04. Madhehebu ya Jabriyyah yanaivunja Shari´ah tokea kwenye msingi wake

Iwapo tungefuata maoni ya pote la kwanza ambalo limepindukia katika kuthibitisha makadirio Shari´ah ingevunjika kutoka kwenye msingi wake. Kwa sababu maoni yanayosema kuwa mja hana utashi yanapelekea yule mwenye kufanya matendo mema asisifiwe na yule mwenye kufanya matendo mabaya asikatazwe kwa kuwa hakuna katika wao aliyefanya kitu kwa kutaka. Natija inakuwa – na Allaah ametakasika kutokamana na hayo – ya kwamba Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ni dhalimu kwa mtenda dhambi endapo atamuadhibu kwa dhambi yake kwa kuwa atakuwa amemuadhibu kwa kitu alichokifanya pasi na kutaka kwake. Hili ni jambo linalopingana na Qur-aan. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

وَقَالَ قَرِينُهُ هَـٰذَا مَا لَدَيَّ عَتِيدٌ أَلْقِيَا فِي جَهَنَّمَ كُلَّ كَفَّارٍ عَنِيدٍ مَّنَّاعٍ لِّلْخَيْرِ مُعْتَدٍ مُّرِيبٍ الَّذِي جَعَلَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَأَلْقِيَاهُ فِي الْعَذَابِ الشَّدِيدِ قَالَ قَرِينُهُ رَبَّنَا مَا أَطْغَيْتُهُ وَلَـٰكِن كَانَ فِي ضَلَالٍ بَعِيدٍ قَالَ لَا تَخْتَصِمُوا لَدَيَّ وَقَدْ قَدَّمْتُ إِلَيْكُم بِالْوَعِيدِ مَا يُبَدَّلُ الْقَوْلُ لَدَيَّ وَمَا أَنَا بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ

“Mwenzake atasema: “Haya yaliyoko kwangu yameshatayarishwa.” [Hapo ndipo itapita hukumu ya Allaah:] “Mtupeni Motoni kila ambaye ni kafiri mno na mkaidi mzuiaji wa kheri, mrukaji mipaka na mwenye kutia shaka ambaye ameweka pamoja na Allaah mungu mwingine – mtupeni katika adhabu kali!” Rafiki yake aliyekuwa akimfuata kila mahala [hapa duniani] atasema: “Mola wetu, sikumpoteza mimi akaasi; lakini yeye mwenyewe alikuwa katika upotofu wa kipindukia! [Allaah] atasema: “Msikhasimiane mbele Yangu! Nilikutangulizeni maonyo. Haibadilishwi hukumu Yangu, na Mimi si mwenye kuwadhulumu waja Wangu.”[1]

Amebainisha (Subhaanah) ya kwamba adhabu Yake sio dhulumu bali ni uadilifu kamili. Kwa kuwa Allaah amewatangulizia matishio, akawaonyesha njia iliyonyooka na akawabainishia haki na batili. Hawana hoja mbele ya Allaah (´Azza wa Jall). Lau tungelikuwa na maoni yao haya batili basi maneno ya Allaah (Ta´ala):

رُّسُلًا مُّبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى اللَّـهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ

“Mitume wenye kutoa bishara njema na wenye kutoa maonyo, ili pasikuwepo hoja yoyote kwa watu juu ya Allaah baada ya [kutumwa] Mitume.”[2]

yangelibatilika. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amekataa watu kuwa na hoja baada ya kutumwa Mitume. Kwa kuwa hoja imewasimamia. Lau makadirio yangelikuwa ni hoja kwao basi hoja hii ingeliendelea kufanya kazi hata baada ya kutumwa Mitume kwa kuwa makadirio ya Allaah (Ta´ala) ni yenye kuendelea siku zote, kabla na baada ya kutumwa Mitume. Kwa hiyo maoni haya yanabatilishwa kwa dalili na ukweli wa mambo, kama tulivyopambanua kwa mifano iliyotangulia.

[1] 50:22-29

[2] 04:165

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Qadhwaa’ wal-Qadar, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (5/218-219)
  • Imechapishwa: 25/10/2016