Swali 4: Leo tunasikia sana kukisemwa “makundi ya Kiislamu” ulimwenguni kote. Je, inajuzu kwenda pamoja nao na kushirikiana nao ikiwa hawana Bid´ah?

Jibu: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametueleza na kutuwekea wazi nini tunachotakiwa kufanya. Hakuna kitu ambacho kinaukurubisha ummah kwa Allaah isipokuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekibainisha[1] ikiwa ni pamoja na suala hili. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Hakika yule katika nyinyi atakayeishi kipindi kirefu basi atakuja kuona tofauti nyingi.”

Vipi jambo hili litatatuliwa wakati litapotokea? Akasema:

”Hivyo basi, lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu na wenye kuongoza. Ziumeni kwa magego yenu. Na nakutahadharisheni na mambo yaliyozuliwa, kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotofu.”[2]

Sisi tunajinasibisha na yale makundi[3] yanayomfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Maswahabah na khaswa wale makhaliyfah waongofu na vile vizazi bora. Sisi tuko pamoja na wao na kufanya nao kazi.

Kila chenye kwenda kinyume na uongofu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tunajitenga nacho. Haijalishi kitu hata kama watajiita “makundi ya Kiislamu”. Kinachozingatiwa ni uhakika wa mambo, na sio majina. Kuna majina yalio na maana yenye kuvutia, lakini ni mashimo. Hana lolote na pengine hata yakawa ni batili. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mayahudi wamegawanyika makundi sabini na moja. Manaswara wamegawanyika makundi sabini na mbili.  Na ummah wangu utagawanyika katika mapote sabini na mbili. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu.” Wakasema: ”Ni lipi hilo, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: ”Ni lile linalofuata yale ninayofuata mii hii leo na Maswahabah zangu.”[4]

Njia iko wazi kabisa. Kuwa pamoja na kundi lililo na sifa hii. Lile linalofuata yale ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifuata na Maswahabah zake, ndio kundi la Kiislamu na la haki.

Kuhusiana na kila chenye kwenda kinyume na mfumo huu na akafuata mfumo mwingine, yeye si katika sisi na sisi si katika wao. Hatujinasibishi nalo na lenyewe halijinasibishi na sisi. Wala lisijiite kuwa ni “kundi”. Linatakiwa kuitwa “pote potofu”. Kundi ni lile lenye kushikamana na haki na watu wakakusanyika kwalo. Kuhusu batili, hutenganisha na wala haileti umoja. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَّإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا هُمْ فِي شِقَاقٍ

“Wakikengeuka [na kwenda njia nyingine], basi hakika wao wamo katika upinzani.”[5]

[1] Shaykh (Hafidhwahu Allaah) anaashiria ile Hadiyth iliyothibiti na Swahiyh ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Sikuacha kitu kinachowakurubisha kwa Allaah isipokuwa nimekuamrisheni nacho.” (´Abdur-Razzaaq katika ”al-Muswannaf” (11/125) na al-Bayhaqiy katika ”Ma´rifat-us-Sunan wal-Aathaar” (1/20))

[2] Abu Daawuud (4607), at-Tirmidhiy (2676) na Ibn Maajah (34). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (2455).

[3] Ni sawa kuwaita wale wote wanaoenda kinyume na Qur-aan, Sunnah na ufahamu wa Salaf “mapote”. Ni jina lililowekwa katika Shari´ah kwao. Kama ambavyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyowaita. Kuhusiana na jina “makundi”, waislamu wana kundi limoja tu kama alivyoashiria – na Allaah ndiye anajua zaidi.

[4] Ibn Maajah (3992), at-Tirmidhiy (2641) na Abu Daawuud (4596). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Mishkaat-ul-Maswaabiyh” (171).

[5] 02:137

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 24-26
  • Imechapishwa: 18/02/2017