Yule mwenye kufuata mfumo wa Salaf anahitajia mambo mawili yafuatayo:

1- Autambue mfumo wa Salaf.

2- Kushikamana nao bila kujali shida utazopata. Mtu atapata maudhi, matusi, tuhuma na majina ya kebehi kutoka kwa wapinzani. Pamoja na hivyo mtu anatakiwa awe na subira juu ya hayo, kwa kuwa yuko na uhakika kwa lile alilomo. Asibabaishwe na kutikiswa. Asubiri kwa hayo mpaka atapokutana na Mola Wake.

Mosi mtu anatakiwa kujifunza mfumo wa Salaf. Pili awafuate kwa wema. Tatu awe na uvumilivu kwa yatayomkumba kutoka kwatu. Haya hayatoshelezi vilevile, ni lazima kuyaeneza madhehebu ya Salaf, ni lazima alinganie katika njia ya Allaah, alinganie katika ´Aqiydah ya Salaf, awabainishie watu, ayaeneze kati ya watu. Huyu ndiye Salafiy wa kihakika. Mwenye kudai Salafiyyah naye hajui mfumo wa Salaf au akawa anatambua lakini akawa haufuati, bali yeye anafuata yale waliyomo watu, au anafuata yale yenye kuendana na matamanio yake huyu sio Salafiy. Haijalishi kitu hata kama atajiita “Salafiy”. Mtu wa sampuli nyingine ni yule ambaye hana uvumilivu wakati wa mitihani. Isitoshe akawa ni mwenye kupakana mafuta kwa ajili ya dini yake, yuko tayari kuacha kitu chenye kuhusiana na mfumo wa Salaf, huyu hana lolote kuhusiana na mfumo wa Salaf. Kinachozingatiwa sio madai matupu, kinachozingatiwa ni uhalisia.

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com