04. Mambo ya kidharurah matano ambayo ni wajibu kuyachunga


Kwa sababu dini ndio jambo la kwanza katika mambo ya kidharurah matano ambayo ni wajibu kuyahifadhi. Kwa hivyo dini ni wajibu kuhifadhiwa na ni wajibu vilevile kutekeleza hukumu za wale wanaoritadi juu ya wale wanaotoka katika Uislamu. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kubadilisha dini muueni.”[1]

“Damu ya muislamu haiwi halali isipokuwa kwa moja ya mambo matatu; nafsi kwa nafsi nyingine, mzinifu ambaye kishaoa/olewa na mwenye kuiacha dini yake anayefarikisha Jamaa´ah.”[2]

Kinacholengwa ni maneno yake:

“… na mwenye kuiacha dini yake anayefarikisha Jamaa´ah.”

2- Jambo la kidharurah la pili: Nafsi. Ndio maana Allaah akawekea katika Shari´ah kisasi. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِصَاصُ فِي الْقَتْلَى ۖ الْحُرُّ بِالْحُرِّ وَالْعَبْدُ بِالْعَبْدِ وَالْأُنثَىٰ بِالْأُنثَىٰ ۚ فَمَنْ عُفِيَ لَهُ مِنْ أَخِيهِ شَيْءٌ فَاتِّبَاعٌ بِالْمَعْرُوفِ وَأَدَاءٌ إِلَيْهِ بِإِحْسَانٍ ۗ ذَٰلِكَ تَخْفِيفٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَرَحْمَةٌ ۗ فَمَنِ اعْتَدَىٰ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَلَهُ عَذَابٌ أَلِيمٌ وَلَكُمْ فِي الْقِصَاصِ حَيَاةٌ يَا أُولِي الْأَلْبَابِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Enyi walioamini! Mmeandikiwa shari´ah ya kisasi kwa waliouawa; muungwana kwa muungwana, na mtumwa kwa mtumwa, na mwanamke kwa mwanamke – na anayesamehewa na nduguye kwa lolote basi kufuatilizwa kwake kuwe kwa wema na kumlipa kwake iwe kwa ihsani. Hiyo ni takhafifu kutoka kwa Mola wenu na rehema. Atakayevuka mipaka baada ya hapo basi atapata adhabu iumizayo. Na mtapata katika kisasi kuokoa uhai, enyi wenye akili ili mpate kuwa na uchaji.” (al-Baqarah 02:178-179)

Hivyo Akaamrisha kuhifadh nafsi iliyoamini. Kwa ajili hii ndio maana akaweka katika Shari´ah kisasi kwa ajili ya kuhifadhi nafsi dhidi ya mashambulizi:

وَلَكُمْ فِي الْقِصَاصِ حَيَاةٌ

“Na mtapata katika kisasi kuokoa uhai.”

Kisasi, ijapokuwa ni kuua vilevile, kunasababisha kupatikana uhai kwa watu. Kwa sababu kunazuia mauaji. Watu wanapata amani juu ya damu zao. Yule muuaji au yule anayetaka kuua akijua kuwa na yeye pia atauawa, basi atajizuia na mauji. Hivyo anakuwa ameisalimisha nafsi yake na amemsalimisha vilevile yule aliyekuwa amekusudia kumuua. Hivyo inapata kuhifadhi damu.

3- Jambo la tatu katika mambo ya kidharurah matano ni akili. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amemuumba mwanadamu huyu na akampambanua kutokamana na viumbe wengine kwa kule kumpa akili, ambayo anaitumia kwa kupambanua kati ya chenye manufaa na chenye kudhuru, kizuri na kibaya, kufuru na imani:

وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ وَحَمَلْنَاهُمْ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ

“Hakika Tumewakirimu wanaadamu na tukawabeba katika nchi kavu na baharini.” (al-Israa´ 17:70)

لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ فِي أَحْسَنِ تَقْوِيمٍ

”Hakika Tumemuumba mwanaadamu katika umbile bora kabisa.” (at-Tiyn 95:04)

 Allaah (Jalla wa ´Alaa) amempambanua mwanadamu huyu kwa akili hii. Hivyo mwanadamu huyu akiitumia vibaya akili hii, kama akatumia kitu katika madawa ya kulevya, basi Allaah amewajibisha asimamishiwe adhabu ya Kishari´ah kwa kupigwa bakora. Yote haya kwa ajili ya kuhifadhi akili isichezewe.

4- Jambo la nne katika mambo ya kidharurah matano ni kuhifadhi mali. Ni lazima kwa watu wawe na mali ambayo kwayo wataweza kusimamisha manufaa yao. Mali ndio mishipa ya maisha – kama wanavosema wenyewe. Amesema (Ta´ala):

وَلَا تُؤْتُوا السُّفَهَاءَ أَمْوَالَكُمُ الَّتِي جَعَلَ اللَّـهُ لَكُمْ قِيَامًا

“Wala msiwape wasiokomaa kiakili mali yenu ambayo Allaah ameifanya kuwa ni kisaidizi chenu cha maisha.” (an-Nisaa´ 04:05)

Yule mwenye kushambulia mali ya watu kwa kuiiba, basi mkono wake unatakiwa kukatwa ili watu wasalimike na mali yao. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

وَالسَّارِقُ وَالسَّارِقَةُ فَاقْطَعُوا أَيْدِيَهُمَا جَزَاءً بِمَا كَسَبَا نَكَالًا مِّنَ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

“Mwizi mwanamume na mwizi mwanamke ikateni mikono yao – ni malipo kwa yale waliyoyachuma, ndio adhabu ya kupigiwa mfano kutoka kwa Allaah. Allaah ni Mwenye nguvu kabisa, Mwenye hekima.” (al-Maaidah 05:38)

Mkono mmoja ukikatwa, mali ya watu itahifadhika na watu watasalimika na mali yao. Kwa ajili hiyo zile nchi ambazo zinasimamisha adhabu za Kishari´ah mtaziona ni zenye amani na zenye utulivu katika dini yao, nafsi zao, mali yao na heshima zao. Upande mwingine zile nchi zisizosimamisha adhabu za Kishari´ah ni zenye kuingiliwa na vurugu, fujo, khofu na unyama. Mambo hayo yanatambulika.

5- Jambo la tano katika mambo ya kidharurah matano ni kuhifadhi nasabu na heshima. Hilo ni kwa kuharamisha uzinzi na kuwajibisha kusimamishiwa adhabu kwa mwenye kuzini. Akiwa ni bikira basi anatakiwa kupigwa bakora mia moja. Akiwa tayari ni mtumzima basi anatakiwa kupigwa mawe mpaka afe. Yote haya kwa ajili ya kuhifadhi kuchanganyika kwa nasabu. Wazinifu wakisimamishiwa adhabu, basi nasabu za watu zitahifadhika. Lakini wazinzi wakiachwa kusimamishiwa adhabu, nasabu zitachanganyika. Mtoto hatojulikani ni nani baba yake kwa sababu ya kuchanganyika kwa nasabu. Mwanamke huyu ataingiliwa na wanaume wengi na hivyo isijulikane ni nani kambebesha mimba. Hivyo nasabu, ambayo Allaah ameiweka kati ya watu kwa lengo kila mmoja apate kujulikana ni kutokamana na nani, itapotea. Jengine ni kwamba nasabu inapelekea katika hukumu za Kishari´ah kama za umahramu, mirathi na hukumu nyenginezo zilizofungamana na nasabu. Nasabu inapata kufanya watu kufahamiana kwa njia ya kwamba mtu anapata kumfahamu fulani kwamba ndiye baba yake, fulani ndiye kaka yake, fulani ndiye ami yake, fulani ndiye mjomba wake. Matokeo yake watu wanapata kuungana. Huku ndio kuhifadhi nasabu.

Kuhusu kuhifadhi heshima za watu, nako inakuwa kwa kuwasimamishia adhabu wale wanaowatumu wengine machafu. Yule anayewatuhumu wengine machafu na kusem “fulani ni mzinifu”, “fulani ni mfanya liwati”, n.k., mtu huyu atatakiwa kuleta mashahidi wane ambao watatakiwa kutoa ushahidi juu ya maneno aliyosema. Vinginevyo atapigwa bakora themanini na utaanguka uadilifu wake na hivyo anakuwa fasiki. Amesema (Ta´ala):

وَالَّذِينَ يَرْمُونَ الْمُحْصَنَاتِ ثُمَّ لَمْ يَأْتُوا بِأَرْبَعَةِ شُهَدَاءَ فَاجْلِدُوهُمْ ثَمَانِينَ جَلْدَةً وَلَا تَقْبَلُوا لَهُمْ شَهَادَةً أَبَدًا ۚ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ إِلَّا الَّذِينَ تَابُوا مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ وَأَصْلَحُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

“Wale wanaowatuhumu wanawake watwaharifu kisha wasilete mashahidi wanne, basi wapigeni bakora themanini na wala msipokee ushahidi wao kabisa – na hao ndio mafasiki. Isipokuwa wale waliotubu baada ya hayo na wakatengemaa, basi hakika Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.” (an-Nuur 24:04-05)

Haya ndio mambo ya kidharurah matano ambayo Allaah kaamrisha kuyahifadhi na akapanga adhabu juu yake ambapo jambo la kwanza ni kuihifadhi dini. Kuihifadhi dini kunakuwa kwa kujiepusha na vitenguzi ambavyo vinaitengua dini hii na kusimamisha adhabu kwa yule mwenye kuritadi kutoka katika dini hii na kumfanya mtu akaritadi. Kunakuwa vilevile kwa kumuua yule mwenye kuritadi.

[1] al-Bukhaariy (3017), an-Nasaa´iy (4059), at-Tirmidhiy (1458) na Ahmad (1871) kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

[2] al-Bukhaariy (6878), Muslim (1676), Abu Daawuud (4352), at-Tirmidhiy (1402), an-Nisaa´iy (4016), Ibn Maajah (2534) kupitia kwa ´Abdullaa bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 17-20
  • Imechapishwa: 03/05/2018