04. Je, Inajuzu kujiunga na makundi ya Kiislamu?


Swali 4: Leo tunasikia sana kukisemwa “makundi ya Kiislamu” ulimwenguni kote. Je, inajuzu kwenda pamoja nao na kushirikiana nao ikiwa hawana Bid´ah?

Jibu: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametueleza na kutuwekea wazi nini tunachotakiwa kufanya. Hakuna kitu ambacho kinaukurubisha Ummah kwa Allaah isipokuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekibainisha[1] ikiwa ni pamoja na suala hili. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika yule atakayeishi katika nyinyi basi ataona tofauti nyingi.”

Vipi jambo hili litatatuliwa wakati litapotokea? Akasema:

“Jilazimisheni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhaliyfah wangu waongofu baada yangu. Shikamaneni nazo bara bara na ziumeni kwa magego yenu. Tahadharini na mambo ya kuzua, kwani hakika kila kitakachozushwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”[2]

Sisi tunajinasibisha na yale makundi[3] yanayomfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Maswahabah na khaswa wale Makhaliyfah waongofu na karne bora. Sisi tuko pamoja na wao na kufanya nao kazi.

Kila chenye kwenda kinyume na uongofu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tunajitenga nacho. Haijalishi kitu hata kama watajiita “makundi ya Kiislamu”. Kinachozingatiwa ni uhakika wa mambo, na sio majina. Kuna majina yalio na maana yenye kuvutia, lakini ni mashimo. Hana lolote na pengine hata yakawa ni batili. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mayahudi wamegawanyika mapote sabini na moja. Manaswara wamegawanyika mapote sabini na mbili. Na Ummah wangu utakuja kugawanyika mapote sabini na tatu. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu.” Wakasema: “Ni lipi, ewe Mtume wa Allaah?” Akasema: “Ni lile linalofuata yale niliyomo mimi leo na Maswahabah zangu.”[4]

Njia iko wazi kabisa. Kuwa pamoja na kundi lililo na sifa hii. Lile linalofuata yale ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifuata na Maswahabah zake, ndio kundi la Kiislamu na la haki.

Kuhusiana na kila chenye kwenda kinyume na mfumo huu na akafuata mfumo mwingine, yeye si katika sisi na sisi si katika wao. Hatujinasibishi nalo na lenyewe halijinasibishi na sisi. Wala lisijiite kuwa ni “kundi”. Linatakiwa kuitwa “pote potevu”. Kundi ni lile lenye kushikamana na haki na watu wakakusanyika kwayo. Ama upotevu, unafarikanisha. Haufanyi umoja. Allaah (Ta´ala) Amesema:

وَّإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا هُمْ فِي شِقَاقٍ

“Na wakikengeuka [na kwenda njia nyingine], basi hakika wao wamo katika upinzani.” (02:137)

“Sikuacha kitu kinachowakurubisha kwa Allaah isipokuwa nimekuamrisheni nacho.” (´Abdur-Razzaaq katika ”al-Muswannaf” (11/125) na al-Bayhaqiy katika ”Ma´rifat-us-Sunan wal-Aathaar” (1/20))[1] Shaykh (Hafidhwahu Allaah) anaashiria Hadiyth iliyothibiti Swahiyh ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

[2] Swahiyh kwa njia zake zote. Abu Daawuud (4607), at-Tirmidhiy (2676) na Ibn Maajah (34). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (2455).

[3] Ni sawa kumwita kila anayeenda kinyume na Qur-aan, Sunnah na ufahamu wa wema waliotangulia (Salaf-us-Swaalih) “mapote”. Ni jina lililowekwa katika Shari´ah kwao. Kama ambavyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyowaita. Kuhusiana na jina “makundi”, waislamu wana kundi limoja tu kama alivyoashiria na Allaah ndiye Anajua zaidi.

[4] at-Tirmidhiy (2641) na al-Haakim (1/129). Inatiliwa nguvu na mapokezi ”Ni mkusanyiko (Jamaa´ah).” Rejea katika ”Tuhfat-ul-Ahwadhiy” (7/398). Upokezi huu umepokelewa na Ibn Maajah (3992) na Abu Daawuud (4597).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Adjwibah al-Mufiydah ´an As'ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 24-26
  • Imechapishwa: 18/02/2017