwamba Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) anasikia kila kitu. Hivyo tutafaidika faida kubwa kutoka katika majina ya Allaah. Kwa sababu mambo haya matatu tuliyothibitisha yanapelekea sisi kumwabudu Allaah ikiwa yanapelekea katika sifa nyingine (المتعدية). Hivyo tutakuwa ni wenye kutendea kazi maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا

”Allaah ana Majina mazuri kabisa, hivyo basi muombeni kwayo.”[2]

Wewe ukiamini ya kwamba Allaah ni Mwenye kusikia basi hutomsikilizisha Mola wako yale yenye kumfanya kukukasirikia. Utamsikiliza tu yale yenye kukufanya Yeye kuweza kukuridhia. Kwa sababu unaamini chochote utakachosema katika maneno. Ni mamoja umeyasema kwa siri au kwa dhahiri basi Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) anayasikia. Hiyo siku ya Qiyaamah atakujuza yale uliyokuwa ukiyasema. Atakufanyia hesabu juu ya hayo kwa kiasi cha vile hekima Yake itavyopelekea kwa namna inayoendana Naye (Tabaarak wa Ta´ala). Kwa hiyo kanuni kwa mujibu wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kwamba jina likiwa linapelekea katika sifa nyingine basi haiwezekani kulihakiki isipokuwa mpaka mtu aamini mambo matatu yafuatayo:

1- Kuamini kwamba ni jina la Allaah na hivyo tumthibishie nalo.

2- Kuamini ile sifa iliofahamishwa.

3- Kuamini ile athari inayopelekewa na sifa hiyo.

Kwa mambo haya mtu atakuwa amehakikisha imani ya kuamini majina ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) yanayopelekea katika sifa nyingine.

[1] 07:180

[2] 07:180

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manhaj Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah fiy-´Aqiydah wal-´Amal, uk. 11-12
  • Imechapishwa: 28/06/2019