04. Kujitenga mbali na mizozo, mijadala na magomvi

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“… na kujiepusha na kurushiana maneno, mijadala na ugomvi katika dini.”

MAELEZO

Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah ni kujiepusha na kurushiana maneno, mijadala na ugomvi katika dini.

Mizozo haina lengo sahihi. Sio katika tabia za Ahl-us-Sunnah. Haina kheri ndani yake. Watu wabaya tu ndio wenye kujishughulisha na mambo hayo. Lengo lao ni kuwashinda wengine, sio kuifanya haki ndio ishinde na kuisaga batili. Inahusiana tu na kufuata matamanio. Imekuja katika upokezi:

“Ubishi katika Qur-aan ni kufuru.”[1]

Qur-aan haiteremshwa isipokuwa tu ni kwa ajili ya kutendewa kazi na kufuatwa, sio kwa ajili ya kuzozana nayo wapumbavu na wajinga katika Ahl-ul-Bid´ah na wengineo.

Kadhalika inahusiana na mizozo iliyokatazwa isiyopelekea katika manufaa yoyote juu ya Uislamu na waislamu. Pindi watu watapoingia kwa wingi kwenye mizozo ya kidini ndipo watakuwa na shubuha na nyoyo dhaifu. Ahl-ul-Bid´ah wanawapaka watu mchanga wa machoni na kuwavuta kwao. Wakiweza kumvuta mtu kutoka katika Sunnah na kumwingiza kwenye Bid´ah, wanafanya hivo. Wanamshawishi yule wanayeweza kumshawishi. Hatimaye anakuwa ni mwenye kudangana; anakuwa hajui ni wapi pa sawa na ni njia ipi inayoelekeza katika uokozi. Lakini wale wenye kushikamana na Sunnah wanabaki hali ya kuwa ni mwenye kuthibiti kwa mujibu wa yale yaliyotajwa katika Qur-aan na Sunnah na ufahamu sahihi. Anapokuja mtu mwenye kufuata matamanio yake kwenda kwa mtu wa Ahl-us-Sunnah kwa ajili ya kubishana na kujadiliana naye, hawamkubalii. Hawamuitikii. Hawafanyi naye vikao. Wanazungumza tu na yule mtu anayetaka haki ili aweze kuitendea kazi. Hata kama baadhi ya mambo yanaweza kuwa hayako wazi, wanambainishia. Hivi ndivo wanavyokuwa kwa yule mtu anayetaka ubainifu. Wanampangia vikao kwa ajili ya kumbainishia yale mambo yasiyokuwa wazi kwake, wanamkaribisha katika Sunnah na wanamtahadharisha juu ya wazushi wenye kupotosha wanaomsababishia kupata adhabu duniani na Aakhirah.

Ama kuhusu mtu ambaye anawajia kwa ajili ya kujadiliana na kubishana nao na wakashauri kwamba yule mwenye kushinda mjadala ndiye ambaye anatakiwa kufuatwa, hawamkubalii. Ubishi kama huu ndio ambao haukubaliwi na Salaf na wafuasi wao.

[1] Ahmad (7835) na Abu Daawuud (4603). Swahiyh kwa mujibu wa Ahmad Shaakir na Swahiyh na nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy.

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 24-25
  • Imechapishwa: 01/10/2019