04. Hadiyth “Tulikula daku pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)… “


Hadiyth ya nne 

4- Anas bin Maalik amesimulia kupitia kwa Zayd bin Thaabit (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesema:

“Tulikula daku pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kisha akasimama kwa ajili ya swalah.” Anas akasema kumuuliza Zayd: “Kulikuwa muda kiasi gani kati ya adhaana na daku?” Akajibu: “Kiasi cha Aayah khamsini.”

Maana ya kijumla:

Anas bin Maalik anapokea kutoka kwa Zayd bin Thaabit (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Zayd alikula daku pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Miongoni mwa Sunnah zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kwamba alikuwa akila daku kabla ya kuingia alfajiri. Kwa ajili hiyo baada ya kula daku akasimama kwenda katika swalah ya Fajr. Anas akamuuliza Zayd: “Kulikuwa muda kiasi gani kati ya adhaana na daku?” Akajibu: “Kiasi cha Aayah khamsini.”

Faida zinazochukuliwa kutoka katika Hadiyth:

1- Ubora wa kuchelewesha daku mpaka kabla kidogo ya Fajr.

2- Kuharakisha kuswali swalah ya Fajr pale inapofika wakati wa kujizuia.

3- Wakati wa kujizuia ni kule kuingia kwa alfajiri [ya kweli]. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ

“Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu uzi mweupe wa alfajiri kutokana na uzi mweusi. Halafu timizeni swawm mpaka usiku.” (02:187)

Kwa haya tunapata kujua kuwa yale yanayofanywa na watu kuweka nyakati mbili; wakati wa kujizuia na wakati wa kuingia kwa alfajiri ni Bid´ah ambayo Allaah  hakuteremsha dalili yoyote juu yake. Hilo si jengine isipokuwa ni wasiwasi kutoka kwa shaytwaan na shaytwaan anataka kucheza na dini yao. Vinginevyo Sunnah ya kiutume ni kwamba wakati wa kujizuia unakuwa pale kunapoingia alfajiri ya kweli.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdullaah bin ´Abdir-Rahmaan al-Bassaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-´Allaam Sharh ´Umdat-il-Ahkaam, uk. (01/318)
  • Imechapishwa: 25/05/2018