04. Ibn Rajab kuhusu sherehe ya usiku wa nusu ya Sha´baan

Haafidhw Ibn Rajab (Rahimahu Allaah) amesema kuhusu masuala haya katika kitabu chake “Latwaaif-ul-Maa´arif” kama ifuatavyo:

“Usiku wa nusu ya Sha´baan Taabi´uun katika watu wa Shaam, kama mfano wa Khaalid bin Ma´daan, Mak-huul, Luqmaan bin ´Aamir na wengineo wakiutukuza na wakijipinda kufanya ´ibaadah. Watu walichukua ubora na matukizo yake kutoka kwao. Imesemekana kwamba walifikiwa katika jambo hilo na Aathaar za ki-Israaiyl. Pindi jambo hilo lilipotangaa kutoka kwao katika miji mbalimbali ndipo watu wakatofautiana juu ya jambo hilo. Miongoni mwao wako waliolikubali na wakaafikiana nao katika kuutukuza. Miongoni mwao ni kundi la wafanya ´ibaadah wa Baswrah na wengineo. Wanazuoni wengi wa Hijaaz wakalipinga jambo hilo. Miongoni mwao ni ´Atwaa´ na Ibn Abiy Mulaykah. ´Abdur-Rahmaan bin Zayd bin Aslam akalinukuu hilo kutoka kwa wanazuoni wa Madiynah. Ni maoni ya marafiki zake Maalik na wengineo na wakasema kuwa yote hayo ni Bid´ah. Wanazuoni wa Shaam wakatofautiana kunako maoni mawili kuhusu namna ya kuyahuisha:

1 – Inapendekeza kwa kikosi cha watu kadhaa kusherehekea misikitini. Khaalid bin Ma´daan, Luqmaan bin ´Aamir na wengineo walikuwa wakivaa mavazi yao mazuri kabisa na wakijitia manukato na wanja na wakisimama msikitini katika usiku wao huo. Ishaaq bin Raahuuyah ameafikiana nao katika jambo hilo na kuna jopo wamesema kuwa kusherehekea msikitini kwa mtindo huo sio Bid´ah. Ameyanukuu hayo Harb al-Karmaaniy katika “Masaa-il” yake.

2 – Inachukizwa kukusanyika kwa ajili yake misikitini kwa ajili ya kuswali, kupiga visa na kuomba du´aa. Lakini haichukizwi kwa mtu yeye mwenyewe iwapo ataswali. Haya ndio maoni ya al-Awzaa´iy pia ambaye ni Faqiyh na mwanachuoni mkubwa zaidi wa watu wa Shaam. Maoni haya ndio yako karibu zaidi – Allaah akitaka. Mpaka alipofikia kusema: Hakuna maneno yanayotambulika kutoka kwa Imaam Ahmad kuhusu usiku wa nusu ya Sha´baan. Kuna riywaayah mbili zilizopokelewa kutoka kwake kuhusu mapendekezo ya kuitekeleza. Moja riyaawah hizo mbili kutoka kwake ni kuhusu kuifanya usiku wa kuamkia ´iyd. Katika riwaayah moja hakupendekeza kuitekeleza kwa mkusanyiko. Kwa sababu ni jambo halikunakiliwa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake. Katika riwaayah nyingine akapendekeza kufanya hivo kwa sababu ya kufanywa na ´Abdur-Rahmaan bin Yaziyd al-Aswad ambaye ni katika Taabi´uun. Vivyo hivyo kusimama usiku wa nusu ya Sha´baan hakukuthibiti chochote kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala kutoka kwa Maswahabah zake. Kumethibiti juu yake kutoka kwa kikosi cha Taabi´uun katika wanazuoni mashuhuri wa watu wa Shaam.”

Ndani yake kumewekwa wazi ya kwamba hakukuthibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala kutoka kwa Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum) juu ya chochote kuhusu usiku wa nusu ya Sha´baan.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr minal-Bid´ah, uk. 24-26
  • Imechapishwa: 17/01/2022