04. Imani na elimu vitakuja kutulizana Shaam

18- ´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aasw ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Niliona kama nguzo ya Kitabu inavutwa kutoka chini ya mto wangu. Nikaiandama kwa macho na kuona kuwa ni nuru yenye kuangaza inayopelekwa kuelekea Shaam. Pindi kutapotokea mtihani imani itakuwa Shaam.”

Ameipokea al-Haakim aliyesema:

“Ni Swahiyh kwa masharti ya al-Bukhaariy na Muslim.”

19- Imaam Ahmad na an-Nasaa´iy wamepokea kupitia kwa Salamah bin Nufayl ambaye amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Kutaendelea siku zote kuwepo kundi kutoka katika Ummah wangu litalokuwa shindi juu ya watu. Allaah atapotosha nyoyo za kundi la watu ambapo wataanza kuwapiga vita. Wataendelea kuwa katika hali hiyo mpaka ije amri ya Allaah. Tanabahi! Msingi wa nyumbani kwa waumini ni Shaam.”

20- Haafidhw Abul-Qaasim amepokea kwa mlolongo wa wapokezi wake kupitia kwa Abud-Dardaa´ ya kwamba alikuwa Dameski na Mu´aawiyah akamuomba arudi Hims. Ndipo akasema:

“Ee Mu´aawiyah! Unaniamrisha kutoka katika msingi wa nyumba ya Kiislamu?”

21- ´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aasw ameeleza kuwa Mtume (Swalla Alalahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Zitafika zama ambapo hakutakuwepo muumini isipokuwa atajiunga na Shaam.”

Ameipokea Abul-Qaasim ad-Dimashqiy katika “at-Taariykh” ambaye amesema:

“Ameipokea Ibn-ul-Mubaarak, Ibn Mahdiy, Qaabiswah na Abu Hudhayfah kupitia kwa Sufyaan. Yaliyo Swahiyh zaidi ni matamshi haya ya maneno ya ´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aasw.”

22- al-Mas´uudiy amepokea kupitia kwa al-Qaasim bin ´Abdir-Rahmaan ambaye amesema:

“Eufrat ilipanuka wakati wa ´Abdullaah bin Mas´uud, kitu ambacho watu hawakukipenda. Ibn Mas´uud akasema: “Enyi watu! Msichukie kupanuka kwake. Hakika kunakaribia mtu atataka kujaza maji kwenye pipa kwa maji yake na asipate kitu. Hapo itakuwa pale kila maji yataporudi katika shimo lake na waislamu waliobaki watakuwa Shaam.”

23- Ibn ´Umar amesema:

“Utafika wakati ambapo hakutakuwa muumini isipokuwa atakuwa Shaam.”

24- ´Abdur-Rahmaan bin Yaziyd bin Jaabir amesema:

“Kulikuwa kunasemwa: “Yule anayetaka elimu basi ahame kwenda Daarayyah kati ya ´Ans na Khawlaan.”

25- ´Atwaa´ al-Khuraasaaniy amesema:

“Sijawahi kumuona Faqiyh mkubwa kama mtu aliye Shaam.”

26- Ibn-ul-Mubaarak amesema:

“Sikuja Shaam isipokuwa tu ni kwa sababu nisiwe na haja ya Hadiyth za watu wa Kuufah.”

27- Mwanzoni tumetaja Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) inayoifasiri ndoto ya kwamba Qur-aan itakuja kutulizana Shaam kupitia utawala. Qur-aan itashinda kupitia utawala utaoitia nguvu. Yule mwenye kuipiga vita atapigwa vita. Allaah amekusanya kati ya hayo mawili pale aliposema:

لَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا بِالْبَيِّنَاتِ وَأَنزَلْنَا مَعَهُمُ الْكِتَابَ وَالْمِيزَانَ لِيَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ ۖ وَأَنزَلْنَا الْحَدِيدَ فِيهِ بَأْسٌ شَدِيدٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَلِيَعْلَمَ اللَّـهُ مَن يَنصُرُهُ وَرُسُلَهُ بِالْغَيْبِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ قَوِيٌّ عَزِيزٌ

“Hakika Tuliwatuma Mitume Wetu kwa hoja bayana na tukateremsha pamoja nao Kitabu na Mizani ili [wawasaidie] watu wasimamie kwa uadilifu. Na Tukateremsha chuma chenye nguvu na manufaa kwa watu na ili Allaah ajue nani atakayeinusuru na Mitume Wake hali ya kuwa ni ghaibu. Hakika Allaah ni Mwenye nguvu kabisa, Mshindi kabisa!”[1]

28- Imepokelewa ya kwamba Ibn ´Abbaas alimuuliza Ka´b:

“Ni vipi ameelezwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Tawraat?” Akasema: “Tunasoma kuwa Muhammad bin ´Abdillaah amezaliwa Makkah. Atahama kwenda Twaabah na ufalme wake utakuwa Shaam.”

Haya yamepokelewa kutoka kwa Ka´b kupitia njia nyingi.

[1] 57:25

  • Mhusika: Imaam ´Abdur-Rahmaan bin Rajab al-Baghdaadiy al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwaa-il-ush-Shaam, uk. 37-41
  • Imechapishwa: 02/02/2017