04. Hivi ndivo Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab alivoanza Da´wah yake

Wakati alipotazama hali waliokuwa nayo watu wakati wake akaona tofauti ya wazi kabisa kati yake na yale yaliyomo ndani ya Qur-aan na Sunnah na mfumo wa Salaf inapokuja katika ´Aqiydah na mfumo. Wanachuoni katika wakati wake kwa ujumla walikuwa ni wenye kujishughulisha na Fiqh na falsafa inayokwenda kinyume na ´Aqiydah ya Salaf pasi na kupambanua kati ya kilicho sahihi na kisichokuwa sahihi. Watu wasiokuwa na elimu walikuwa wamefungamana na mambo ya Bid´ah, ya ukhurafi, ya shirki na kuwaomba wafu. Hapakuwepo mwanachuoni yeyote mwenye kuchukua jukumu la kurekebisha uhalisia huu wenye kuuma. Hapo ndipo Shaykh Muhammad (Rahimahu Allaah) hakuweza kuendelea kujizuia na kubadilisha na kukemea. Akaanza kulingania katika kutengeneza na kurudi katika Qur-aan na Sunnah na kuisafisha ´Aqiydah ya Kiislamu iliokuwa imechafuliwa.

Akachukua jukumu la kulingania katika njia ya Mola wake kwa hekima na maneno mazuri na akaanza kulingania katika mji wa baba yake Huraymalaa´. Baada ya muda alifukuzwa ndipo akaenda ´Uyaynah. Hakuwahi huko kupata utulivu, ndipo akaenda Dir´iyyah ambapo akakubaliwa na kukaribishwa na kiongozi  wake Muhammad bin S´uud (Rahimahu Allaah):

وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجًا وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ ۚ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ

“Na yeyote mwenye kumcha Allaah, basi Atamjaalia njia ya kutokea na Atamruzuku kutoka njia ambayo hatizamii na yeyote mwenye kumtegemea Allaah, basi Yeye humtosheleza.”[1]

Akaendelea kulingania kwa Allaah, akiandikiana barua na wanachuoni na viongozi wa miji mingine akiwalingania katika dini ya Allaah. Akiwabainishia mambo wanayoenda kinyume nayo, akiwatungia vitabu na akiwajibu maswali yao ambao haki inawatatiza kutokamana na batili. Wale waliokuwa wanakusudia haki wakaitikia Da´wah ya Shaykh. Wale waliokuwa wakisukumwa na ushabiki wa kipofu wakafanya inda. Matokeo yake Shaykh (Rahimahu Allaah) akaona kuwa ni lazima kupambana na watu hawa kwanza kwa hoja na dalili, kisha baadaye kwa upanga na mkuki chini ya uongozi wa Muhammad bin Su´uud.

Allaah akamtunuku nusura na akaifanya Da´wah yake kuenea. Hiyo ilikuwa ni natija ya maimamu hao wawili, Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab na Muhammad bin Su´uud. Mmoja akipambana kwa hoja na dalili na mwingine akipambana kwa upanga na mkuki. Namna hii pindi vinapokutana upanga wa Qur-aan na Jihaad basi haki hushinda na batili hushindwa. Amesema (Ta´ala):

لَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا بِالْبَيِّنَاتِ وَأَنزَلْنَا مَعَهُمُ الْكِتَابَ وَالْمِيزَانَ لِيَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ ۖ وَأَنزَلْنَا الْحَدِيدَ فِيهِ بَأْسٌ شَدِيدٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَلِيَعْلَمَ اللَّـهُ مَن يَنصُرُهُ وَرُسُلَهُ بِالْغَيْبِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ قَوِيٌّ عَزِيزٌ

“Hakika Tuliwapeleka Mitume wetu kwa hoja za waziwazi na tukateremsha pamoja nao Kitabu na Shari´ah ili watu wasimamie kwa uadilifu na tukateremsha chuma chenye nguvu madhubuti na manufaa kwa watu na ili Allaah ajue nani atakayeinusuru [dini Yake] na Mitume wake hali ya kuwa ni ghaibu. Hakika Allaah ni Mwenye nguvu kabisa, asiyeshindikana.”[2]

Haikuchukua muda mrefu mpaka nchi na watu wakanyenyekea Da´wah ya haki. I´tiqaad ya Tawhiyd ikasimama barabara ndani ya nchi. Kheri zake zikaenea kwenda mpaka sehemu za mbali na vizazi vilivyokuja, ambazo zinaendelea mpaka hii leo. Moja katika matunda yake makubwa ni kusimama kwa nchi ya Tawhiyd. Ikaongoza kwa Shari´ah safi na bado inaendelea kufanya hivo mpaka hii leo, licha ya vizuizi vikwazo vyote vinavyosababishwa na maadui na tuhuma za batili.

[1] 65:2-3

[2] 57:25

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 11-12
  • Imechapishwa: 24/07/2019