04. Mazingatio yanayopatikana juu ya kisa cha waja wema kutoka kwa watu wa Nuuh

Ile Athar tulioipitia iliyopokelewa na al-Bukhaariy kupitia kwa Ibn ´Abbaas katika kubainisha sababu za kuzuka kwa shirki kwa watu wa Nuuh tunapata kujifunza yafuatayo:

Mosi: Ukhatari wa kutundika picha kwenye kuta na kutengeneza masanamu katika vikao na kwamba hilo mwishowe huwapeleka watu katika shirki. Hatimaye mambo huwa makubwa na mapicha na masanamu yale yakaadhimishwa mpaka kufikia kuabudiwa na kuamini kuwa ndio yenye kuleta kheri na kuzuia shari, kama ilivyokuwa kwa watu wa Nuuh.

Pili: Shaytwaan anavyopupia kumpotosha mwanaadamu na namna anavyowafanyia vitimbi na kwamba wakati mwingine anaweza kuwajia kwa njia ya kuzitumia zile hisia zao na madai kwamba anawaita katika kheri. Alipoona kuwa watu wa Nuuh wanawaheshimu waja wema na wanawapenda ndipo akawalingania katika upetukaji kutokana na mapenzi haya kwa njia ya kwamba akawaamrisha waweke mapicha yao kwenye vikao vyao. Malengo yake ilikuwa kuwatoa katika njia ya sawa.

Tatu: Shaytwaan haishilii kutazama kizazi kilichoko hivi sasa. Bali anatazama kizazi kitachokuja huko mbele. Aliposhindwa kufanya shirki itokee katika kizazi kilichokuwepo wakati huo, watu wa Nuuh, ndipo akawa na matarajio juu ya kizazi kitachokuja huko mbele na akawawekea mitego.

Nne: Haijuzu kuchukulia wepesi juu ya njia za shirki. Bali ni wajibu kuzikata na kufunga njia zake.

Tano: Fadhilah ya wanachuoni watenda kazi na kwamba uwepo wao kati ya watu ni kheri na kukosekana kwao ni shari. Shaytwaan alishindwa kuwapotosha watu wa Nuuh mpaka walipofariki wote.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Haqiyqat-it-Tawhiyd, uk. 08-09
  • Imechapishwa: 04/02/2019