Haafidhw Ibn Hajar al-´Asqalaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

679- Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kuleni daku. Kwani hakika katika daku kuna baraka.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

MAELEZO

Daku ni kula mwishoni mwa usiku kwa yule anayetaka kufunga. Kitendo hicho ni Sunnah, kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekiamrisha, yeye mwenyewe akakifanya na akawakubalia nacho Maswahabah zake. Amekokoteza juu yake akasema:

“Kuleni daku. Kwani hakika katika daku kuna baraka.”

Ameiamrisha, akabainisha faida yake, kwamba ina baraka. Miongoni mwa baraka zake ni kwamba ni kutekeleza amri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kila kitu ambacho kina maana ya kutekeleza amri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi ni kheri na baraka na mtu anahisi matunda yake moyoni, matendo yake, katika kupenda kwake kheri na kadhalika.

Miongoni mwa baraka zake ni kumwingiliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye tumeamrishwa kumfuata. Allaah (Ta´ala) amesema:

“… wa fatabiu tahdatuna” 7:158

Miongoni mwa baraka zake ni kwamba inamsaidia mtu kufunga. Kitu ambacho kinamsaidia mtu katika ´ibaadah hapana shaka kwamba ni kheri na baraka. Mtu anapokula daku basi funga inakuwa nyepesi kwake.

Miongoni mwa baraka zake ni kwamba anakwenda kinyume na mayahudi na wakristo. Kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kipambanuzi kati ya swawm yetu na swawm ya mayahudi na wakristo ni daku.”[2]

Zote hizi ni katika baraka zake. Kwa ajili hiyo wakati tunapokula daku tunatakiwa kufikiria amri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba tunakula kwa ajili ya kutekeleza amri yake, kumwigiliza na kutaraji baraka za chakula hichi. Kwa ajili hiyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameiita:

“Njoo katika chakula cha mchana kilichobarikiwa.”[3]

[1] al-Bukhaariy (1923) na Muslim (1095).

[2] Muslim (1096).

[3] Abu Daawuud (2344) na an-Nasaa’iy (2164). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (2344).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mukhtaswar ´alaa Buluugh-il-Maraam (2/410-413)
  • Imechapishwa: 24/04/2020